Thursday, September 12, 2024

Askofu Sendoro kuzikwa Septemba 17, 2024

Askofu Chediel Elinaza Sendoro
(Mei 1,1970-Septemba 9, 2024)

Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), imesema mazishi ya aliyekuwa Askofu  wa (KKKT) Jimbo la Mwanga Chediel Elinaza Sendoro, yatafanyika Septemba 17 mwaka huu Wilayani humo.

Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mwanga Mathias Msemo, aliyasema hayo jana, baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha halmashauri hiyo, kilichofanyika Wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, kujadili juu ya msiba huo.

“Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Mwanga ilikutana kwa dharura Septemba 10 majira ya asubuhi na kupanga tarehe ya maziko ya aliyekuwa Askofu Chediel Elinaza Sendoro, kuwa yatafanyika Septemba 17, Jumanne ijayo; tumeweka muda wa wiki moja kwa sababu msiba huu sio wa dayosisi pekee yake, ni msiba wa Kanisa kwa ujumla”, alisema Katibu Msemo.

Msemo alisema kuwa kwa sasa vikao mbalimbali vya Kanisa vinakaa ili kuandaa mazishi ya askofu huyo wa Kwanza wa Dayosisi hiyo.

Alisema muda huo utatoa nafasi kwa Maaaskofu wenzake, Waamini na watu wengine kupata muda mzuri wa kujitayarisha kwa mazishi hayo.

“Kifo cha Hayati Askofu Chediel Elinaza Sendoro, kimekuja wakati ambao dayosisi hiyo ilikuwa kwenye maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Dayosisi, hivyo tumekuwa kwenye taharuki kuubwa na tunawasihi waumini wa Kanisa kuwa watulivu wakati huu wa msiba.”alisema.

Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Joseph Tadayo ameelezea kushtushwa kwake na kifo cha Askofu huyo ambaye alisema alikuwa ni mtu wake wa karibu ikiwemo enzi zao  wakiwa shuleni.

“Nimeupokea msiba huu kwa masikitiko makubwa sana, kwa sababu, ukiacha tu kwamba alikuwa kiongozi wangu wa kiroho pia alikuwa rafiki ambaye tulikuwa naye pamoja wakati tukisoma shule ya Sekondari ya Lutheran Junior Seminary iliyoko mkoani Morogoro na baada ya kumaliza masomo yetu yeye akaenda kwenye kazi za kiroho na mimi nikaenda kusomea maswala ya Sheria,”

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (SACP), ajali hiyo ilitokea eneo la Kisangiro Wilayani humo.

Alisema Askofu Sendoro alikuwa akitokea Barabara ya Njiapanda ya Himo ambako gari alilokuwa akiendesha lipata ajali ya kugongana uso kwa uso na lori na hivyo kusababisha kifo chake.

Alizaliwa Mei Mosi, 1970 akiwa mtoto wa kwanza wa Askofu Elinaza Sendoro aliyewahi kuwa askofu mkuu wa dayosisi ya Mashariki na Pwani,

Baba Askofu Sendoro ameacha mjane, watoto wawili na wajukuu wawili. Askofu Chediel Sendoro  alifariki dunia Septemba 9, 2024 kwa ajili ya gari wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.


0 Comments:

Post a Comment