Tuesday, October 9, 2018

RON W. DAVIS: Kocha wa Riadha aliyemfundisha Filbert Bayi, anayehusudu vipaji vya Afrika-1

Ron Davis
DAR ES SALAAM, TANZANIA
Michuano ya Olimpiki mwaka 1968 ilifanyika nchini Mexico kuanzia Oktoba 12 hadi 27, 1968. Hii ilikuwa michuano ya kwanza kufanyika katika ardhi ya watu wanaozungumza Kihispaniola. 


Raia wa Mexico waliandamana kupinga michuano hiyo hatimaye ilifanyika. Nchi 112 zilishiriki huku Afrika Kusini ikitolewa kutokana na ubaguzi wa rangi. 


Ubaguzi wa mtu mweusi ulikuwa ukinuka kila kona. Tukio ambalo litakumbukwa ni lile lililotokea siku nne baada ya michuano hiyo kuanza, pale Wamarekani wenye asili ya Afrika Tommie Smith na John Carlos wakiwa wamechukua medali ya dhahabu na shaba kwenye mita 200 kwa wanaume walipoonyesha kupinga ubaguzi kwa vitendo. 


Wakati walipoenda kuchukua medali zao walivaa glovu nyeusi na soksi na walipopanda jukwaani hawakuwa na viatu, na walikuwa wamevaa badges za haki za binadamu na wakapanda jukwaani na kuinamisha vichwa vyao huku wakinyanyua mkono uliokuwa umevaa glovu wakati wimbo wa taifa wa Marekani ukiimbwa. 


Aidha mwanariadha wa Australia Peter Norman aliwaunga mkono kwa mapambano hayo. Kwa kitendo hicho walifungiwa maisha kutoshiriki michezo. 


Sasa Tommie na John waliporudi Marekani walienda kukutana na kocha Ron Davis ambaye aliona ni vema akikutana nao, wakati huo alikuwa mkurugenzi wa Michezo na Sanaa Edmonton, Canada na kuzungumza nao. 


Katika makala haya tutamulika maisha ya kocha Ron Davis ambaye alionekana nchini Tanzania kwa mara ya pili Septemba 2018 na namna alivyokutana na mkongwe wa riadha Filbert Bayi aliweka rekodi ya dunia mbio za mita 1500.

RON DAVIS NI NANI?
Alizaliwa Februari 7, 1941 New York City nchini Marekani kwa wazazi William Davis na Rhoda Scott.
Wazazi wake walikuwa wakiishi Baltimore huko Maryland. Sababu zilizowafanya waishi Baltimore ilikuwa kutafuta fursa bora za ajira. Ron katika maisha yake akiwa Baltimore alikuwa akiishi na mama yake na wadogo zake wawili wa kiume Chester na Frank. 


Wazazi wake walikaa pamoja kwa miaka 16 kabla ya kutengana. Sababu kubwa za kutengana ilikuwa ni ulevi wa kupindukia wa baba yake ambao hatimaye aliishia jela ya Sing Sing. 


Ron alikaririwa akisema kuwa mama yake alikuwa akipambana kwa hali na mali hadi kuwapata na kuwalisha watoto wake watatu lakini hatimaye aliishia kupata talaka wakati baba yake akiwa jela.
Kabla ya hapo mama yake akiwa katika Chuo Kikuu cha Temple ambako alikutana na baba yake wakati akiwa anafanya kazi katika Hospitali moja jijini New York. 


Baada ya talaka mama yake aliishia kufanya kazi za ndani na kupika katika familia moja ya Kiyahudi huko Manhattan jijini New York. 


Hata hivyo hakukaa sana akiwa Manhattan alikutana na mwanaume mmoja kutoka Stratford mjini Connecticut hivyo ikabidi wahamie Stratford. 


Akiwa Connecticut, Ron Davis alianza shule ya chekechea huku mama yake akimpangia mbali na kusoma alimtaka awe anafanya mazoezi ya Saxaphone hivyo ilimpa hamasa ya kujiingiza kwenye michezo.

Akiwa na wajumbe wa riadha Tanzania katika viunga vya shule za Filbert Bayi Septemba 2018

Ron alicheza mchezo wa kikapu wakati wa majira ya baridi na baseball hadi alipokuwa akiingia sekondari. Maisha yaliendelea huko Connecticut lakini wakahama kutoka Stratford hadi Bridgepor.
Akiwa High School Ron alikuwa mahiri katika mchezo wa Baseball na alifanikiwa kushiriki ligi ya Babe Ruth na kushinda MVP katika timu yao kwenye michuano ya ligi. 


Katika michuano ya riadha ya jimbo la Connecticut alifanikiwa kushiriki kwenye mbio za maili moja pia akiwa katika michuano ya shule ya New England alipambana na kushika nafasi nzuri na baadaye michuano ya New England States huko Marekani alishika nafasi ya saba.


Baada ya kushika nafasi hiyo alilia sana na kurudi Providence huko Rhode Island kwasababu hakuwamo katika nafasi sita bora hivyo hakupata medali yoyote. 


Kocha wake alimtia moyo Ron akimtaka aendelee kufanya mazoezi kwa nguvu na kwamba mwaka ujao angekuwa tofauti. 


Baada ya mazoezi ya muda mrefu akiwa bado High School alivunja rekodi ya maili moja ambako alishika nafasi ya saba huko Providence, Rhode Island akitumia dakika 4:20.1 hivyo kuvunja rekodi iliyodumu kwa miaka 22. 


Muda huo uliweka rekodi ya kuwa  wa sita kwa kasi zaidi nchini Marekani. Baada ya hapo zilikuwa scholarship 100 zilizomtaka kwenda Chuo Kikuu lakini alichagua kwenda Chuo Kikuu cha San Jose State. 


Akiwa huko San Jose State hakufanikiwa kumaliza miaka mitatu isipokuwa aliacha masomo. Wakati huo akiacha alipata ufadhili katika mbio fupi na zile za nyika. 


Katika mbio kwenye chuo hicho alifanikiwa kushika nafasi sita katika michuano ya mwaka 1952. 


Ron Davis alikuwa mahiri kweli kweli, ubora wake ulimfanya apewe unahodha kikosi cha mashindano. Katika michuano hiyo aliiwezesha kutwaa ushindi katika mbio za nyika hivyo kuwa nahodha wa kwanza kuongoza kikosi cha timu hiyo kilichochanganyika kutwaa taji. 

Katika mbio za kuwania kufuzu kuwamo katika kikosi cha timu ya taifa ya Marekani kwa ajili ya michuano ya Olimpiki alishindwa mwishoni katika majaribio hayo mawili. 


Wanariadha 13 bora walifuzu kwenye majaribio hayo huku Ron Davis akishindwa kuwamo kwenye wachezaji sita bora. Angeweza kufuzu mita 3,000 kuruka viunzi lakini alijikuta akidondoka katika kiunzi cha tatu licha ya kuinuka na kuendelea alishindwa kufuzu. 


Juhudi za Ron Davis zilionekana akapata ufadhili katika ziara ya kuzuru bara la Afrika akiwa na Goodwill.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya Ron Davis alisema,"Safari hiyo ilinifariji baada ya ndoto zangu katika michuano ya Olimpiki kushindwa kutimia."


Safari hiyo ndiyo iliyomfanya kuona umuhimu wa kuwasaidia watu weusi hususani bara la Afrika hadi sasa kwani katika kuzunguka nchi mbalimbali aligundua kuwa Afrika ina vipaji vinavyohitaji kuungwa mkono kwa kila hali.

ZIARA YA GOODWILL
Ziara hiyo ilichukua nchi nane katika Afrika Magharibi na Afrika Kaskazini. Kwa maelezo yake Ron Davis alisema wakati akianza ziara hiyo moyo wake ulianza kuchanganyika na chembechemba za uanaharakati (uanamapinduzi) kwani nyakati hizo ubaguzi wa rangi ulikuwa kitu cha kawaida. 


Ron Davis aliamua kwa dhati kuung'oa ubaguzi huo ndani na nje ya michezo ikiwamo kuwafanya wanaokandamiza na wanaokandamizwa kutambua haki na wajibu wao kama binadamu. 


Timu hiyo ya kuzuru Afrika haikuwa imejimbanua katika hilo lakini Ron Davis aliona iko haja ya kuwasaidia wanamichezo katika jamii zao. 


Nchi ya kwanza ilikuwa Ghana ambako walijifunza mambo mengi na baadaye walitua Algeria ambako walikutana na wanafunzi, ambao mmojawapo aliuliza swali kwanini Wamarekani weusi kabla hawajaitwa kwenye timu wanaitwa Wanegro na baada ya kuwa kwenye timu ya taifa wanaitwa Wamarekani na baada ya hapo wanaitwa tena Wanegro. 


Swali hilo lilimshtua sana Ron Davis ambaye aliamua kurudi tena chuoni kumalizia masomo yake, wakati huo akitoka kuinoa timu yake ya shule aliyosoma ya Bridgeport na miaka miwili alikaa katika Chuo Kikuu cha Bridgeport. 


Majira ya joto ya mwaka 1968 alichaguliwa katika Idara ya Elimu ya Goodwill kitengo cha ukocha kwenye nchi za Afghanistan,Pakistan na Ireland. 


Mwaka huo huo alirudi shuleni kumalizia shahada yake akiwa kama kocha msaidizi chini ya mikono salama ya  mkongwe Budwinter wakati ambao John Carlos na Tommie Smith walipopokea vitisho kutokana na kuvaa glovu nyeusi ikiwa ni sehemu ya kupingana na unyanyasaji aliokuwa akifanyiwa mtu mweusi, tukio ambalo walilifanya kwenye michuano ya Olimpiki mwaka j1968 ijini Mexico.

UJIO WAKE MARA YA PILI AFRIKA
Alihitimu masomo ya Chuo Kikuu cha San Jose mwaka 1970 na akapata nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Michezo na Sanaa kwenye Chama cha Wahindi wa Alberta, Edmonton nchini Canada.


Kazi yake kubwa ilikuwa kusimamia programu kwa ajili ya michezo 44 ya wahindi. Alipotoka Canada moyo wake ulikuwa ukiitaka sana Afrika kwa ajili ya kuweka ujuzi wake hapo katika riadha hususani mbio fupi. 


Alitua Afrika ambako alikuja kuzinoa Nigeria, Msumbiji, Congo Brazzaville na Tanzania kwa ajili ya mashindano ya Olimpiki, All Africa Games na Jumuiya ya Madola.

NAMNA ALIVYOKUTANA NA FILBERT BAYI
Miongoni mwa mafanikio makubwa aliyoyapata Ron Davis ni kumnoa Filbert Bayi ambaye aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa Kwanza kutwaa medali ya Olimpiki akifanya hivyo mwaka 1980. 


Jarida la Afro Sports lilimchagua kuwa Kocha Bora wa Afrika wa Mwaka. Wachezaji wengine aliowafundisha ni Mwinga Mwanjala, Jimmy Igohe, Zakaria Barie na Suleiman Nyambui. 


Mwaka huu (2018), Ron Davis alipata wasaa wa kurudi tena Tanzania ambako alipata mwaliko kutoka kwa Filbert Bayi anayemiliki Shule za Filbert Bayi kwa ajili ya kutoa uzoefu wake kwa wanafunzi wanaosoma hapo na kuchukua masomo ya michezo. 


Mwanzoni mwa mwezi Oktoba anatarajiwa kuondoka na kurudi nchini Marekani. Kwa kinywa chake anasema akipata nafasi ya kurudi atafurahi sana kwani uwekezaji uliofanywa na Bayi una maana kubwa sana katika mchezo wa riadha.

Makala haya yametayarishwa na Jabir Johnson ambaye alipata fursa ya kuzungumza na Ron Davis  Septemba 14, 2018 kuhusu maisha yake na medani ya riadha alipotua nchini Tanzania. Kwa maoni ushauri barua pepe: jaizmela2010@gmail.com

0 Comments:

Post a Comment