Thursday, November 19, 2020

Taswira ya mashindano ya kikapu CRDB Taifa Cup 2020

Miongoni mwa mechi hatua ya makundi CRDB Taifa Cup 2020 baina ya Pemba na CRDB Youth katika viwanja vya Chinangali, Dodoma. (Picha na Michuzi Blog)

MCHEZO wa kikapu ulivumbuliwa mnamo mwaka 1891 nchini Marekani na raia wa Canada aitwae James Naismith. Alikuwa ni mwalimu. Alibuni mchezo huo kuchezwa ndani ya jengo (indoor) ili kuepukana na baridi katika jimbo la Massachusetts alipokua akifundisha kama mwalimu wa mazoezi.

Naismith ambaye alizaliwa huko Almonte, Canada West ambayo kwa sasa ni sehemu ya jimbo la Mississippi Mills huko Ontario nchini Canada mnamo Novemba 6, 1861. Aliubuni mchezo wa kikapu akiwa na umri wa miaka 30 tu.

Hata kama Naismith alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78 mnamo Novemba 28, 1939 lakini chachu ya mchezo huo imesambaa duniani kote. Afrika imekuwa miongoni mwa mabara ambayo yamenufaika na uvumbuzi wa raia huyo wa Marekani mwenye asili ya Canada.

Ugunduzi wake ulikuwa na maana pale Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa ilipouingiza mchezo huo kuwa miongoni mwa michezo ya olimpiki mnamo mwaka 1904 na kuonekana katika mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto ya mwaka 1936 jijini Berlin.

Pia Naismith aliona maendeleo ya mchezo huo pale ambapo kulizaliwa Mashindano ya Kitaifa mnamo mwaka 1938 na Mashindano ya Vyuo nchini Marekani  (NCAA) mnamo mwaka 1939. Aliondoka Ontario na kwenda zake kutafuta maisha huko Springfield, Massachusetts ambako alibuni mchezo huo.

Sasa Tanzania inaendelea kufaidika na mchezo wa kikapu kutokana na uvumbuzi wa Naismith ambapo mashindano mbalimbali yamekuwa yakifanyika katika ardhi ya Tanzania ambapo mwaka huu tangu Novemba 12, 2020 Mashindano ya Taifa ya Kikapu yalianza kutimua vumbi katika jiji la Dodoma kwa udhamini mkubwa wa Benki ya CRDB.

Siku ya Ufunguzi wa CRDB Taifa Cup 2020 Novemba 12.

Kutokana na heshima na uzalendo wa benki hiyo Shirikisho la Kikapu la Tanzania (TBF) ambalo kwa sasa lipo mikononi mwa Phares Magesa liliyapa mashindano hayo jina la CRDB Taifa Cup 2020. Aidha mashindano hayo yanabebwa na Kauli Mbiu “Ni Zaidi ya Game Ni Maisha.”

Viwanja vya Chinangali vimekuwa wenyeji wa mashindano hayo ambayo bingwa atapatikana Novemba 21, 2020; Timu mbalimbali za mikoa zinaendelea na juhudi za kusaka taji la ushindi wa michuano ya mwaka huu.

BUSARA ZA SPIKA NDUGAI

Ufunguzi wa mashindano hayo ulifanyika Novemba 12, majira ya jioni  ikiwa ni saa chache baada ya bunge la 12 kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. 

Spika Job Ndugai alikuwa mgeni rasmi wa ufunguzi wa mashindano hayo alipongeza udhamini wa benki ya CRDB na juhudi kubwa za TBF kutafuta wadhamini ili kufanikisha mashindano hayo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Pia Spika Ndugai alitoa kilio chake kwa wadhamini kuwa changamoto ya vifaa vya michezo kwa timu mbalimbali hususani kwa zile zinatoka vijijini.

UWEPO WA WASANII WA MUZIKI

Wasanii Joh Makini na Moni Centrozone walinogesha uzinduzi huo uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa jijini Dodoma. Pia mbunge wa Muheza na msanii wa kizazi kipya Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA alikuwepo katika ufunguzi wa mashindano hayo. MwanaFA aliingia viwanjani Chinangali akiongoza na mbunge mwenzake wa Tanga Mjini Ummy Mwalimu ili kuonyesha uzalendo wao kwa timu ya mkoa wa Tanga na taifa kwa ujumla katika mchezo wa kikapu.

MATOKEO YA UWANJANI CHINANGALI


Novemba 18 mwaka huu Timu ya Kikapu ya mkoa wa Kigoma ilipata ushindi wake wa kwanza katika mashindano hayo baada ya kuizabua Simiyu kwa alama 58-50. Ushindi huo ulipokelewa kwa shangwe na kocha wa timu hiyo Mazinda Malanja baada ya kupoteza michezo mitatu mfululizo.

Kigoma ilianza mashindano hayo ikipoyeza dhidi ya Manyara mwishoni mwa juma kwa kichapo cha alama 67-54 ikiwa ni mwendelezo baada ya kupoteza dhidi ya Pwani na Mwanza.

Kwa upande wao Simiyu walipoteza dhidi ya Pwani na Kigoma huku matumaini yao yakiibuka baada ya kuichapa timu ya mkoa wa Manyara katika mashindano hayo.

Ilala waliendeleza wimbi lao la ushindi baada ya kuitandika Rukwa kwa pointi 70-61 huku Tanga wakiikung’uta Mtwara kwa pointi 88-53

Hadi sasa Ilala inasalia kuwa timu iliyoanza mashindano hayo kwa kasi kubwa baada ya ushindi wake wa ufunguzi wa alama 114-73 dhidi ya Tabora ambao haujafikiwa na timu yoyote mpaka sasa kwenye mashindano hayo.

Wenyeji wa mashindano hayo Dodoma walianza vibaya dhidi ya Songwe baada ya kuzabuliwa kwa alama 75-72

Awali droo ya mashindano hayo ilichezwa makundi manne yalipangwa ambapo kwa timu za wanaume; Kundi A: Ilala, Katavi, Rukwa, Kilimanjaro, Shinyanga, Tabora; Kundi B: Kigoma, Simiyu, Manyara, Mbeya, Mwanza, Pwani; Kundi C: CRDB Youth, Dodoma, Mtwara, Songwe, Tanga; na Kundi D: Arusha, Iringa, Pemba, Singida, Temeke, Unguja

Kwa timu za wanawake Kundi A: Mwanza, Iringa, Morogoro, Pwani; Kundi B: Arusha, Dodoma, Singida, Temeke; Kundi C: CRDB Youth, Mbeya, Tanga, Unguja.

Kanuni ya mashindano inasema kila kundi litatakiwa kutoa timu mbili kwenda katika hatua ya robo fainali ambapo mpaka makala haya yanaandikwa kwa timu za wanaume za Rukwa na Ilala za kundi A na Temeke ya kundi D zilikuwa tayari zimeshajikatia tiketi kwenda katika hatua ya nane bora huku timu za wanawake za Pwani na Mwanza zilikuwa tayari zimetinga hatua hiyo

Wadhamini wa kuu benki ya CRDB wametoa kiasi cha shilingi milioni 200 kwa timu 36 za Tanzania Bara na Zanzibar. Mkurugenzi wa Mahusiano wa CRDB Tully Mwambapa alisema benki hiyo inatekeleza kwa vitendo sera ya michezo ili kuibua vipaji, kutoa ajira, na kukuza uchumi kupitia sekta ya michezo

Makala haya yametayarishwa na Jabir Johnson, mwandishi wa habari na mtangazaji nchini Tanzania; Novemba 18, 2020

0 Comments:

Post a Comment