Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Monday, April 28, 2025

PAPA FRANCIS (1936-2025): Papa wa Kwanza, nje ya Ulaya tangu Karne ya 8; azikwa...R.I.P

Papa Francis (jina la kuzaliwa: Jorge Mario Bergoglio) alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 huko Buenos Aires, Argentina. Alikuwa Papa wa 266 wa Kanisa Katoliki, na alichaguliwa kuwa Papa tarehe 13 Machi 2013.


Papa Francis alifariki dunia tarehe 21 Aprili 2025 (Jumatatu ya Pasaka) saa 1:35 asubuhi kwa saa za Ulaya ya Kati, akiwa na umri wa miaka 88.

Alifariki kutokana na kiharusi kilichosababisha mshtuko wa moyo usioweza kurekebishwa. Alikuwa amehutubia hadhara kwa mara ya mwisho siku iliyotangulia, akitoa wito wa kusitisha mapigano huko Gaza.

Mazishi yake yalifanyika tarehe 26 Aprili 2025 katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na kuhudhuriwa na zaidi ya watu 250,000 pamoja na wajumbe kutoka nchi zaidi ya 130. Alizikwa katika Basilika ya Santa Maria Maggiore mjini Roma, kwa ombi lake mwenyewe ili kupata mazishi ya kawaida na yasiyo na fahari nyingi.

Papa Francis (jina la kuzaliwa: Jorge Mario Bergoglio) alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 huko Buenos Aires, Argentina. Alikuwa Papa wa 266 wa Kanisa Katoliki, na alichaguliwa kuwa Papa tarehe 13 Machi 2013. Yeye alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini, wa kwanza kutoka Bara la Kusini, na wa kwanza kutoka nje ya Ulaya tangu karne ya 8. Pia alikuwa Papa wa kwanza ambaye ni mtawa wa Shirika la Yesu (Jesuit).

Wednesday, April 23, 2025

Camerlengo Kadinali Kelvin Farrell ni nani?

Wakati dunia ikitoa machozi kwa kuondokewa na Papa Francis mnamo Jumatatu ya Aprili 21, 2025; kuna mtu asiyefahamika sana na maelfu ya wafuatiliaji wa masuala ya dini ya Katoliki mwenye asili ya Ireland aliyeishi muda mwingi nchini Marekani kabla ya kurudishwa makao makuu ya kanisa hilo jijini Vatican. 

Baada ya kutangaza kuwa Papa Francis “amerudi nyumbani kwa Baba” Kadinali Kevin Farell  ilikuwa ni habari mpya kabisa miongoni mwa wafuasi wa kanisa katoliki duniani kwamba kwa sasa atakuwa Camerlengo wa kanisa hilo ikiwa na maana kuwa atashikilia majukumu ya kuliongoza kanisa hilo mpaka atakapochaguliwa Papa mwingine. 

Papa Francis alimtangaza kuwa kadinali mnamo mwaka 2019 na kwamba kwa sasa Kadinali Farell atasalia katika nafasi hiyo “Apostolica Sedes Vacans ambapo neno "Apostolica Sedes Vacans" hutumika wakati wa kipindi cha mabadiliko baada ya kifo cha Papa au wakati ambapo Papa amejiuzulu, na wakati huu ni muhimu kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya kupitia Konklave.

Pia Camerlengo Kadinali Kevin Farell anahudumu katika matukio yote kwa kipindi chote cha maombolezo.

Farell alizaliwa jijini Dublin mnamo mwaka 1947, alisoma katika Chuo Kikuu cha Salamanca nchini Hispania pia katika chuo kikuu cha Pontifical Gregorian jijini Rome.

Utumishi wake katika kanisa katoliki duniani alianza huduma za kiroho katika Chuo Kikuu cha Monterrey huko Mexico  pia katika Parishi ya Bethesda, Maryland.

Kadinali huyo mwenye umri wa miaka 77 sasa amehudumu katika makanisa ya katoliki kwa miaka 30 nchini Marekani, ambapo mwaka 2007 atangazwa kuwa Askofu wa Dallas hadi mwaka 2016 wakati ambao Papa Francis  alimtaka kurudi Vatican kama kiongozi wa Idara mpya ya Uangalizi wa Familia na ndio mwaka ambao alipandishwa hadi kuwa Kadinali. 

Mnamo mwaka 2023 Kadinali Farell alitajwa kama Camerlengo, pia alitangazwa na Papa Francis kama Rais wa Mahakama ya Juu ya Vatican City State na kuwa Rais wa Kamati ya Masuala ya Siri ya Kanisa Katoliki. 

Kadinali Farell atasimamia katika mkutano wa makadinali unaojulikana kama Konklave kwa ajili ya kumchagua Papa mpya wa kanisa hilo.

Vilevile kama ulikuwa hufahamu hili; Camerlengo anaweza kuchaguliwa kuwa Papa kama ilivyofanyika kwa Papa Leo wa XIII mnamo mwaka 1878 na Papa Pius XII mnamo mwaka 1939.

Camerlengo ina maana gani?

Camerlengo ni cheo cha juu kabisa katika Kanisa Katoliki kinachohusiana na uongozi wa Vatikani, Neno hili linatokana na maneno ya Kilatini "camerarius" (mtoa huduma au msimamizi wa chumba), na linahusiana na jukumu muhimu alilokuwa nalo Camerlengo katika kusimamia mali za Kanisa, hasa wakati wa kipindi cha mabadiliko baada ya kifo cha Papa au wakati ambapo Papa hayupo. 

Camerlengo ni kiongozi ambaye anachukua nafasi muhimu wakati wa kipindi cha mpito katika Kanisa Katoliki na kuhakikisha kwamba mchakato wa uongozi na uchaguzi wa Papa mpya unakwenda kwa usahihi.

Sunday, April 20, 2025

LILIAN KITHEE: Mwanamke Shujaa wa Gurudumu kutoka Kili Red Bikers, Kilimanjaro

 TASNIA YA UJASIRI NA UZALENDO: MWANAMKE AENDESHAE BAISKELI ZAIDI YA KILOMITA 1000 KUHAMASISHA MASUALA YA RED CROSS.

Katika jamii ya sasa inayokumbwa na changamoto mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kiafya, kuna haja ya kuwa na watu wanaojitolea kwa hali na mali ili kuleta mabadiliko chanya. Mwanamke anapojitokeza kuendesha baiskeli zaidi ya kilomita 1000 kwa ajili ya kuhamasisha masuala ya Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross), anatoa taswira ya ujasiri, kujitolea, na kuonesha kuwa mwanamke ana uwezo sawa wa kuleta mabadiliko katika jamii kama ilivyo kwa mwanamume.

Kwanza kabisa, tukio hilo linaonyesha nguvu ya mwanamke na usawa wa kijinsia. Kwa muda mrefu, jamii nyingi zimekuwa zikiamini kuwa kazi ngumu au shughuli zinazohitaji uvumilivu wa hali ya juu ni za wanaume pekee. Hata hivyo, mwanamke huyu anapovuka zaidi ya kilomita 1000 kwa baiskeli, anavunja minyororo ya dhana hizo potofu na kuhimiza jamii kutambua kuwa wanawake wana uwezo wa kufanya mambo makubwa yanayohitaji nguvu, maarifa, na dhamira thabiti.

Pili, hatua hiyo ni ishara ya uzalendo na moyo wa kujitolea. Kujiweka katika hali ya uchovu, hatari ya ajali, na changamoto za hali ya hewa ili kufikisha ujumbe wa msaada kwa jamii ni kitendo cha kujitoa kwa kiwango cha juu. Ni mfano bora kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutoa mchango binafsi kwa ajili ya ustawi wa wengine, hasa wale walioko katika mazingira hatarishi kama waathirika wa maafa au migogoro.

Aidha, mwanamke huyu anatoa taswira ya uongozi wa kijamii. Katika harakati zake, si tu anahamasisha msaada kwa Red Cross bali pia anakuwa kielelezo cha mabadiliko. Anachochea mjadala wa kijamii kuhusu masuala ya kibinadamu na kuibua ari ya kujitolea kwa watu wengine. Uongozi huu wa kimyakimya lakini wenye nguvu, unaleta mabadiliko ya kweli ambayo mara nyingi hayawezi kupimwa kwa vyeo bali kwa athari.

Mbali na hayo, tukio hili linatoa taswira ya mshikamano wa kijamii. Mwanamke anapochukua jukumu kama hilo, anawakilisha siyo tu jinsia yake bali jamii nzima inayotaka kuona mabadiliko. Safari yake inaweza kuwa kichocheo cha watu kuungana kwa ajili ya kusaidia shughuli za kibinadamu kama vile kutoa damu, kusaidia waathirika wa maafa au kuelimisha jamii kuhusu afya.

Hitimisho, mwanamke anapojitokeza kuendesha baiskeli zaidi ya kilomita 1000 kuhamasisha masuala ya Red Cross anakuwa kielelezo hai cha ujasiri, usawa wa kijinsia, uzalendo, uongozi na mshikamano wa kijamii. Ni mfano wa kuigwa na sauti ya matumaini kwa jamii yenye kiu ya mabadiliko. Safari yake si tu ya baiskeli, bali ni safari ya matumaini, huruma, na mabadiliko ya kweli.

Tuesday, April 15, 2025

MMFA yapokea marekebisho ya Uwanja wa Railway Moshi; Meya Kidumo apewa maua yake

 

Marekebisho ya Uwanja wa Railway uliopo Njoro katika Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi ukifanyiwa marekebishwa kwa makatapira ikiwa ni mwendelezo wa kuinua vipaji vya soka kwa kuboresha miundombinu ikiwamo maeneo ya kuchezea yaani pitch. Meya wa Manispaa ya Moshi Injinia Zuberi Kidumo ndiye Diwani wa Kata hiyo ambako Uwanja wa Railway unafanyiwa marekebisho. (Credit to: Jabir Johnson/JAIZMELA).

Chama Cha Soka Manispaa ya Moshi (MMFA) mkoani Kilimanjaro kimepokea kwa shangwe kuu marekebisho yanayoendelea ya Uwanja wa Soka wa Railway.

Hatua ya kufanya marekebisho ya uwanja vya soka wa Railway yanatoa taswira kadhaa muhimu kuhusu maendeleo ya michezo, usimamizi wa miundombinu, na mwelekeo wa kijamii na kiuchumi katika mji.

Akizungumza uwanjani hapo Katibu wa MMFA Mwalimu Japhet Mpande amesema marekebisho yanaonyesha dhamira ya Manispaa ya Moshi kuboresha mazingira ya michezo kwa vijana na wakazi wake.

Mwalimu Mpande amesema yote yanaonesha kuwa Moshi inajitahidi kufikia viwango bora vya michezo na kuvutia mashindano ya kitaifa, pia inaweza kusaidia vijana wengi kujiingiza katika michezo kitaaluma au kupata ajira kupitia michezo.

………

Aidha Mwalimu Mpande ameongeza kuwa marekebisho ya viwanja mara nyingi huambatana na mpangilio mzuri wa mazingira ambapo yataongeza mvuto wa Manispaa ya Moshi kama sehemu inayojali mazingira na ustawi wa jamii.

Kwa upande wao wakazi wa Njoro uliopo uwanja wa Railway wamepokea kwa furaha na kutoa pongezi lukuki kwa Meya wa Manispaa ya Moshi Injinia Zuberi Kidumo ambaye ni Diwani wa Kata ya Njoro.

Aidha wakazi hao wameapa kuulinda uwanja huo ikiwamo tabia mbaya za udokozi, pia watu kukatisha uwanjani ili uendelee kuwa lulu kwa kata ya Njoro na Manispaa ya Moshi kwa ujumla.

…………….

Gharama za ukarabati huo bado hazijawekwa wazi mpaka utakapokamilika na taarifa rasmi kutolewa.

Viwanja bora vinaweza kuleta fursa za biashara ndogondogo (mfano wauzaji wa vyakula, vinywaji, mavazi ya michezo) na kuongeza mapato ya halmashauri kupitia kodi na matumizi ya viwanja kwa shughuli mbalimbali.

Uwanja wa Railway unafanyiwa marekebisho ikiwa ni takribani miongo minne kupita licha ya kwamba umekuwa ukitumiwa katika mashindano mbalimbali ikiwamo Zuberi Cup.















Sunday, April 13, 2025

Freeman Mbowe: Usiangalie siasa kama burudani; Siasa ni Maisha yako...


Safari ya Ukombozi wa Nchi yetu imekuwa ngumu, kwasababu watu hamko SERIOUS..Siasa imekuwa kama kitu cha mlipuko wakati wa Kampeni; kampeni zikiisha watu wanalegea, wanadhirika…tumekuwa na tabia kuhusudu na kuwaabudu viongozi, tunawasujudu viongozi; tunasahau sana watu wa Tanzania kuwa siasa ni maisha; Usiangalie siasa kama burudani…Siasa ni maisha yako; Viongozi wakeo ndio wanasababisha maisha uliyoko nayo leo…Sio Mungu; Wanasiasa na siasa wanaamua elimu yako leo; wanasiasa na siasa ndiyo imeamua ukaishia darasa la saba..

Freeman Mbowe; M/KITI Mstaafu wa Chadema.

Thursday, April 3, 2025

KIBONG’OTO: Kutoka kituo cha Utafiti wa Kahawa hadi Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi


Mpaka mwaka 1882 katika bara la Ulaya mtu mmoja kati ya watu saba alikuwa anakufa kwa ajili ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ambapo tarehe 4 Machi 1882 Mjerumani wa Chuo Kikuu cha Gottingen Dkt. Robert Koch alitangaza kugundua kimelea kinachosababisha ugonjwa huo
  na kukipa jina la “Mycobacterium tuberculosis” MTB.

Hatua ya kubaini kinachosababisha ugonjwa wa kifua kikuu ilikuwa ni ugunduzi mkubwa kuwahi kutokea ulimwenguni kwani kwa miaka kenda rudi watalaamu mbalimbali waliketi chini kubaini kimelea kinachosababisha ugonjwa huo kama ni bakteria, protozoa, minyoo au ectoparasaiti.

Mwaka 1848 Mmishionari wa Kijerumani Johannes Rebmann aliandika rekodi ya kuwa mzungu wa kwanza kutoka barani Ulaya kuuona Mlima Kilimanjaro na baadaye walifuata wengine Richard Burton na  John Hanning Speke mnamo mwaka 1858 ambao walifanikiwa kuchora ramani ya Ziwa Tanganyika.

Mnamo mwaka 1884 kulifanyika Mkutano wa Berlin ambao ulikuwa maalum kwa ajili ya kuligawa bara la Afrika ambapo Tanganyika iliangukia mikononi mwa Ujerumani ambao walichukua na maeneo mengine kama Togo na Namibia. Walikaa Tanganyika kutoka miaka hiyo ya 1880 hadi waliposhindwa vita vya kwanza vya dunia mnamo mwaka 1919.

Tanganyika ilichukuliwa na Waingereza ambao walikaa hadi kupata uhuru mnamo tarehe 9 Desemba 1961; hivyo mambo mengi waliendeleza ikiwamo miradi mbalimbali ya kilimo;

Katika ardhi ya Tanganyika kanda ya kaskazini walianza utafiti wa mazao ya kahawa katika mkoa wa Kilimanjaro na Arusha; hata hivyo walivutiwa na eneo la Kibong’oto ambalo waliamua kuweka kituo chao cha utafiti wa zao la kahawa.

Hata hivyo baadaye walikuja kubaini wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi katika mashamba ya utafiti walikuwa wakikabiliwa na matatizo ya vifua na mapafu pia vikohozi visivyoisha na baridi hata wengine kupoteza maisha.



Zaidi anasimulia Dkt. Peter Daud ambaye ni Mtafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza wa Hospitali ya Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto

Hospitali ya Kibong’oto ni hospitali yenye historia ndefu sana, Imekuwepo toka mwaka 1926 ilianzishwa kama kituo kidogo. Kilichoanzishwa na wakoloni, kilikuwa ni kituo cha utafiti wa mabo ya kahawa. Kwa nchi za Afrika Mashariki chini ya Mjerumani, Mjerumani alianzisha kama kituo kidogo cha utafiti wa kahawa; kadri muda uliuvyoenda wale waliokuwa wakifanya kazi katika mashamba ya kahawa wakaanza kuona, Kama wana ugonjwa ambao haueleweki; wanabanwa na mapafu, wanakohoa; kwasababu Mjerumani alikuwa anashirikiana na wenzao waliowaacha huko ndio wakajakugundua kuwa ulikuwa ni kifua kikuu. Ukiangalia kwenye memo walizokuwa wanaandikiana zilionyesha ni ugonjwa wa TB. Kwa hiyo wakahamisha kutoka kituo cha utafiti wa kahawa hadi kuwa sanatorium kuhudumia wagonjwa wanaopata ugonjwa kifua kifuu. Kwa hiyo ikaendelea hivyo mpaka tunafika kupata uhuru; pia tunafahamu kuwa baada ya vita ya dunia Tanganyika ilikuwa chini ya koloni la Waingereza; lakini wakaendeleza kuwa wanatibu wagonjwa wote waliokuwa chini ya makoloni ya Wajerumani na Waingereza. Baada ya kupata uhuru tunafahamu hali ya afya ilivyokuwa nchini; vituo vilikuwa vichache na vingine vilikuwa ni vya taasisi za kigeni; ilivyoendela hivyo; Kibong’oto ikaendelea kuwa ni hospitali ya kutibu wagonjwa wa Kifua Kikuu,” alisema Dkt. Peter Daud

Wakati inaanzishwa kama Sanatorium ya Kibong’oto mnamo mwaka 1926 Dkt. Norman Davies aliweka rekodi ya kwanza ya kuwa Mganga Mfawidhi akifuatiwa na Dkt. Allen Yatera. Mnamo mwaka 1978 Dkt. John Jacob Kifaruka alikuwa Mganga Mfawidhi hadi mwaka 1986, kisha Dkt. James Salekwa alihudumu katika wadhifa huo hadi mwaka 1992.

Dkt. Cathbert Kiwia alishika wadhifa huo hadi mwaka 1998 alipoukabidhi kwa Dkt. Liberate John Mleah ambaye alihudumu kwa miaka 10 hadi     mwaka 2014 akiweka rekodi ya kwanza tangu Tanganyika ipate uhuru kuwa Mganga mfawidhi aliyekalia kiti hicho kwa muda mrefu.

Dkt. Riziki Kisonga aliushika kwa miaka saba hadi tarehe 14 Oktoba mwaka 2021 pale Dkt. Leonard Subi alipokabidhiwa hadi sasa akiwa katika wadhifa wa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto.




“Jambo la Msingi katika Hospitali yetu ni kwamba hii ni hospitali ya kihistoria kwasababu ni moja ya chimbuko la sayansi ya matibabu ya  ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini; Mwaka 1926 ndiyo ilianza kama hospitali ambapo ilianza kama kituo cha kutenga wagonjwa wa Kifua Kikuu. Lakini mwaka 1952 ikapandishwa hadhi na kuwa hospitali kamili ya Taifa ya Kifua Kikuu. Na ikumbukwe kwamba ilichukua takribani miaka 60 kugundua dawa za kutibu Kifua Kikuu tangu vimelea vya Kifua Kikuu vilivyogundulika mwaka 1882 na mwanasayansi mahiri wa Kijerumani Dkt. Robert Koch;” alisema Dkt. Leonard Subi

Mchango wa Hospitali  Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto baada ya uhuru wa Tanganyika mnamo mwaka 1961 ni mkubwa hasa ikizingatiwa wakati ule juhudi za kulikabilli janga hili la kifua kikuu lilikuwa bado katika kiwango cha chini ikilinganishwa na sasa

Sisi kama Hospitali ya Kibong’oto tunayo michango mikubwa sana na mpaka sasa tunaitwa Hospitali Maalumu ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto;  Hii kufuatia Tangazo la Serikali NA. 8828 la Novemba 2010 ambapo tulitangazwa kuwa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi. Na kwa muda mrefu tumekuwa tukitoa huduma za kimatibabu hususani matibabu ya kibingwa hususani katika magonjwa ya Kifua Kikuu lakini tangu tutangazwe sasa tumepanua wigo na kuyafikia magonjwa mengineyo;” aliongeza Dkt. Leonard Subi

Kibong’oto pia inatoa taswira ya athari za  Ukoloni katika sekta ya afya, kwani wakati wa utawala wa kikoloni hospitali hii ilikuwa pekee kwa ajili ya matibabu ya kifua kikuu licha ya kwamba baada ya uhuru serikali ya Tanzania ilijitahidi kufanya mabadiliko katika utoaji wa huduma za afya.

Mtafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Dkt. Peter Daud anatupitisha katika eneo la vifaa na rekodi mbalimbali ambazo zilikuwa zikitumika wakati huo kabla ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa na serikali ya Tanzania.
















Mbele yenu vitu mnavyoviona, hizi ni malikale sehemu ya kumbukumbu ya historia ya Hospitali ya Kibong’oto kama tunavyofahamu Hospitali imekuwepo tangu mwaka 1926 ikiwa inatoa matibabu ya kifua kikuu, ina maana kabla ya uhuru. Kwa hiyo hapa vitu tunavyoviona, hivi ni baadhi tu ya kumbukumbu za wagonjwa zinazoonyesha taarifa za wagonjwa waliowahi kutibiwa hapa kama inavyoonekana kuanzia mwaka 1923. Na hii hapa ndiyo rejista au leja ya wagonjwa wote waliokuwa wanafanyiwa upasuaji. Kama tunavyofahamu kabla ya dawa kuwepo, Hospitali ya Kibong’oto; ni ya kwanza Tanzania kufanya upasuaji wa mapafu; hii ni mojawapo ya kumbukumbu za wagonjwa waliokuwa wanafanyiwa upasuaji wa mapafu, moja ya sehemu ya matibabu ya Kifua Kikuu. Na hii kama inavyoonekana ni mihuri iliyokuwa inatumika kwamba mgonjwa alipokuwa akija; baada ya kuwa Daktari ameshampima kifua chake alikuwa anagonga muhuri sehemu alipoandika taarifa zake na sehemu ambayo imeharibika ya kifua. Na hiyo ilikuwa kwa ajili ya mwendelezo na kuonyesha wapi alipotoka na wapi anaelekea mgonjwa husika. Hiki pia kilikuwa ni kifaa kilichokuwa kikitumika katika upasuaji wa mapafu, kwasababu tunafahamu kwamba; wataalmu wa enzi hizo kabla ya uhuru walikuwa wakijaza hewa kwenye mapafu. Unajaza hewa kwa ajili ya kwenda kuua hivyo vijidudu kenye mapafu waliojificha. Kama unavyojua, upasuaji wa mapafu ni lazima uweze kuchana mbavu na hivi ni mojawapo ya vifaa vilivyotumika enzi za ukoloni kufanya upasuaji wa mapafu pia ni sehemu ya matibabu ya Kifua Kikuu. Kama tunavyoona vifaa vyote vilivyokuwa vikitumika katika kufungua mapafu, vingine vya sehemu za kujazia hewa na hewa hiyo ilikuwa inapimwa na mitambo. Mbele yenu huu ni mtambo, ulikuwa unatumika kwa wale wagonjwa waliokuwa wanakuja baada ya madaktari wameshawaona na vipimo vimefanyika kuwa wamejaa maji au usaha au kitu kingine ambacho kinahitaji kuvutwa na hii ilitumika wakati huo kufyonza, kwa sasa zipo za kisasa. Ilikuwa inatumika kuvuta damu, uchafu pia wakati wa upasuaji kwa mfano upasuaji wa mapafu, damu nyingi zilipokuwa zinatoka hii ilikuwa inatumika. Na hii ilikuwa sehemu ya mitungi ya Oksijeni, mgonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji alikuwa anapelekwa katika chumba cha uangalizi maalum huku akiendelea kupata hewa ya Oksijeni. Hii hapa ni Mashine ya kuchomelea na sisi huku kwenye udaktari kuna sehemu huwa tunachomelea, wakati wa upasuaji unapokuwa unafungua kifua; ile mishipa midogo midogo ya damu inayovujisha damuili uwezekuona eneo lako la upasuaji vizuri; hii ndiyo mashine iliyokuwa inatumika kuchomelea kwa ajili ya kuziba ile mishipa ya damu isiweze kuchafua eneo ambalo daktari anafanyia upasuaji. Ni mashine ya zamani lakini bado ni mashine nzuri sana, kwa sasa bado inafanya kazi lakini kuna mashine za kisasa ambazo hatuwezi kutumia tena;” alifafanua Dkt. Peter Daud    

Baada ya Uhuru serikali ya Tanzania imeendelea kujikita katika mfumo wa afya wa kidemokrasia na unaohudumia watu wote wenye changamoto za kifua kikuu; Kibong’oto imekuwa mfano na alama muhimu ya utekelezaji  wa sera za afya na kuonyesha umuhimu wa kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapatikana kwa watu wote bila kujali hali zao za kijamii na kiuchumi.      

Jina la Kibong’oto; yeyote Yule anayekuja hapa; ndiyo hospitali pekee inayotoa huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu ndiyo maana unaona sisi tunapokea wagonjwa wote nchi nzima. Na wengine wanatoka nchi za jirani hizi za maziwa makuu;  (Kibong’oto) imekuwa ni chachu ya kutoa matibabu kwa viwango vya kimataifa. Mgonjwa anayetibiwa hapa TB hata angeenda Ujerumani ataweza kutibiwa vilevile. Kwa hiyo kuna mwingine yuko Shinyanga, labda yupo Kazuramimba, Kigoma anavyoanza kujiona hapa nipo aua akawa anahisi naweza kuwa na TB; wengine wamekuwa wakipanda basi wenyewe, wanajileta wenyewe Kibong’oto na wanapata matibabu kasha kurudi majumabni kwao kuendelea na shughuli zao;” alongeza Dkt. Peter Daud    

Dkt. Peter Daud kama mwajiriwa katika Hospitali  Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto anafunguka kuhusu namna ambavyo mapambano dhidi ya Kifua Kikuu katika hospitali hiyo yalivyoacha kumbukumbu isiyofutika katika maisha yake pia yameacha matokeo chanya kitaifa na kimataifa.

Ilikuwa ni kuhamisha wagonjwa kutoka kwenye matibabu ya sindano na kuwahamisha moja kwa moja kwenye matibabu ya vidonge

Kwasababu tunafahamu hapo zamani tulikuwa tunatumia sindano kwani ilikuwa sehemu ya matibabu; kuna mgonjwa alikuwa anachomwa miezi nane na mwingine zaidi ya miezi nane; Unaweza ukafikiria kwamba kila siku ya Mungu anachoma sindano, sindano, sindano, sindano zaidi ya miezi nane lilikuwa siyo jambo la kawaida. Lakini kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia sisi Kibong’oto tumekuwa sehemu ya kushiriki mabadiliko, tumeweza  kushiriki kushiriki kuwahamisha wagonjwa kutoka matumizi ya sindano hadi kwenye matumizi ya vidonge pekee. Hilo na jambo ambalo limenifurahisha sana, na sisi Kibong’oto ilikuwa ni sehemu ya mabadiliko na kuchangia kuwahamisha kutoka matumizi ya sindano hadi kwenye matumizi ya vidonge pekee;” alisema Dkt. Peter Daud    

Kwa upande wake Dkt. Subi anasisitiza kuwa mabadiliko makubwa yanayofanywa hospitalini hapo ikiwamo kukamilika kwa maabara ya Utafiti na Teknolojia ya Afya unaonyesha juhudi za kujenga uwezo wa utafiti na matumizi  ya teknolojia za kisasa katika kugundua na kutibu magonjwa.

Nikianza na matumizi ya ardhi; tumeandaa Master Plan. Kwamba hii ardhi tunaitumiaje? Kwasababu ni Hospitali ya Magonjwa Ambukizi; Master Plan yetu tumeigawanya katika maeneo, katika zones. Kwa mfano kuna zone ya maabara; maabara ya afya ya jamii, usalama wa kibaiolojia daraja la tatu;  Na maabara hiyo ina kazi zake maalum za uchunguzi wa magonjwa. Siyo maabara ya Kibong’oto peke yake lakini itatoa huduma za mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza hususani yale yenye umuhimu wa kipekee katika jamii; Lakini pia itatoa huduma za uchunguzi wa magonjwa mengine ya tiba ya kawaida; yakiwemo ya kuambukiza na yasiyokuwa ya kuambukiza. Na maabara ile ukiiangalia imejengwa na serikali makusudi. Na ndiyo uwekezaji mkubwa wa maabara katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ambayo ina kila kitu kinachotakiwa duniani. Kwa maana kwamba, inaweza kuchunguza vimelea hatarishi duniani, vya ebola, Marburg, na vinginevyo; lakini inatumia teknolojia za kimolekyuli katika ugunduzi wa magonjwa. Lakini maabara hiyo pia inamwangalia binadamu kama yeye na pia itatumika katika tafiti mbalimbali;” alisema Dkt. Leonard Subi

Kwa ujumla Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto inatoa taswira ya mabadiliko katika sekta ya afya, athari za ukoloni na juhudi za taifa katika kujenga mifumo ya afya baada ya uhuru pia inasimama kama kielelezo cha historia ya matibabu ya kifua kikuu na mchango wake  katika maendeleo ya afya nchini Tanzania.

Credit to: Johnson Jabir/JAIZMELA/ Kibong’oto Hospital; Barua Pepe: johnsonjabir@gmail.com