Rai hiyo imetolewa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Ulimwenguni ambayo hufanyika kila Machi 8 ambayo nchini Tanzania mwaka huu wa 2025 inafanyika Jijini Arusha.
Akizungumza na hadhira ya wanawake katika Halmashauri ya Moshi mnamo Machi 5 katika viwanja vya KDC wilayani humo Mkuu wa Wilaya ya Moshi Komredi Godfrey Mnzava amesema mpaka sasa hatua katika kushughulikia ukatili wa kijinsia imepigwa kuelekea kuitokomeza kabisa.
DC Mnzava amesema kumekuwa na tabia ambayo nivema idhibitiwe ya kumalizana wenyewe kwa wenyewe katika jamii pindi mwanamke au msichana anapofanyiwa vitendo vya ukatili hatua ambayo imekuwa ikivuta shati juhudi za serikali na wadau mbalimbali katika kumpigania mwanamke na msichana.
Akiwasilisha ripoti kuhusu Wanawake katika Halmshauri ya Moshi Afisa Maendeleo Stella Magori amesema jamii inapaswa kuendelea kutoa ulinzi kwa watoto wa kike kwani ndani ya kipindi kifupi matukio hayo yametokea.
“Ingawa juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia zinaendelea, lakini bado watoto wa kike wanatendewa vitendo vya ukatili ambapo Katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025 watoto wa kike 16 walifanyiwa ukatili wa kijinsia na matukio hayo yaliripotiwa katika vyombo vya kisheria ambapo matukio 13 yameshatolewa hukumu na mengine matatu yanaendelea mahakama,” amesema Bi. Magori
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Morris Makoi ametaka ushirikiano baina yake na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kuhusu elimu ya biashara ili kuwasaidia wanawake wanapoenda kukopa mikopo wawe wana ufahamu kuhusu fedha watakazopata watazifanyia kitu gani kwa ustawi wao na jamii kwa ujumla.
Awali DC Mnzava alishuhudia Bonanza la Michezo ikiwa sehemu ya kionjo katika kuadhimisha siku ya mwanamke, michezo kama kukimbiza kuku, kukimbia na magunia na kukimbia na yao katika kijiko kikiwa mdomoni ilikuwa ni burudani tosha kutoka kwa wanawake.
Pia mashindano ya unywaji wa soda katika bonanza hilo ambalo DC Mnzava aliwakabidhi washindi wa michezo hiyo vyeti vya kutambua mchango wao na Shilingi 10,000/= kila mmoja ambapo jumla ya washindi wapatao 15 walijipatia zawadi hizo kwenye bonanza hilo.
Kwa upande wao washiriki wa Siku hiyo iliyopambwa kwa Kauli mbiu, “Wanawake na Wasichana 2025, Haki, Usawa na Uwezeshaji,” wamesema ushiriki wa mwanamke katika kuijenga jamii ni mkubwa hivyo mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ni vema yakaendelea ili kujenga jamii iliyo bora.
0 Comments:
Post a Comment