Raia wa Msumbiji waishio mkoani Kilimanjaro na maeneo mengine nchini Tanzania wametakiwa kujitokeza katika uchaguzi mkuu wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika unaotarajiwa kufanyika Oktoba 9, 2024
Akizungumza na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro katika ziara yake ya siku moja mkoani humo mnamo Aprili 17, 2024 Balozi Ricardo Amrosio Mtumbuida amewataka diaspora wa taifa lake kujitokeza mjini Moshi ambako kutakuwa na kituo kimoja kwa ajili yao.
“Watu wa Msumbiji mwaka huu tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Wakuu wa Mikoa, Tayari uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulishafanyika mwaka jana, sasa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu,” alisema Balozi Mtumbuida. Nimekuja kuwaomba viongozi wangu wa CCM mtusaidie kuwahamasisha raia wetu wa Msumbiji wanaoishi Kilimanjaro, itakapofika Oktoba mwaka huu wajitokeze kwa wingi kwanda kukipiga kura chama cha Frelimo ili kiweze kuendelea kuwa imara,” alisema Balozi Mtumbuida
Balozi Mtumbuida amesema miaka mitano iliyopita kumefanyika mabadiliko mengi katika katiba yao likiwamo suala la uchaguzi wa wakuu wa mikoa ambalo hapo awali halikuwepo ambapo mwaka huu watafanya uchaguzi wa viongozi hao
“Bunge wa Msumbiji lina viti 250 na chama cha Flelimo kinaongoza kwa asilimia 94 ya Wabunge wote, na uchaguzi wa mwaka huu tunatamani kufikia asilimia 100. Kipindi cha miaka mitano iliyopita zoezi la kuwachagua Wakuu wa Mikoa halikuwepo , lakini baada ya mabadiliko ya Katiba kwa mara ya kwanza tunakwenda kufanya uchaguzi wa Wakuu wa Mikoa,” aliongeza Balozi Mtumbuida.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Faraji Kibaya Swai; alisema ziara ya Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania imemkumbusha mambo mengi sana, wakati ule wa harakati za kutafuta ukombozi Kusini mwa Afrika, Tanzania ilikuwa mstari wa mbele chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliweza kuweka undugu baina yetu na Msumbiji.
“Nakumbuka nikiwa Chuoni , tulikuwa tunatoa damu kwa ajili ya wapigania Uhuru kule nchini Msumbiji , undugu wetu na nchi ya Msumbiji ni damu.Ninamshukuru sana Balozi ameonesha kuendeleza undugu wetu kwa kuja katika mkoa wetu wa Kilimanjaro hususan hapa Moshi mjini na kuzungumza na Wanachama wa CCM,” alisema Swai.
0 Comments:
Post a Comment