MOSHI, TANZANIA.
Timu ya
Kikapu ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU) imetwaa ubingwa wa Ligi ya Mkoa
wa Kilimanjaro baada ya kuibamiza Wakuda
kwa pointi 100-82 katika mchezo wa fainali uliochezwa katika dimba la
Ushirika mjini Moshi.
Katika
mchezo huo wa fainali kulishuhudiwa ufundi mwingi huku MOCU ikionyesha umahiri
mkubwa katika robo ya kwanza na ya mwisho ya mchezo huo.
Licha ya
Wakuda kutawala zaidi katika robo ya pili na ya tatu ya mchezo lakini
hawakuweza kuzuia kasi ya MOCU ambayo imetoa mcheza bora wa mashindano hayo
mwaka huu.
Mashabiki wa
kikapu mkoani Kilimanjaro walisema msimu wa ligi mwaka huu ulikuwa wa kuvutia
na umetoa ari na hamasa kujiandaa kwa msimu mwingine.
Kwa upande
wao Wakuda walisema ubora wa MOCU ndio uliowafanya washindwe kutoboa na kubeba
taji hilo mwaka huu licha ya kupita katika hatua za awali kwa kishindo.
Daniel
Kayusi wa timu ya kikapu ya MOCU ameibuka mchezaji bora wa mashindano mwaka huu
akifikisha pointi 249 nyuma ya mfungaji bora wa msimu huu kutoka Wakuda
aliyefikisha pointi 255 Noel Joseph .
Mratibu wa
Mashindano hayo Emmanuel Constantine alisema msimu wa mwaka huu licha ya
changamoto zake lakini umekuwa ni msimu bora na ametoa wito kwa msimu ujao timu
kujitokeza kwa wingi kushiriki.
Ubingwa wa
kikapu kwa MOCU unakuja baada ya kufanya vizuri katika hatua za awali ambapo
ameweka rekodi ya kushinda michezo yote iliyochezwa kwa mfumo wa nyumbani na
ugenini katika ligi ya timu saba zilizoshiriki msimu huu.
Timu
nyingine zilizoshiriki ni VTI, KCMC, Don Bosco, Kijiji Mashujaa na Hai.
0 Comments:
Post a Comment