Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Tuesday, April 30, 2024

Miili ya Familia iliyosombwa mafuriko yaagwa KDC-Moshi DC

Miili ya Watu waliofariki kwa mafuriko wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro imeagwa leo asubuhi Aprili 30, 2024 katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya hiyo na Mamia ya waombolezaji.


Tito Chaki (1961-2024), Joram Kimambo (2011-2024), Freddy Justus (2018-2024), Anjela Chaki (2012-2024) na Edward Chaki (2010-2024), walikutwa na umauti mnamo Aprili 25 mwaka huu, kutokana na Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini ambazo zimeleta athari kubwa ikiwamo vifo, uharibifu wa mashamba, nyumba, madaraja na barabara.


Viongozi wa Siasa na dini wamehudhuria Ibada hiyo na marehemu hao wanatarajiwa kuzikwa katika kata Mbokomu na Kimochi. wilayani humo.


Mungu Awape Pumziko la Amani. AMEN






 

Saturday, April 27, 2024

AMANI GOLUGWA: Maandamano ya Chadema sio Kelele, Sherehe au Picnic

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini Amani Golugwa akizungumza na waandishi wa habari siku chache kabla ya maandamano ya Aprili 30, 2024 mjini Moshi Kushoto ni Katibu wa Chadema Moshi Mjini Mzee Minja na Kulia ni Mwenyekiti wa Chadema na Mstahiki Meya Mstaafu Moshi Raymond Mboya. (Picha na JAIZMELA)


Joto la maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yanayotarajiwa kufanyika Aprili 30, 2024 linazidi kupanda mjini Moshi  ambapo wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kutambua kuwa maandamano hayo sio kelele za wahuni bali ni ya Amani kwa Ustawi wa Tanzania


Akizungumza na vyombo vya habari mjini Moshi Leo Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini Amani Golugwa amesema watanzania wanaaminishwa kuwa maandamano hayo ni ya wahuni na wapiga kelele na kwamba huko ni kuwakosea watanzania wanaokabiliwa na hali ngumu za Maisha.


"Kama unanunua sukari kilo shilingi 1000 usiandamane kaa nyumbani, maandamano haya hayatakoma, tutaandamana pia katika ngazi za wilaya mpaka serikali ielewe," amesema Golugwa.


Golugwa amesema  Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limetoa ushirikiano mzuri ambapo njia zilizoruhusiwa ni tatu na mkutano wa hadhara utafanyika katika Viwanja vya Mashujaa ambako viongozi wa Chadema watakuwepo.


Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, ataongozana na Boniphace Mwabukusi, Peter Msigwa, Godbless Lema, Raymond Mboya, John Heche na Japhary Michael pamoja na viongozi wengine wa ngazi za Kijiji, Kata na. Wilaya.



Tuesday, April 23, 2024

Takukuru Kilimanjaro yabaini ‘madudu’ ujenzi Bweni Machame Girls

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro Mussa Chaulo akizungumza na vyombo vya habari mnamo Aprili 23, 2024 kuhusu utendaji kazi wa miezi mitatu kutoka Januari hadi Machi 2024 wa taasisi hiyo. Picha na JAIZMELA


Sintofahamu ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya wasichana Machame iliyopo Hai mkoani Kilimanjaro umeifanya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuingilia kati kwa ajili ya uchunguzi wa namna fedha zilivyotumika.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro Mussa Chaulo amesema mradi huo ulipangiwa kiasi cha shilingi milioni 260 hadi kukamilika kwake ambapo uchunguzi wa awali umebaini kuna fedha kiasi cha shilingi milioni 38 zimetumika kutoka vifungu vya matumizi na kuibua sintofahamu hiyo ya namna zilivyotumika.

Katika taarifa yake ya kila miezi mitatu ya utendaji wa Takukuru mkoani hapa Chaulo amesema mradi huo wa ujenzi wa Bweni ni miongoni mwa miradi ya maendeleo 40 katika sekta ya Afya, Elimu, Maji na ujenzi hususani barabara ambayo wamefanya ufuatiliaji katika wilaya zote saba ambapo mradi huo tu ndio ulioonyesha dosari.

“ Tumefanya ufuatiliaji wa fedha za umma katika miradi ya maendeleo katika wilaya zote 7 ambapo ufuatiliaji umefanyika katika miradi 40 yenye thamani ya Shs. 23,265,832,716.76 katika afya, elimu, maji na ujenzi (barabara),” amesema Chaulo.

Mbali na hilo Chaulo amesema katika kipindi hicho cha Januari hadi Machi mwaka huu wameendelea kufanya chambuzi za mifumo sita ili kubaini iwapo kuna mianya ya rushwa na kuweka mikakati ya kudhibiti mianya hiyo kwenye mifumo hiyo ya serikali.

Aidha Chaulo amesema Takukuru imetoa warsha kwa wadau wa sekta ya mazingira kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Kituo cha Utalii cha Chemka kilichopo wilayani Hai ambako walibaini hakuna sheria ndeogo inayoruhusu Halmashauri husika kukusanya mapato ndani ya chanzo cha Chemka, Hakuna njia maalum ya watembea kwa miguu wala sehemu maalum ya maegesho ya magari.

“ Watu na vyombo vya moto vimekuwa vikiharibu uoto wa asili kwa kupita na kuegesha sehemu ambao zina uoto wa asili katika kituo cha utalii cha Chemka Hot Spring na katika uchunguzi wetu tumebaini hilo linatokana na halmashauri husika kukosa nguvu kukusanya mapato kwani hakuna sheria ndogo, pia hakuna njia maalum ya watembea kwa miguu wala sehemu ya maegesho ya magari,” ameongeza Chaulo.

Chaulo ameongeza kuwa katika Chemichemi ya Chemka choo kimejengwa ndani ya mita 60 kutoka kilipo chanzo cha maji, na kumekosekana uhifadhi mzuri wa taka ngumu hali inayosababisha uchafuzi wa mazingira  katika maeneo ya karibu na chanzo chenyewe.

Takukuru mkoa wa Kilimanjaro imebaini katika suala la matumizi ya maji katika wilaya ya Hai, Halmashauri hiyo haina kibali cha matumizi ya maji kutoka Bodi ya Maji, Bonde la Pangani ambapo kibali hicho kikiweza kukilinda chanzo hicho na kuwa na utali endelevu wenye tija.

Hata hivyo Chaulo amesema malalamiko 122 yalipokelewa kati ya hayo 74 yalihusu makosa ya rushwa na 48 hayakuhusu rushwa. Sekta ya Elimu ilipeleka malalamiko 12 ikifuatiwa na Ulinzi malalamiko 11 na Ujenzi malalamiko 11. Kesi tatu mpya zimefunguliwa katika mahakama mbalimbali za mkoa wa Kilimanjaro  na kufanya jumla ya kesi zinazoendelea mahakamani kufikia 29 kutoka Takukuru mkoa wa Kilimanjaro.

“Malalamiko yaliyohusu rushwa yanaendelea na uchunguzi katika hatua mbalimbali na ambayo hayahusu rushwa walalmikaji wamepatiwa ushauri  na kuelimishwa na taarifa kufungwa kisha kuwasilishwa katika mamlaka husika,” amesema Chaulo.


 

Wednesday, April 17, 2024

Diaspora wa Msumbiji mkoani Kilimanjaro kupiga kura mjini Moshi Okt. 9, 2024


Raia wa Msumbiji waishio mkoani Kilimanjaro na maeneo mengine nchini Tanzania wametakiwa kujitokeza katika uchaguzi mkuu wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika unaotarajiwa kufanyika Oktoba 9, 2024 

 

Akizungumza na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro katika ziara yake ya siku moja mkoani humo mnamo Aprili 17, 2024 Balozi Ricardo Amrosio Mtumbuida amewataka diaspora wa taifa lake kujitokeza mjini Moshi ambako kutakuwa na kituo kimoja kwa ajili yao.

 

 “Watu wa Msumbiji mwaka huu tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Wakuu wa Mikoa, Tayari uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulishafanyika mwaka jana, sasa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu,” alisema Balozi Mtumbuida.  Nimekuja kuwaomba viongozi wangu wa CCM mtusaidie kuwahamasisha raia wetu wa Msumbiji wanaoishi Kilimanjaro, itakapofika Oktoba mwaka huu wajitokeze kwa wingi kwanda kukipiga kura chama cha Frelimo ili kiweze kuendelea kuwa imara,” alisema Balozi Mtumbuida


Balozi Mtumbuida amesema miaka mitano iliyopita kumefanyika mabadiliko mengi katika katiba yao likiwamo suala la uchaguzi wa wakuu wa mikoa ambalo hapo awali halikuwepo ambapo mwaka huu watafanya uchaguzi wa viongozi hao 


“Bunge wa Msumbiji lina viti 250 na chama cha Flelimo kinaongoza kwa asilimia 94 ya Wabunge wote, na uchaguzi wa mwaka huu tunatamani kufikia asilimia 100. Kipindi cha miaka mitano iliyopita zoezi la kuwachagua Wakuu wa Mikoa  halikuwepo , lakini baada ya mabadiliko ya Katiba kwa mara ya kwanza tunakwenda kufanya uchaguzi wa Wakuu wa Mikoa,” aliongeza Balozi Mtumbuida.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Faraji Kibaya Swai; alisema ziara ya Balozi wa  Msumbiji nchini Tanzania  imemkumbusha mambo mengi sana, wakati ule wa harakati za kutafuta ukombozi  Kusini mwa Afrika, Tanzania ilikuwa mstari wa mbele chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,  ambaye aliweza kuweka undugu baina yetu na Msumbiji. 


“Nakumbuka nikiwa Chuoni , tulikuwa tunatoa damu kwa ajili ya wapigania Uhuru kule nchini Msumbiji , undugu wetu na nchi ya Msumbiji ni damu.Ninamshukuru sana Balozi ameonesha kuendeleza undugu wetu  kwa kuja katika mkoa wetu wa Kilimanjaro hususan hapa Moshi mjini na kuzungumza na Wanachama wa CCM,” alisema Swai.



 

Thursday, April 11, 2024

Uwekezaji Shule ya Kibo Shanty, Moshi unavyomtesa Ibra Line; Jumuiya ya Wazazi yamwita 'Muhuni'



Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro imethibitisha bila shaka yoyote kuwa mleta vurugu katika uwekezaji katika Shule ya Kibo Shanty ni mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu  Ibrahim Shayo "Ibra Line".

Aidha Jumuiya hiyo imesema kuwa Ibra Line hatambuliki katika mkataba ya uwekezaji Kibo Shanty na kwamba wanaendelea kumwonya kuacha kukivuruga Chama kwa manufaa yake binafsi.

Katibu wa Jumuiya hiyo mkoani Kilimanjaro Nada Orry ameiambia JAIZMELA  bila kumung'unya maneno kuwa mwanasiasa na mfanyabiashara huyo ni mleta vurugu kwani wanaotambulika ni watu Wawili katika mkataba wa uwekezaji shuleni hapo.

Chanzo kingine kimesema tafrani hizo zinaendelea kujitokeza ikiwa ni mwendelezo baada ya kusitishiwa uwekezaji katika Shule ya Sekondari ya Kibo ambao umemwacha njiapanda katika mapambano yake ya kutaka Ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini ambalo katika kura za maoni ndani ya CCM mnamo 2020  aliongoza licha ya kutopitishwa.

Ibra Line alipata fursa ya kuwekeza katika Sekondari ya Kibo mnamo mwaka 2019 na ilipofika Novemba 30, 2023 alikabidhi Shule hiyo kwa kile kilichoelezwa kushindwa kuiendesha Shule hiyo.

Awali Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM mkoa wa Kilimanjaro Chifu Daudi Mrindoko alimwita mwanasiasa na mfanyabiashara huyo kuwa ni muhuni kama wahuni wengine huku akitoa onyo la kuacha kuitikisa mihimili ya Chama kwani kwa Sasa ni muda wa kufanya kazi kwa maendeleo ya wananchi.

Chifu Mrindoko aliweka bayana kuwa vuta nikuvute shuleni hapo na Ibra Line zinajitokeza kutokana na mwanasiasa na mfanyabiashara huyo kutaka wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari kuchanganywa pamoja kinyume na mitaala ya Elimu inavyotaka.

Katika kura za maoni ndani ya Chama chake mnamo mwaka 2020 Ibra Line alimzidi Mbunge wa Sasa wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo ambaye alipata kibali cha kuteuliwa na Chama Chao kusimama katika Uchaguzi Mkuu wa Diwani, Wabunge na Rais wa mwaka huo.