Wachina wana methali
isemayo, “Wakati mzuri zaidi wa kupanda mti ulikuwa miaka 20 iliyopita. Wakati
mzuri wa pili ni sasa.”
Nchini Uingereza alitokea
mchezaji wa raga kwa jina Nelson Faviell Henderson ambaye alizaliwa tarehe 24
Septemba 1865.
Nyota huyo wa raga
alifariki dunia miaka 80 iliyopita (Juni
16, 1943) na alizikwa huko Blewbury, Berkshire nchini England.
Hakuwa maarufu sana
miongoni mwa wafuatiliaji wa mchezo huo lakini umaarufu wake ulikuja baada ya
siku moja kuhojiwa.
Unajua alisema nini katika
mahojiano hayo? Alisema, “Maana halisi ya maisha ni kupanda miti.”
Nukuu hiyo inaishi hata leo
kutokana na ukweli kwamba miti imekuwa msaada mkubwa katika miasha ya binadamu.
Mnamo Machi 27, 2023 Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango
alisema kupanda miti ni suala la lazima na alizitaka Halmashauri zote nchini
kusimamia kwa karibu na kuhakikisha kwamba mazingira ya maeneo yao yanakuwa ya
kijani, safi na ya kuvutia na zoezi hilo liwe endelevu.
Dkt. Mpango aliyasema hayo wakati akizindua kampeni ya
kupanda miti kitaifa ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), uzinduzi
uliofanyika katika eneo la Mtumba Jijini Dodoma.
Katika uzinduzi wa kampeni hiyo zaidi ya miti 3000 ilipandwa
katika eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Kwanini jamii mbalimbali zinasisitiza suala la upandaji
miti?
Hiyo ni kutokana na faida zinatokana na miti ambazo ni Miti hutoa oksijeni ambayo tunahitaji kupumua.
Miti hupunguza kiwango cha mtiririko wa maji ya dhoruba,
ambayo hupunguza mmomonyoko na uchafuzi wa mazingira katika njia zetu za maji
na inaweza kupunguza athari za mafuriko.
Aina nyingi za wanyamapori hutegemea miti kwa makazi.
Miti hutoa chakula, ulinzi, na nyumba kwa ndege na mamalia wengi.
Pia binadamu wamekuwa wakivuna na kutumia miti kwa
matumizi ya dawa kwa miaka mingi kutokana na changamoto za maradhi mbalimbali.
Hata sasa dawa kutoka kwa miti, nyingine zimekuwa
zikitlewa kutoka kwenye kuni, magome ya miti, mizizi, majani, maua, matunda au
mbegu hayo yote ni msingi kwa ustawi wa mamilioni ya watu.
Katika makala haya tutaangazia namna TFS inavyopambana
kuendelea kuifanya miti kuwa sehemu ya maisha ya binadamu hususani kupanda
miche tiba kwa ajili ya kukabiliana na maradhi mbalimbali ikiwamo tezi dume.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa ugonjwa wa tezi dume
unashambulia wanaume wenye umri kuanzia miaka arobaini (40) na kuendelea, hii
inatokana na kuongezeeka kwa vichocheo vya homoni katika mwili ambavyo
vinasababisha tezi dume kukua na kuathiri kibofu cha mkojo.
Uvimbe wa tezi dume ukiwa mkubwa sana, mgonjwa hushindwa
kukojoa hivyo mkojo kuendelea kujaa kwenye kibofu hali ambayo hulazimu kuwekewa
mrija maalumu kumsaidia kutoa haja ndogo.
Sasa basi TFS imetoa matumaini mapya kwa wagonjwa wa
tezi dume nchini baada ya kuotesha miche tiba ya asili kwa ajili ya kutatua
changamoto hiyo.
Akizungumza katika Shamba la Miti la Rongai lililopo,
North Kilimanjaro Mhifadhi Msaidizi Fred Ng’wavi amesema uoteshaji huo
umefanywa kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti ya Muhimbili (MUHAS)
“Miche tunayozalisha hapa ni ya mbao laini, na miche ya
miti migumu kutoka kwenye misitu yetu ya hifadhi, tulipo tupo katika kitalu cha
miti inayoitwa Brunos Africana ambayo inajulikana kama Mkoma Oyee; ni miti tiba
ambayo inatibu tezi dume na taasisi ya utafiti ya Muhimbili (MUHAS) waliingia
makubaliano na TFS kwa ajili ya kuzalisha hii miche,” amesema Ng’wavi.
Aidha Mhifadhi huyo ameongeza kuwa ndani ya miaka mitano
miche hiyo maarufu kwa jina la Mkoma Oyee itaweza kuoteshwa katika mashamba
mengine ya TFS yenye hali ya hewa kama ya Rongai
Eneo ambalo lilionekana kama linaweza kutunza miti hii
ni shamba letu ambalo kwa kiasi kikubwa miti hii kwenye kitalu hiki kwa hapa
ipo zaidi ya 28,500 tunaisambaza nchi nzima kwenye mashamba ya TFS ili
kurahisisha upatikanaji wa miti tiba aina hii ya Brunos Africana…hivyo kwa
miaka hii ya karibuni kuanzia miaka 10 au mitano tutapata miti mingi,”
ameongeza Mhafidhi huyo.
Wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro wameonyesha kuguswa na
hatua ya TFS na MUHAS kuiona changamoto ya tezi dume nchini na kuitafutia tiba
“Mimi nimelipokea kwa furaha sana na kwa upana kwasababu Tanzania tuna misitu mingi lakini tunashindwa kuitumia; wenzetu ukiangalia kwa mfano China, wa India dawa hizi za miti asili zinawasaidia sana,” amesema Hamad Haule mkazi wa Moshi.
Kwa upande wake Mkazi wa Moshi Samwel John amesema,
“Kwanza kabisa ninashukuru kwa kupata taarifakuwa wataalamu wetu wa tiba asili
wameendelea kugundua dawa ambazo
zinasaidia magonjwa mengi kama tezi dume.”
Mkoma Oyee ni jina maarufu nchini Tanzania ambapo miti
hii inafanana na ile ya Uganda maarufu Warbugia Ugandensis.
Miti hii hustawi zaidi katika eneo la Afrika Mashariki
hivyo TFS na MUHAS wameonyesha njia kwa watanzania wenye maradhi ya tezi dume.
0 Comments:
Post a Comment