Thursday, October 18, 2018

Mchungaji Msigwa: Kuomba msamaha sio dhambi


Mchungaji Msigwa (wa kwanza kutoka kushoto) akijipiga picha na wabunge Said Kubenea wa Ubungo na Anthony Komu wa Moshi Vijijini mbele ya mkutano wa wanahabari Oktoba 18, 2018 jijini Dar es Salaam, katika tukio ambalo wabunge Kubenea na Komu waliomba msamaha kwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na watanzania wanaopenda mabadiliko kwa ujumla kutokana na kukutwa na hatia ya kukiuka Katiba ya cham hicho kikuu cha upinzani Tanzania.

Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa amewataka watanzania kutambua kuwa kuomba msamaha sio dhambi. 

Hayo yanajiri baada ya hukumu kutolewa kwa wabunge wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Said Kubenea wa Ubungo na Anthony Komu wa Moshi Vijijni iliyowataka kuomba radhi kwa wananchi kutokana na kukiuka katiba ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini. 

Wabunge hao walikutwa na hatia baada ya kipande cha sauti kusambaa kwenye mitandao ya kijamii wakijadili namna ya kukihujumu chama hicho na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe.
Mchungaji Msigwa aliandika katika akaunti yake ya twitter; “Kuomba msamaha sio udhaifu, ni ujasiri. Wote hukosea tofauti ni kuwa unafanya nini baada ya kukosea. Peter Msigwa MP for Iringa Urban.”

Oktoba 18 mwaka huu Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho John Mnyika aliutangazia umma wa watanzania na wanachama wake kuwa hatua kali zimechukuliwa kwa wabunge hao ikiwamo kuvuliwa nyadhifa za ndani ya chama hicho na kuwapo kwenye uangalizi wa miezi 12. 

Mbali na kukiri kuwa sauti zinazosikika kwenye kipande hicho ni za kwao, Kubenea aliwatoa wasiwasi wananchi wake hawezi kuhama chama hicho cha upinzani. 

Kubenea alisema, “Mimi ni imara, waambieni CCM sifanani nao. Mimi kupita vigingi vyote hivi, kuja mbele ya kamati kuu ni ishara kwamba nipo CHADEMA. Waliokimbilia CCM hawakuwahi hata kufika mbele ya kamati kuu. Wengine walisimamishwa tu uongozi wakakimbia.”

0 Comments:

Post a Comment