Tuesday, November 17, 2020

Falsafa ya Stalin na mustakabali wa kumaliza tofauti Jimbo la Tigray, Ethiopia

 
Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka kwa muda mrefu na uhusiano baina ya Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (TPLF) na Serikali Kuu umezorota kabisa.

Mzozo unaoendelea nchini humo unaonekana kuchukua taswira mpya baada ya matukio ya mashambulizi kadhaa ya viwanja vya ndege pia ufyatuaji wa maroketi katika jimbo jirani na kutua katika mji mkuu wa nchi jirani ya Eritrea yanayoongozwa na TPLF.

TPLF ilitawala Jeshi la Ethiopia na maisha ya kisiasa kwa miongo kadhaa kabla ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed Ali kuingia mamlakani mwaka 2018 na kupitisha mageuzi mkubwa.

Hivi karibuni Bunge la Ethiopia lilipitisha kwa wingi wa kura mchakato wa kubadilisha muundo wa nguvu za utekelezaji huko Tigray baada ya kuibuka kwa mapigano baina ya harakati hiyo na wanajeshi wa serikali kuu.

Mnamo mwaka 2019 Abiy alivunja muungano tawala, unaojumuisha vyama vilivyoundwa kwa misingi ya kikabila na kuviunganisha katika chama kimoja cha kitaifa cha Prosperity ambapo TPLF walikataa kujiunga.

Utawala wa Tigray unayona mageuzi ya Abiy kama jaribio la kujenga mfumo wa serikali moja na kuharibu mfumo uliopo sasa wa shirikisho.

Pia kukasirishwa na kile wanachodai kuwa urafiki wa Waziri Mkuu na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki “usiokuwa na kanuni”.

Abiy ambaye alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2019 kwa juhudi za kuleta amani kwa kumaliza mzozo wa muda mrefu wa nchi yake na Eritrea, anadai kuwa maofisa wa TPLF wanadharau mamlaka yake.

Abiy aliamuru mashambulio ya kijeshi dhidi yao baada ya kusema kuwa wapiganaji wa TPLF wamevuka “mstari wa mwisho mwekundu” na aliwashutumu viongozi wa kushambulia kambi ya kijeshi ya vikosi vya shirikisho mnamo Novemba 4.

Katibu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa ujumbe wake akieleza wasiwasi wake kuhusu matukio ya Tigray huku akitoa wito wa kusitisha mara moja mapigano hayo sambamba na kutoa fursa ya kuanza mazungumzo ya amani ili kupata ufumbuzi wa mzozo huo.

MAPAMBANO YA TIGRAY NA FALSAFA ZA STALIN

Baada ya kifo cha mwanafalsafa wa Urusi Vladimir Lenin mnamo mwaka 1924 kiliwaacha washirika wa Ukomunisti Joseph Stalin, Leon Trotsky na Nikolay Bukharin kama viongozi waliobakia kusimamia falsafa hizo kwa tiketi ya All Russian Communist Party.

Hata hivyo Lenin aliwaonya wanachama wa chama chake kuhusu matarajio aliyonayo Stalin. Stalin akapokea mikoba na anajulikana kutokana na utofauti wake na Lenin katika kuchukua hatua. Stalin aliandika kazi zake ikiwamo ile ya “Voprosy leninizma” (1926; Matatizo ya Falsafa za Lenin).

Kazi hizo zilionyesha mwelekeo mzima wa Stalin katika utawala wake. Stalin alionyesha ni kwa namna gani taifa linatakiwa kuwa.

Mwandishi wa Kitabu kiitwacho “A Political History of the Tigray People’s Liberation Front” na mwanzilishi wa vuguvugu la TPLF Dkt. Aregawi Berhe anasema Stalin aliweka misingi ya taifa kuwa na nguvu kabla halijaondolewa.

Lazima kuwepo na juhudi za makusudi kuhakikisha uimara huo unalindwa “….the state must be strong,” ili kuondoa uwezakano wa maadui wa ujamaa waliopo ndani na nje ya taifa husika.

Dkt. Berhe anasisitiza kuwa TPLF wakati inaanzishwa Februari 18, 1975 ilijikita katika falsafa za Stalin ambaye alipokea mikoba ya watangulizi wake Lenin na Karl Marx hususani katika kipengele cha kujitawala (self-determination).

Katika manifesto (mwongozo) ya TPLF ya mwaka 1976 inasisitiza kuhusu kujitawala. Hata hivyo Dkt. Berhe anasema, “kujitawala kwa TPLF kulikuwa na maana ya kuwa na eneo la binafsi la utawala katika Ethiopia na eneo hilo ni Tigrai ambalo litakuwa na kidemokrasia.”

Dkt. Berhe anasisitiza kuwa kinachoendelea kwa sasa katika Tigray ni kutokana na kuathiriwa na misimamo ya Stalin ya kutaka kujitawala kwa misingi ya ukabila (ethnicity), “Ukabila umekuwa ni itikadi ya kitaifa na imeshika hatamu. Hivyo TPLF wanaona wao wana haja ya kuiunda upya Ethiopia na kuyaunganisha makundi mengine ya kikabila ambayo yameonekana kutokuwa na nguvu kwa miongo kadhaa.”

Hata hivyo msimamo huo wa Dkt. Berhe unaopingwa na wanataaluma wengine Dereje Feyisa na Prof Jon Abbink ambao wote kwa pamoja wanadai kuwa Ethiopia ina makundi madogo madogo ya kikabila ambayo yamekuwa yakijikusanya ili yajitawale.

Wanataalamu hao wanaongeza kwamba kiu ya makundi hayo kutaka kujitawala yatasababisha kujiondoa (seccession) na kujitenga na mfumo wa kisiasa uliopo sasa kama Tigray walivyo kwa ajili ya kutafuta namna ya kushika hatamu katika taifa hilo lenye historia kubwa barani Afrika.

TPLF, harakati hiyo imekuwa ikifahamika na watu wa Tigrai wanaopatikana Kaskazini Magharibi mwa Ethiopia kama Wayane.

Tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1975 ndani ya miaka 16 ya mwanzo TPLF ilikuwa na wanaume wengi ambao walijiunga na kulifanya kuwa kundi kubwa la harakati nchini humo.

Ujio wa TPLF uliyaibua makundi mengine ya muungano kama EPRDF ambalo lilishika taifa hilo kutoka mwaka 1989 hadi 2018.

Itakumbukwa kwa msaada wa harakati ya ukombozi ya Eritrea (EPLF), EPRDF ililivamia na kuliweka chini ya utawala wake kundi la PDRE, hatua ambayo iliunda serikali mpya kutoka Mei 28, 1991 nchini Ethiopia hadi ambapo uundwaji wa chama kipya cha Kitaifa cha Prosperity kilipoundwa mnamo mwaka 2019. TPLF ilikataa kujiunga katika chama hicho kipya ambacho hadi sasa kimedumu takribani mwaka mmoja.

Aidha Clapham katika maandiko yake (Clapham 2002:38) kuhusu hali ya kisiasa nchini Ethiopia anasema, “Historia ya Ethiopia…imejikita hivyo kuwa historia ya taifa, na imekuwa ikionyesha kupanda na kushuka kwa kile kinachoonekana uundwaji wa mamlaka za kisiasa.”

Hali hiyo imekuwa ikizidisha shauku ya kila kundi la watu wenye itikadi zinazofanana za kikabila kutaka kujitawala hivyo kuleta ugumu kwa viongozi wa serikali kuu ya Ethiopia kutatua mizozo hiyo kutokana na kuathiriwa na falsafa za Stalin na historia ya taifa hilo kwa ujumla.

Kulingana na Harold G. Marcus katika kitabu chake cha ‘A History of Ethiopia’ uk. 222 anaandika kuwa Ethiopia ilikuwa na majimbo 14 kabla ya mwaka 1991 ambayo ni Eritrea, Gonder, Tigray, Welo, Gojam, Welega, Shewa, Arsi, Ilubabor, Kefa, GamoGofa, Harerge, Bale na Sidamo.

Aidha Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) mnamo mwaka 1996 katika maandiko yake ‘Emergency Unit for Ethiopia’ liliandika uwepo wa majimbo tisa (9) mapya ambayo ni Tigray, Beni Shangul, Amhara, Afar, Harar, Oromya, Somali, Gambela na Southern Region.

Dkt. Berhe anasema shinikizo kutoka nje ya mipaka ya Ethiopia limekuwa kubwa hususani namna harakati ya wananchi ya Ukombozi wa Eritrea (EPLF) ambayo ilizaa taifa hilo la Eritrea ambalo zamani lilikuwa mojawapo ya majimbo ya Ethiopia.

“EPLF imekuwa ikitoa shinikizo kubwa kwa TPLF kutaka kujitenga,” anasema Dkt. Berhe.

Hata hivyo anasisitiza kuwa hakuna shaka kuwa mashinikizo ya nje yamekuwa kiungo muhimu katika migogoro nchini Ethiopia na maeneo ya jirani.

“Tunahitaji kufanya upembuzi kama matokeo ya mashinikizo hayo ya nje tunaweza kuyatumia kwa namna chanya kwa ajili ya kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe na machafuko ya kisiasa badala ya kuendelea kwa migogoro isiyoisha ya kikabila,” anaongeza Dkt. Berhe

Makala haya yametayarishwa na Jabir Johnson kwa msaada wa vitabu, mitandao ya kimataifa na mashirika ya habari.

0 Comments:

Post a Comment