Sunday, June 30, 2024

TFF yatakiwa kulipa hadhi soka la Mitaa, Viwanja nyasi bandia

Soka ni miongoni mwa michezo maarufu ulimwenguni na unaopendwa na watu wengi, kazazi cha Karne ya 21 hakiwezi kuwasahau Cristiano Ronaldo wa Ureno na Lionel Messi wa Argentina.

Nyota hawa Wawili wamekuwa katika viwango vya juu siku zote katika maisha Yao ya soka lakini Jambo moja kubwa ambalo wengi huenda hawalipi uzito zaidi ya kuangalia namna wanavyovuna mabilioni ya Shilingi kutokana na kutandaza soka lenye mvuto ni kwamba wote Wawili walitoka katika familia maskini.

Cristiano Ronaldo alitoka katika familia ya baba mlevi kupindukia ambaye alifariki Dunia kutokana na ulevi wake, mama yake alikuwa akifanya kila jitihada kuhakikisha mwanaye anapata fursa ya kucheza mpira na ndoto ikawa kweli.

Lionel Messi alifahamika kwao kwa jina moja la Kiroboto au kwa kihispaniola La Pulga kutokana na ufupi wa kimo licha ya kuzaliwa akiwa na changamoto ya mgongo lakini wazazi wake hawakukata tamaa kumkuza katika soka na ndoto ikawa kweli alipotua katika Akademi ya La Masia.

Mifano hiyo miwili inaweza kuwa mfano mzuri kwa watoto wa Kitanzania ambao wengi wanatoka mazingira duni ambayo hata kununua kiatu cha mpira ni changamoto.

Katika Manispaa ya Moshi kumekuwa na Mashindano ya kandanda ya Mtaa yaliyoasisiwa katika Viwanja vya Railway kwenye Kata ya Njoro ambako Diwani na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Injinia Zuberi Abdallah Kidumo anatokea.

Mashindano hayo maarufu ya kandanda iliyopewa jina la Zuberi Cup Tournament hufanyika baada ya msimu wa soka unaomalizika mwezi Mei kila mwaka unapoisha hivyo wakazi wengi wa Mkoa wa Kilimanjaro hupata fursa ya kujionea vipaji vya kandanda.

Baada ya msimu mitatu kuchezwa mwaka huu tena yameanza ambapo kipute mwaka huu kinashiriki timu 25 huku zawadi ya bingwa itakuwa shilingi milioni tatu za Kitanzania ikiwa ni rekodi ya juu kuwahi kutokea katika michuano ya soka mkoani Kilimanjaro.

Mnamo Juni 16, 2024 katika ufunguzi wa Zuberi Cup Tournament Mgeni rasmi alikuwa Mwasisi wa Michuano ya Kandanda mitaani maarufu Ndondo Cup Shaffih Dauda.

Katika ujumbe wake kwa Watanzania na wapendwa kandanda nchini alitaka Mashindano hayo ya kandanda yanayofanyika katika Mitaa yatambulike rasmi kama sehemu ya kudaka vipaji na kukuza soka nchini.

"Sisi kama wadau wa Mpira wa Mtaani tunaomba mtutambie rasmi sio tuje kuchukua vibali na kutuacha, mtushike mkono, mtutambue jitihada zetu na sisi tupo hapa kwa ajili ya kuwasapoti nyie, hatupo hapa kwa ajili ya kuwatengenezea labda ushindani tupo hapa kwa ajili ya kusapoti mambo mazuri," alisema Dauda.

Dauda aliwataka waratibu wa Mashindano kama hayo kote nchini kuungana pamoja na kutengeneza Taasisi itakayokuwa inatambulika kwa ajili ya kandanda la mtaani ili kuongeza ushawishi nchini.

"Kuna Jambo ambalo naliota siku zote sisi kama waandaji wa Mashindano nchini tuwe na umoja wetu, tutengeneze umoja kwenye mikoa yote ambayo Mashindano yanafanyika uswahilini. Na sisi tuwe na sauti moja kuzungumza kwa pamoja na ikiwezekana tuwe na mipango ya kuboresha," aliongoza Dauda.

Aidha Mwasisi huyo na mchambuzi wa kandanda nchini aliliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutumia mwanya wa serikali kusamehe Kodi katika vifaa vya Taasisi za serikali kupeleka kwa Miradi ya Viwanja vya Nyasi Bandia katika kila wilaya kote nchini.

"Hivi viwanja ambayo viko huku mtaani chini kupitia kwenye uongozi wenu nafikiri kuna haja ya kuviangalia kwa Jicho lingine na kutumia fursa ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa ya kutoa wave ya Kodi ya majani bandia, na huku mtaani, huku uswahilini hatuhitaji hii natural grasses, tunakuhitaji artificial grasses ndio zinatufaa zinakaa muda mrefu katika mazingira yetu," alisisitiza.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Injinia Zuberi Kidumo alisema mchezo wa kandanda unapendwa na watu wengi ulimwenguni hivyo juhudi ni vema kuongeza katika kuyafanya Mashindano ya Uswahilini kuwa sehemu ya ajira, burudani na fursa kwa wachezaji kuipandisha viwango vyao.

Awali Dauda katika ufunguzi alisifu juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuunga mkono sekta ya Michezo nchini.

"Sisi sote ni mashahidi, Ningeomba kwa pamoja tumpigie makofi kuonyesha appreciation kwake kwa kutubeba maana yake ni kwamba amekuwa akihamasisha timu zetu, amekuwa akipambana, Afcon inakuja hapa kwetu ni fursa kubwa kwetu sisi kama Watanzania na kwa vijana ambao wanapata nafasi ya kucheza timu ya taifa baadhi lakini ni jambo kubwa," alisema Dauda.

Imeandikwa na:
Jabir Johnson
+255 693 710 200

0 Comments:

Post a Comment