Wanawake katika
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi wameonyesha umuhimu wa wa uungwaji mkono, usawa,
na haki, baada ya kufanya ziara fupi katika Gereza la Karanga-Moshi huku wakidhihirisha
huruma na utambuzi wa haki za binadamu.
Hayo yanajiri ikiwa ni
siku ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kuhama kutoka KDC na kuingia makao mapya
Sango wilayani humo pia kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 8 Machi ambapo Kitaifa yatafanyika
jijini Arusha.
Akizungumza baada ya
kuzuru Gereza la Karanga-Moshi Afisa Maendeleo na Mratibu wa Mikopo katika
Halmashauri ya Moshi Bi. Stella Magori amesema kuenda kuwaona wafungwa na
kuwasaidia kunaweza kuhamasisha jamii kuwa na mtazamo wa usawa na haki, na
kwamba sio kila mtu alikosea kwa kiwango cha kuwa na adhabu ya kudumu na kwamba
wafungwa wanastahili haki za kimsingi.
“Huu ni mwendelezo wa
kuadhimisha siku ya wanawake duniani, tumeona ni vema kusherehekea na wafungwa
na mahabusu walioko katika gereza la Karanga; wanawake wametoa michango
mbalimbali ambayo imetumika kununua baadhi ya mahitaji kwa ajili ya wafungwa na
mahabusu hao. Tuna la kujifunza ikiwamo kupata faraja kujimuika na kina mama
wenzetu ambao hawapati nafasi ya kuwepo uraiani; kuna haja ya kwenda kuwafariji
kila wakati,” amesema Bi. Stella Magori.
Akipokea msaada huo
kutoka kwa wanawake wa Halmashauri ya Moshi kwa niaba ya Mkuu wa Gereza; SSP
Rehema Okello wa Gereza la Karanga –Moshi amesema kitendo kilichofanywa na
watumishi hao ni mfano wa kuigwa na kwamba wasisite kufanya hivyo na kuihamasisha
jamii kujitolea kuwaona wafungwa na kuwatia moyo.
“Jambo mlilofanya ndugu
zangu ni la kuigwa, nasi tunalipokea kwa mikono miwili kwani mnapokuja kuwaona
wafungwa hawa mnawatia moyo n ahata wengine wakimaliza vifungo vyao watarudi
kwenye jamii na kuwa watu wema, asanteni sana,” amesema SSP R.J Okello.
Wakizungumza kwa hisia
kali wanawake walijionea hali halisi ya wafungwa katika gereza la Karanga –Moshi
wamesema wamejifunza kuwa kutoa ni moyo na sio utajiri na kwamba kila mtu
anastahili nafasi ya kurekebisha maisha yake, hata wale waliokosa bahati au
walikosea.
Wakati mwingine, kusaidia
wafungwa kunaweza kuleta mabadiliko chanya, kama vile kuongeza uelewa kuhusu
haki za wafungwa, kuboresha masharti yao, na kutoa fursa za upya kwao baada ya
kifungo. Hii inachangia katika kupunguza uhalifu na kusaidia mfungwa kuungana
tena na jamii baada ya kutoka gerezani.
0 Comments:
Post a Comment