Thursday, January 10, 2019

Tshisekedi atangazwa rasmi Rais wa DR Congo

Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo ametangazwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na tume ya uchaguzi baada ya kuchelewesha matokeo ya uchaguzi kwa muda mrefu. 

Jana kabla ya kutangaza matokeo hayo Polisi wa kuzuia fujo wakiwa na mizinga ya maji ya kuwasha na magari ya kijeshi waliyazunguka makao makuu ya tume ya uchaguzi kabla ya kutangazwa.  

Matokeo hayo ambayo yametangazwa yamepingwa vikali na Martin Fayulu ambayo alionekana kupata uungwaji mkono wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi wa Desemba 30.

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo Corneille Nangaa ametangaza kuwa Tshisekedi ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 38.57 ya kura zaidi ya milioni 18 zilizopigwa.  

Tshisekedi mwenye umri wa miaka 55 amepata kura milioni saba zaidi ya zile za Fayulu ambaye amepata kura milioni 6.4; Emmanuel Ramazani Shadary ambaye alichaguliwa na Joseph Kabila kuwania nafasi hiyo ameshika nafasi ya tatu kwa kura milioni 4.4 

Kwa upande wake Tshisekedi ameahidi kurudisha utawala wa sheria, kupambana na magenge ya rushwa na kurudisha amani katika eneo la mashariki lenye utajiri mwingi wa madini. 

Uchaguzi huo unakuwa wa kwanza wa kidemokrasia tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1960 kutoka kwa Ubelgiji na Kabila anatarajiwa kuondoka ikulu baadaye mwezi huu.

0 Comments:

Post a Comment