Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Tuesday, June 27, 2023

ZUBERI CUP 2023: Boys United, kocha, wachezaji wasimamishwa kushiriki, kisa.....

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Mashindano ya Zuber Cup 2023, katika kikao chake cha Juni 25, 2023 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali Katika Michezo inayoendelea na kufanya maamuzi yafuatayo;


MCHEZO KATI YA BOYS UNITED 1- 2 MANDELA

Katika Mchezo huu Idadi ya Viongozi walioketi katika eneo la benchi la ufundi la Klabu ya Boys United ilizidi uhalisia na utaratibu wa ukaaji katika benchi la ufundi la timu, hali iliyopelekea fujo za Mara kwa mara zilizotokana maelekezo ya kiufundi yenye kutotenganisha benchi la ufundi na mashabiki.


MCHEZO KATI YA MOSKISA 1-1 BOYS UNITED

Wachezaji wa klabu ya Boys United waliovalia jezi namba 17, 18 na 20 katika mchezo huo wakiongozwa na captain wa timu hiyo alievalia jezi namba 3 walionyesha utovu wa nidhamu wa makusudi kwa kugomea maamuzi ya mwamuzi wa kati wa mchezo huo hali iliyosababisha mchezo kusimama kwa muda, vurugu kuu uwanjani, waamuzi kupigwa na kudharilika kwa kusukumwa na kuzongwa.


Aidha anayedaiwa kuwa kocha wa Klabu hiyo (Lumba) alikuwa sehemu ya kuhamasisha wachezaji kutoka uwanjani na kugomea mchezo huo huku akitoa lugha za kejeli na matusi kwa Waamuzi   na baadhhi ya Viongozi wa Kamati ya mashindano haya na Viongozi wengine kutoka MMFA walioingia uwanjani kutuliza ghasia iliyoibuliwa na kundi la wachezaji wa klabu ya BOYS UNITED na huu ni muendelezo wa tabia zake za utovu wa nidhamu katika mashindano haya tangu msimu uliopita.


Kwa maelezo hayo klabu ya Boys United imeondoshwa kwenye mashindano haya msimu huu 2023 na kufungiwa kushiriki mashindano haya mpaka itakavyo amriwa vingenevyo ili iwe funzo kwa vilabu vingine shiriki vyenye hisia za namna hiyo.


Wachezaji wa klabu ya Boys United waliovalia jezi namba 17, 18 na 20 wakiongozwa na Captain wa timu hiyo alievalia jezi namba 3 (Majina yao tunayo) wamefungiwa kucheza Mashindano ya Zuberi Cup kwa siku zote mpaka itakavyoamriwa vinginevyo.


Anayedaiwa kuwa mwalimu wa klabu ya Boys united (Lumba) amefungiwa kushiriki kwa namna yeyote Mashindano ya Zuber Cup


Aidha kiongozi wa Kilimanjaro Rangers Adam Kipacha anapewa onyo kali kwa matamshi yake aliyoyatoa hivi karibuni dhidi ya Waamuzi na Viongozi wa Kamati ya Mashindano haya kupitia mahojiano yake na chombo kimoja cha habari Mkoani Kilimanjaro.


Taarifa za kimaandishi kuhusu maamuzi haya kwa wahusika itawafikia.


Vile vile Waandaji na Waratibu wa mashindano haya wanatoa rai kwa Viongozi wa Vilabu, Wachezaji, Mashabiki na Wadau wote wa mashindano ya Zuber Cup kuzingatia miiko ya soka na dhana ya mchezo wa kiungwana ( Fair Play) ndani na nje ya Uwanja wawapo uwanjani na kinyume na hapo hatua kali za kimaamuzi zitachukuliwa kwa yeyote atakaekiuka maelekezo haya.


Imetolewa na

Kamati ya Mashindano Zuber Cup Tournament 2023 26.06.2023

Saturday, June 17, 2023

Zuberi Cup 2023: Ufunguzi wafana, Mabhiya atoa neno



Michuano ya Soka ya Zuberi Cup 2023 imezinduliwa rasmi leo katika dimba la Railway mjini Moshi huku Bingwa mtetezi Kaloleni akifungua dhidi ya Moskisa Academy.

Mgeni rasmi katika ufunguzi huo ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro Jonathan Mabhiya ambaye aliongoza na viongozi wengine wa chama chake.


Mabhiya amezitaka timu zote zinazoshiriki mwaka huu kujituma huku akisisitiza waamuzi kutenda haki kwa kila timu ili kuyafanya mashindano hayo kuwa mazuri na bora.


Akizungumza kabla ya mchezo wa Kaloleni dhidi ya Moskisa Academy kuanza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo amesema mwaka huu ameboresha zawadi na kwamba hakutakuwa na malalamiko kwani zawadi zote zipo.


Katika kuhakikisha suala la usalama litakuwa vizuri Inspekta Manyasi amewahakikishia  washiriki na mashabiki wote kuwa hali itakuwa nzuri huku akisisitiza mashabiki kuwa na subira pindi wanapoona timu yao haifanyi kama mategemeo yao.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Michuano hiyo mwaka huu Mwalimu Mpande amewahakikishia utulivu na soka safi kwa timu zote zinazoshiriki.


Katika michuano ya mwaka huu timu 25 zitashuka dimbani kuwani taji hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na vijana wa kutoka kata ya Kaloleni.










Wadau wa Moshi 2023

 









Thursday, June 15, 2023

John Heche aichana Serikali sakata la bandari;

 Heche: Serikali ituambie ilikaa wapi na DP World

Kiongozi Mwandamizi wa Chadema John Heche akihutubia umati wa wakazi wa Moshi Mjini Juni 15, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Posta.


Sakata tata la bandari nchini limeendelea kuchukua sura mpya baada ya Mbunge wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tarime Vijijini  kuitaka serikali ya awamu ya sita iwaeleze watanzania ni lini na wapi walikaa na wawekezaji wa DP World kuhusu bandari zilizopo nchini.


Sehemu kubwa ya wale wanaolijadili suala hilo wanaitupia macho bandari ya Dar es salaam ambayo licha ya kutoa huduma zake kwa sehemu kubwa ya Tanzania pia imekuwa kiunganishi muhimu kwa mataifa mengine kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Rwanda, Malawi, Burundi, Uganda na hata Zimbabwe


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Posta mjini Moshi leo Juni 15, 2023 Heche amesema watanzania wanapaswa kuelezwa kwa uwazi kuhusu mahali walipokaa na DP World kuhusu uwekezaji wa bandari za Tanganyika.


"Tunataka serikali ituambie na Rais atuambie huyu mwarabu wa DP World alipatikanaje, walikutana wapi, walikutana kwenye chai akamwambia mimi nina bandari njoo uchukue? walikutana wapi?"


Kiongozi huyo mwandamizi wa Chadema alisema katika mchakato mzima taratibu na kanuni hazijazingatiwa katika suala la mkataba wa Tanzania na DP World


"Kwasababu utaratibu wa serikali kwa mambo kama hayo yalipaswa kutangazwa...sheria ya manunuzi inasema lazima kuwepo na tangazo tenda shindanishi, kwamba  sisi bandari yetu ya Dar es Salaam au bandari nyingine kama mkataba unavyosema kila mmoja aje."


Heche alisisitiza kuwa swali hilo ni la msingi ambalo watanzania wanapaswa walijuaje na serikali iwaambie kwa ufasaha.


"Huyu mtu mliyempa bandari juzi mmempataje mmejuaje kama ofa yake ingekuwa nzuri kuliko mtu mwingine yeyote hilo ndilo swali la kwanza kabla hatujaingia kwenye masuala ya kimsingi yaliyopo kwenye mkataba," 


Hoja zinazoibuliwa kutoka kwa wakosoaji hao ni pamoja na ukomo wa uwekezaji huo, ugumu wa kujitoa kwenye mkataba endapo kutatokea kutoelewana, huku kampuni ya DP World ikidaiwa kuwa na migogoro na baadhi ya mataifa iliyoingia makubaliano katika mikataba kama hiyo.


Katika mkutano huo wa hadhara Heche aliongoza na mbunge wa zamani wa Arusha Mjini Godbless Lema, Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini Jaffary Michael, Mstahiki Meya Mstaafu Raymond Mboya, na Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro Michael Kilawila.











Monday, June 12, 2023

Silvio Berlusconi Is no More, Rambirambi zatolewa

Waziri Mkuu wa zamani wa Italia Slivio Berlusconi amefariki dunia leo Juni 12, 2023 akiwa na umri wa miaka 86.

Mfanyabiashara huyo bilionea aliunda kampuni kubwa zaidi ya vyombo vya habari nchini Italia kabla ya kubadilisha hali ya kisiasa - huku akikabiliana na kashfa nyingi za kisheria na ngono.

Alikuwa ameteseka mara kadhaa ya afya katika miezi ya hivi karibuni. Alilazwa hospitalini mnamo 2020 baada ya kuambukizwa COVID-19, akielezea kama "Huenda ni hali yangu ngumu zaidi maishani yangu".

Mnamo Aprili 2023, madaktari walifichua kuwa alikuwa katika uangalizi mkubwa akiugua saratani ya damu na maambukizi ya mapafu.

Alilazwa katika hospitali ya Milan siku ya Ijumaa kwa kile wasaidizi walisema ni vipimo vilivyopangwa vilivyohusiana na saratani yake ya damu.

Kifo cha Berlusconi kinaacha simanzi kwa sababu alikuwa mtu mashuhuri, waziri wa ulinzi wa Italia Guido Crosetto alisema kwenye Twitter siku ya Jumatatu.



Tuesday, June 6, 2023

PICHA: Ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM-Mawenzi, Moshi

 

Shule ya Msingi Mawenzi ikiwa katika maboresho baada ya kutengewa kiasi cha Shilingi Mil. 60 ambazo zitatumika kukarabati vyumba sita vya madarasa. Hata hivyo katika ziara hiyo iliyoongozwa na Diwani wa Kata ya Mawenzi Apaikunda Naburi waliukataa mradi huo.











Wajumbe wa Kamati ya Siasa Kata ya Mawenzi Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamesema hawajaridhishwa na vifaa vilivyo nunuliwa kwa ajili ya kuwekwa kwenye vyumba vya madarasa shule ya msingi Mawenzi, kutokana na vifaa hivyo kuwa chini ya viwango.

Aidha Wajumbe hao wamesema endapo vifaa hivyo vitawekwa bila kubadilishwa hawatakuwa tayari kuupokea mradi huo na kumwagiza Mkuu wa shule ya Msingi Mawenzi pamoja na Mhandisi wa ujenzi, kuhakikisha vifaa hivyo vinabadilisha na kuletwa vipya ili viendane na thamani ya fedha.

Akizungumza katika eneo la tukio Diwani wa Kata ya Mawenzi Apaikunda Naburi, ameonesha kusikitishwa na madirisha yaliyonunuliwa kwa ajili ya kuwekwa kwenye vyumba vya madarasa sita yanayokarabatiwa katika shule ya Msingi Mawenzi kwani hayaendani na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na seriakli kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo.

Apaikunda Naburi alisema, serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya ukarabati wa vyumba sita vya madarasa shule ya msingi Mawenzi na  kwamba katika ukaguzi walioufanya wamebaini kukuta madirisha ambayo yamenunuliwa yakiwa chini ya viwango.

Naburi alisema katika ziara hiyo pia Wajumbe hao walitembelea mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa shule ya msingi Uhuru, ujenzi wa ofisi ya Kata na ukarabati wa   kituo cha walimu Mawenzi (TRC), na kuridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo.

Akizungumza Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Kata ya Mawenzi Thomas Temu, alisema Kamati haijaridhishwa na ubora wa madirisha yaliyotengenezwa kwani hayalingani na thamani ya fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na kumshauri mhandisi wa ujenzi pamoja na mwalimu mkuu wa shule hiyo, kuyaondoa, ili yaweze kutengenezwa madirisha mengine ambayo yataendana na thamani ya fedha ambazo zimetolewa na serikali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mawenzi Mujibu Abeid, alisema ziara hiyo ilikuwa imelenga kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya kata hiyo.

Aidha alisema wajumbe wa kamati hiyo, walitembelea miradi mitatu ukiwemo, mradi wa ukarabati wa shule ya msingi Mawenzi na kubaini kasoro hizo na kwamba wajumbe wameyatolea maelekezo ya changamoto  zilizojitokeza.
Akizungumza Ofisa Elimu Kata ya Mawenzi Herry Christopher alisema Kata ya Mawenzi imepokea takribani shilingi milioni 200 ambapo fedha hizo zinakwenda kujenga na kukarabati miundombinu kwenye sekta ya elimu ndani ya kata hiyo.

"Tunaipongeza serikali kwa kutoa fedha hizi ambazo zinakwenda kutatua changamoto ya mlundikano wa wanafunzi madarasani kwenye shule jambo ambalo lilikuwa linasababisha walimu kushindwa kuwafundisha wanafunzi vizuri na kuweza kumuelewa,"alisema.

TANROADS Kilimanjaro yakaidi agizo la Waziri wa Uchukuzi

 

Lori la Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga likizuiwa katika mizani ya Njiapanda, Moshi kutokana na kuzidisha uzito.

Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoani Kilimanjaro Mhandisi Motta Kyando, anadaiwa kukaidi amri ya waziri wa uchukuzi Makame Mbarawa wa kuliachailia gari la halmashauri ya wilaya ya Mwanga, mkoani humo.


Kwa mujibu wa uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mwanga, wamesemalori hilo limezuiliwa katika mizani ya Njiapanda, wilaya ya Moshi kwa madai ya kuzidisha uzito.


Akiongelea swala hilo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mwanga Mwajuma Nasombe amesema lori hilo linashikiliwa kwa zaidi ya wiki mbili sasa, licha ya kuwaomba waliachie huku wakitafuta hela za kulipa faini hiyo jambo ambalo limekuwa shubiri.


“Lori hili tulilinunua ili kuongeza mapato ya halmashauri kwa kusambaza madini ya mchanga pamoja na vifaa vya ujenzi kwa wateja mbalimbali zikiwemo taasisi za umma”, alisema Nasombe.


Alisema “Gari hili lilipata kazi ya kupeleka mchanga wilaya ya Rombo kwa ajili ya shughuli zinazofanywa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini TARURA, lakini lilipofika mizani ya Njiapanda lilonekana kuzidisha mzigo,  na hivyo kuzuiliwa kwa zaidi ya wiki mbili sasa”, alisema.


Mkurugenzi huyo aliendelea kusema ziko juhudi mbalimbali zilizofanywa na uongozi wa halmashauri hiyo ili liweze kuachiliwa na kuendelea na shughuli huku uongozi wa halmashauri hiyo ukitafuta fedha za kulipa faini wanayodaiwa kwa kuzidisha uzito bado hazijafanikiwa hadi sasa. 


“Tumewasiliana na wenzetu wa Tanroads ofisi ya Mkoa wa Kilimanjaro ili waliachilie lakini haujafanikiwa”, alisema Nasombe.


Alisema kuwa uongozi wa halmashauri uliwasiliana na Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, kuhusiana  na sakata hilo lakini pamoja na kufanya hivyo bado swala hilo halijaweza kutatuliwa.


“Mbunge aliwasiliana  na  Waziri wa Uchukuzi na taarifa tulizo nazo ni kuwa aliwasiliana  na uongozi wa Tanroads mkoa wa Kilimanjaro, kuhusiana na  swala hilo ikiwemo Tanroads waliachilie lakini hadi sasa halijaachiliwa kutokana na Meneja wa Tanroads kutokutekeleza agizo la Waziri Mmbarawa”, alisema.


Alipotakiwa kuzungumzia swala hilo, Meneja wa Tanroads mkoani Kilimanjaro Mhandisi Kyando alisema swala hilo ni la kiofisi na kushangazwa na kuhojiwa na mwandishi  wa habari alipopata taarifa hiyo.


“Umeona hiyo ndiyo stori, au wamekutuma uwasemee? Zipo taratibu za kiserikali za kuwasiliana na si kupitia kwa mwandishi wa habari”, alisema Kyando pale alipotakiwa na mwandishi wa habari hizi kuzungumzia swala hilo. 


Kwa upande wao baadhi ya Madiwani wa halmashauri hiyo wameelezea kusikitishwa kwao na swala hilo ambalo walisema hata kama kuna kasoro zilizojitokeza, linaweza kushughulikiwa bila mikwaruzo haswa ikitiliwa maanani ya kuwa Tanroads, Tarura na halmashauri ya Wilaya ya Mwanga zote ni taasisi za serikali. 


Akizungumzia sakata hilo, Diwani wa Kata ya Kigonigoni Jeremiah Shayo alisema kuendelea kushikiliwa kwa lori hilo kunaweza kuisababishia halmashauri hiyo hasara kubwa.


“Lori hili linatumia mfumo wa umeme, likiendelea kukaa muda mrefu tena likiwa na mzigo mfumo wa uendeshaji wake utaharibika na kuisababishia serikali kupitia halmashauri ya Mwanga kupata hasara kubwa”, alisema Shayo.



Thursday, June 1, 2023

Beta Charitable Trust, Lions Club zasaidia wazee 120 kupima macho Kilimanjaro

Taasisi isiyo kuwa ya kiserikali ya Beta Charitable Trust ya nchini Uingereza kwa kushirikiana na Lions Club Tanzania, wametoa ufadhili wa huduma ya matibabu ya uchunguzi wa kupima macho bure kwa wazee 120 , lengo likiwa ni kuwawezesha watu wenye vipato vya chini kupata huduma hiyo.

Hayo yamebainishwa Juni 1,2023 na Kiongozi Mkuu wa Lions Club Tanzania Mustansir Ghulam Hussein wakati wa akizungumza na wazee waliofika kutibiwa katika hospitali ya Kibosho, iliyoko Wilaya ya Moshi

Taasisi ya Beta Charitable Trust kwa kushirikiana na LionsClub Tanzania, imedhamiria kutoa huduma za matibabu bure kwa wananchi wenye matatizo ya mtoto wa jicho, hivyo  wanashirikiana na wataalamu wa afya kutoka hospitali ya Kibosho, ambapo zaidi ya wazee 120 watapatiwa matibabu bure ya upimaji wa macho pamoja na upasuaji.

Amesema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Mei 2023 zaidi ya watanzania 1,000 kutoka Mikoa mbalimbali hapa nchini wamepatiwa matibabu ya bure ya macho kupitia taasisi hiyo.

Aidha amesema katika mkoa wa Shinyanga wilaya ya Kahama taasisi  hiyo iliweka kambi na kutoa huduma ya bure kwa wazee 333 wenye matatizo ya macho na kwamba wanatarajia kuweka kambi ya namna hiyo katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza ambako hadi sasa takwimu zinaonyesha kuwa takribani wazee 250 wamebainika kuwa na changamoto hiyo ya macho.

Kwa upande wake Katibu wa Lions Club Moshi Kibo Inderjeet Rahan ‘NITU’ ameushukuru uongozi wa hospitali ya Kibosho kwa kukubali kuwapokea wazee hao na kuweza kuwapatia matibabu hayo, huku pia akiishukuru taasisi ya Beta Charitable Trust, kwa kukubali kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia matibabu hayo kwa wazee.

Awali akizungumza Daktari bingwa wa macho Christian Mlundwa kutoka hospitali ya Kibosho na Matroni wa hospitali hiyo Sister. Francis Okido wameishukuru taasisi hiyo kwa kuona umuhimu wa kugharamia matibabu hayo kwa wazee.

Aidha wamesema  wagonjwa wengi wanaofika kupata matibabu ya macho wengi wao wanasumbuliwa na tatizo la mtoto wa jicho, ambapo alishauri jamii hiyo kujenge utaratibu wa kufanya uchunguzi wa macho mara kwa mara ili wanapopatikana na tatizo watibiwe kwa mapema ili kuepuka changamoto kubwa zaidi ikiwemo upofu.

Wakizungumza baadhi ya wagonjwa wa macho waliofika kupata huduma hiyo, Michael Massawe Peter Oisso na Suzi Shayo, wameishukuru taasisi ya Beta Charitable Trust kwa kufadhili matibabu hayo na kusema kuwa hatua hiyo itawasaidia kuondokana na tatizo hilo ambalo hivi sasa linawasumbua wazee wengi.