Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro imethibitisha bila shaka yoyote kuwa mleta vurugu katika uwekezaji katika Shule ya Kibo Shanty ni mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu Ibrahim Shayo "Ibra Line".
Aidha Jumuiya hiyo imesema kuwa Ibra Line hatambuliki katika mkataba ya uwekezaji Kibo Shanty na kwamba wanaendelea kumwonya kuacha kukivuruga Chama kwa manufaa yake binafsi.
Katibu wa Jumuiya hiyo mkoani Kilimanjaro Nada Orry ameiambia JAIZMELA bila kumung'unya maneno kuwa mwanasiasa na mfanyabiashara huyo ni mleta vurugu kwani wanaotambulika ni watu Wawili katika mkataba wa uwekezaji shuleni hapo.
Chanzo kingine kimesema tafrani hizo zinaendelea kujitokeza ikiwa ni mwendelezo baada ya kusitishiwa uwekezaji katika Shule ya Sekondari ya Kibo ambao umemwacha njiapanda katika mapambano yake ya kutaka Ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini ambalo katika kura za maoni ndani ya CCM mnamo 2020 aliongoza licha ya kutopitishwa.
Ibra Line alipata fursa ya kuwekeza katika Sekondari ya Kibo mnamo mwaka 2019 na ilipofika Novemba 30, 2023 alikabidhi Shule hiyo kwa kile kilichoelezwa kushindwa kuiendesha Shule hiyo.
Awali Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM mkoa wa Kilimanjaro Chifu Daudi Mrindoko alimwita mwanasiasa na mfanyabiashara huyo kuwa ni muhuni kama wahuni wengine huku akitoa onyo la kuacha kuitikisa mihimili ya Chama kwani kwa Sasa ni muda wa kufanya kazi kwa maendeleo ya wananchi.
Chifu Mrindoko aliweka bayana kuwa vuta nikuvute shuleni hapo na Ibra Line zinajitokeza kutokana na mwanasiasa na mfanyabiashara huyo kutaka wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari kuchanganywa pamoja kinyume na mitaala ya Elimu inavyotaka.
Katika kura za maoni ndani ya Chama chake mnamo mwaka 2020 Ibra Line alimzidi Mbunge wa Sasa wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo ambaye alipata kibali cha kuteuliwa na Chama Chao kusimama katika Uchaguzi Mkuu wa Diwani, Wabunge na Rais wa mwaka huo.
0 Comments:
Post a Comment