Sintofahamu ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya wasichana Machame iliyopo Hai mkoani Kilimanjaro umeifanya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuingilia kati kwa ajili ya uchunguzi wa namna fedha zilivyotumika.
Akizungumza na vyombo
vya habari, Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro Mussa Chaulo amesema mradi huo
ulipangiwa kiasi cha shilingi milioni 260 hadi kukamilika kwake ambapo
uchunguzi wa awali umebaini kuna fedha kiasi cha shilingi milioni 38 zimetumika
kutoka vifungu vya matumizi na kuibua sintofahamu hiyo ya namna zilivyotumika.
Katika taarifa yake ya
kila miezi mitatu ya utendaji wa Takukuru mkoani hapa Chaulo amesema mradi huo
wa ujenzi wa Bweni ni miongoni mwa miradi ya maendeleo 40 katika sekta ya Afya,
Elimu, Maji na ujenzi hususani barabara ambayo wamefanya ufuatiliaji katika
wilaya zote saba ambapo mradi huo tu ndio ulioonyesha dosari.
“ Tumefanya ufuatiliaji
wa fedha za umma katika miradi ya maendeleo katika wilaya zote 7 ambapo
ufuatiliaji umefanyika katika miradi 40 yenye thamani ya Shs. 23,265,832,716.76
katika afya, elimu, maji na ujenzi (barabara),” amesema Chaulo.
Mbali na hilo Chaulo
amesema katika kipindi hicho cha Januari hadi Machi mwaka huu wameendelea
kufanya chambuzi za mifumo sita ili kubaini iwapo kuna mianya ya rushwa na
kuweka mikakati ya kudhibiti mianya hiyo kwenye mifumo hiyo ya serikali.
Aidha Chaulo amesema
Takukuru imetoa warsha kwa wadau wa sekta ya mazingira kuhusu usimamizi na
uendeshaji wa Kituo cha Utalii cha Chemka kilichopo wilayani Hai ambako
walibaini hakuna sheria ndeogo inayoruhusu Halmashauri husika kukusanya mapato
ndani ya chanzo cha Chemka, Hakuna njia maalum ya watembea kwa miguu wala
sehemu maalum ya maegesho ya magari.
“ Watu na vyombo vya
moto vimekuwa vikiharibu uoto wa asili kwa kupita na kuegesha sehemu ambao zina
uoto wa asili katika kituo cha utalii cha Chemka Hot Spring na katika uchunguzi
wetu tumebaini hilo linatokana na halmashauri husika kukosa nguvu kukusanya
mapato kwani hakuna sheria ndogo, pia hakuna njia maalum ya watembea kwa miguu
wala sehemu ya maegesho ya magari,” ameongeza Chaulo.
Chaulo ameongeza kuwa
katika Chemichemi ya Chemka choo kimejengwa ndani ya mita 60 kutoka kilipo chanzo
cha maji, na kumekosekana uhifadhi mzuri wa taka ngumu hali inayosababisha
uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya
karibu na chanzo chenyewe.
Takukuru mkoa wa
Kilimanjaro imebaini katika suala la matumizi ya maji katika wilaya ya Hai,
Halmashauri hiyo haina kibali cha matumizi ya maji kutoka Bodi ya Maji, Bonde
la Pangani ambapo kibali hicho kikiweza kukilinda chanzo hicho na kuwa na utali
endelevu wenye tija.
Hata hivyo Chaulo
amesema malalamiko 122 yalipokelewa kati ya hayo 74 yalihusu makosa ya rushwa
na 48 hayakuhusu rushwa. Sekta ya Elimu ilipeleka malalamiko 12 ikifuatiwa na
Ulinzi malalamiko 11 na Ujenzi malalamiko 11. Kesi tatu mpya zimefunguliwa
katika mahakama mbalimbali za mkoa wa Kilimanjaro na kufanya jumla ya kesi zinazoendelea
mahakamani kufikia 29 kutoka Takukuru mkoa wa Kilimanjaro.
“Malalamiko yaliyohusu
rushwa yanaendelea na uchunguzi katika hatua mbalimbali na ambayo hayahusu
rushwa walalmikaji wamepatiwa ushauri na
kuelimishwa na taarifa kufungwa kisha kuwasilishwa katika mamlaka husika,”
amesema Chaulo.
0 Comments:
Post a Comment