Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Tuesday, February 27, 2024

Vijana watakiwa kuchangamkia ujuzi VETA

Zoezi la hiari la uchangiaji damu limefanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mjini Moshi Kilimanjaro Februari 27, 2024 ambapo wanachuo zaidi ya 300 walijitolea damu zao. (Picha Na: JAIZMELA)


Vijana wametakiwa kuwa imara kiuchumi kwa kuwa na ujuzi ili kujikwamua na changamoto mbalimbali za kimaisha badala ya kwa na vilio vya ukosefu wa ajira huku wakijikita katika ushabiki wa mambo ambayo hayana faida na kuziba fursa za maendeleo.


Akizungumza  wakati wa zoezi la Uchangiaji wa Damu ulioendesha na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Kilimanjaro; Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Moshi mkoani Kilimanjaro Ramadhani Matara amesema vijana wengi wamekuwa wakiamka asubuhi na kwenda kwenye michezo ya pool na ushabiki wa soka katika vijiwe huku wakiwa hawana kazi ya kufanya hatua ambayo imekuwa mwiba kwa maendeleo ya Taifa.


Aidha Matara amewataka vijana kuwa na ujuzi ambao wanaweza kuupa katika vyuo vya mafunzo ya ufundi kwa kozi za muda mfupi au mrefu ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuwa na uwezo wa kuzishangilia klabu hizo wakiwa vizuri.


Katika suala la uchangiaji wa damu Mkuu huyo wa Chuo amewataka vijana wa chuo chake kuendelea kuwa mabalozi wa utoaji wa damu hata baada ya kumaliza masomo yao chuoni hapo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Kilimanjaro Askofu Jones Mollah amesisitiza ulazima wa watanzania kuwa na utaratibu wa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wengine.


Mtaalamu wa Damu Salama Kanda ya Kaskazini Joseph Kessy, amesema bado mwitikio wa jamii kujitokeza kuchangia damu ni mdogo.


Naye Afisa Mhamasishaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi Renalda Kibona, amesema bado kundi la vijana wa kike wamekuwa waoga kujitokeza kuchangia damu tofauti na kundi la vijana wa kiume huku akisema kuwa elimu zaidi inahitajika kutolewa ili na wanawake waweze kujitokeza zaidi kuchangia damu.


Baadhi ya wanachuo walioshiriki katika zoezi hilo wamesema wamehamasika kujitolea damu licha ya dhana kwa walio wengi kuwa ukijitolea damu kuna matatizo yatajitokeza katika miili yao.


Zoezi la uchangiaji wa damu limefanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Moshi ikiwa ni wiki ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani ambayo kitaifa kilele itakuwa ni Machi 6 mwaka ju jijini Mbeya, ambapo wanachuo hao wamesaidia kupatikana kwa uniti zaidi ya 300.
















Friday, February 23, 2024

Shabiki wa Yanga akwama kuiona CR Belouzidad

 

Iddi Shaban Mkhuu, Shabiki kindaki wa Young Africans aliyeweka rekodi ya kutembea kwa baiskeli kutoka Arusha hadi Kigoma kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Simba mnamo mwaka 2021 ambapo Simba ilishinda kwa bao 1-0. (Picha na JAIZMELA)

Shabiki maarufu wa miamba ya soka nchini Yanga inayoshuka dimbani wikiendi hii kujitafuta dhidi ya CR Belouzidad ya Algeria kwenye mchezo muhimu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika amekwama mkoani Kilimanjaro.


Shabiki kindaki wa klabu huyo aliyepata umaarufu mkubwa kutokana na safari zake za kutumia baiskeli pindi klabu hiyo inapocheza kwenye viwanja tofauti nchini Iddi Shaban Mkuu amekwama mkoani Kilimanjaro akitokea Arusha kwa ajili ya mchezo huo.


Akizungumza na gazeti hili Mkuu ambaye alianza kupata umaarufu mnamo mwaka 2021 alisema changamoto ya baiskeli na malazi ndio vimemfanya ashindwe kuendelea na safari hiyo.


" Baiskeli yangu imepata mushkeli sasa sielewi kama nitatoboa kwenda kwenye mchezo muhimu wa timu yangu dhidi ya Belouzidad, hata fedha ya kula sina najitafuta lakini bado mambo hayaelekei kufanikiwa," alisema Mzee Mkhuu.


Shabiki huyo mwenye umri wa miaka 71 aliweka bayana kwamba hata anapotaka msaada kutoka kwa mashabiki wenzake imekuwa vigumu huku wengi wakionyesha kuwa ni mbabaishaji.


" Wengi wanadhani Yanga inanilipa kutokana na namna ninavyojitolea, nikiri kwamba sipewi chochote kutoka uongozi wa Yanga, Jambo ambalo limekuwa likinihuzunisha na wengi wananiona kama mbabaishaji," aliongeza Mkhuu.


Hata hivyo Mzee Mkhuu ambaye rekodi yake bora ilikuwa kusafiri kwa baiskeli kutoka Arusha hadi Kigoma pia kutoka Mwanza hadi Dar zaidi ya kilometa 2000 ameitaka klabu yake imkumbuke kwa kumsaidia Jambo kidogo.

Kupeleka mchezo huo dhidi ya CR Belouzidad, Mzee Mkhuu kama, walivyo mashabiki wengine ana matumaini kibao ya kufanya vizuri licha ya kila timu katika kundi hilo ikiwa nafasi ya kufuzu.

Iddi Shaban Mkhuu akiwa na mwandishi wa habari Johnson Jabir mnamo Februari 2024 alipokwama na safari yake ya kwenda jijini Dar es Salaam dhidi ya CR Belouzidad

 

Wednesday, February 21, 2024

Huko Moshi; Unataka sukari, nunua sabuni au kiberiti

 

Mijadala katika vijiwe vya kahawa katika mitaa nchini ni kuhusu bei ya sukari kupanda huku wengine wakilazimishwa kununua kiberiti au sabuni wakati wanapotaka kununua kilo ya sukari katika maduka ya rejareja hususani mjini Moshi mkoani Kilimanjaro. (Picha na JAIZMELA)

Baadhi ya wafanyabiashara mkoa wa Kilimanjaro, wamelalamikiwa na wananchi, kwa kuwalazimisha watu kununua  mche wa sabuni, kibiriti au sabuni kama bidhaa ya ziada ndipo wauziwe sukari.

 

Mkazi wa Kata ya Majengo Manispaa ya Moshi Dorice Chuwa, ambaye anajishughulisha na biashara za kutembeza viatu, alisema kwa sasa ukienda dukani kununu sukari mfanyabiashara anakulazimisha ununue mche wa sabuni, dawa ya mswaki au kiberiti kama bidhaa ya ziada ndipo akuuzie sukari na ukikataa kununua bidhaa hizo huwezi kukuuzia sukari.

 

“Baadhi ya wafanyabiashara wa  Manispaa ya Moshi, wanawalazimisha watu kununua mche wa sabuni, kibiriti au sabuni kama bidhaa ya ziada ndipo wakuuzie sukari, ukikataa kununua bidhaa hizo huwezi kuuziwa sukari, ” alisema Dorice.

 

Alisema “Changamoto hii imenikuta mimi juzi baada ya kutoka kwenye mihangaiko yangu jioni wakati nawaandalia watoto wangu chai kwa ajili ya kunywa kesho asubuhi waennde shuleni, ndani kwangu sukari ilikuwa imeisha nilimtuma mtoto kwenda dukani kununua sukari kilo moja, nilimpa Sh 4,000, lakini alirudi bila sukari.”alisema.

 

Alisema baada ya kumuuliza mtoto kwa nini hujanunua sukari alinijibu kuwa pale dukani wanataka kwanza ununue sabuni, kiberti au dawa ya mswaki ndipo wakuuzie sukari.

 

Akizungumza kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, aliwaagiza wafanyabiashara kuweka bayana bei ya sukari madukani mwao ili kukabiliana na changamoto ya kupandishwa kwa bei ya bidhaa hiyo.

 

“Yako malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na bei ya sukari kupandishwa kiholela kila siku, hali hii imekuwa kero kubwa kwa wananchi pamoja na juhudi zote zinazofanywa na serikali katika kukabiliana nayo”, alisema.

 

“Kuanzia sasa, wafanyabiashara wote wa jumla na rejareja watatakiwa kuweka tangazo kubwa lenye kuonyesha bei elekezi ya sukari kama ilivyoainishwa na serikali”.

 

Babu aliendelea kusema kuwa kutokana na mapenzi yake kwa wananchi, serikali yake imeagiza sukari ya ziada kutoka nje ili kufidia pengo la sukari lililoko hapa nchini.

 

“Ili kutoa unafuu kwa wananchi, serikali imeondoa kodi ya uagizaji sukari na ile ya ongezeko la thamani (VAT) ili iuzwe kwa bei ya nafuu kwa wananchi, hivyo serikali mkoani hapa haitawavumilia wafanyabiashara ambao watataka kutumia sukari hiyo kujinufaisha huku wakiwaumiza wananchi”, alisema na kuongeza, kwa kuweka bango lenye bei elekezi kutamuwezesha mnunuzi kuuziwa sukari kwa bei kama ilivyoainishwa kwenye bango hilo.

 

Aliongeza, “Serikali mkoani Kilimanjaro imejipanga kuhakikisha wananchi walioanza kufunga Kwaresma kwa Wakristo na Ramadhan kwa Waislamu sukari haitakuwa kikwazo kwao wakati wakitekeleza nguzo hizo muhimu za Kiimani”.

 

Pia mkuu huyo wa mkoa  alitoa wito kwa uongozi wa kiwanda cha sukari cha TPC kuwasilisha orodha ya wafanyabashara wa jumla watakaopewa jukumu la kuuza sukari kwa uongozi wa Mkoa ili waweze kufuatiliwa lengo likiwa ni kuhakikisha wanauza bidhaa hiyo kwa mujibu wa bei elekezi.

 

Awali akitoa taarifa ya hali ya sukari ya kiwanda cha uzalishaji sukari ya TPC kilichoko Moshi, mkoani humo Jaffari Ally alisema kuwa kiwanda hicho kinaendelea na uzalishaji hadi mwezi Machi mwaka huu wakati wa mvua za masika zinapotarajiwa kunyesha.

 

“Kwa upande mwingine sukari iliyoagizwa na serikali kufidia pengo la sukari hapa nchini imeanza kuwasili hivyo hakuna sababu ya uwepo wa uhaba wa sukari”, alisema Ally.

 

Alisema serikali imeondoa asilimia 25 ya kodi ya kuingiza sukari nchini (Income Tax) na asilimia 18 ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ili kumpa nafuu mlaji, ambapo alisema si vyema wafanyabiashara wakatumia mwanya huo kujinufaisha.

 

“Kufuatia uamuzi huo wa serikali, bei ya sukari inatakiwa kuwa kati ya  Sh 2,650 na Sh 2,800/- kwa kilo kwa bei ya jumla na Sh 2,800/- na Sh 3,000/- kwa kilo kwa bei ya rejareja na hii ni kwa mujibu wa muongozo wa serikali kuhusu bei hizi uliotolewa Januari 23, 2024”, alisema Ally.

Tuesday, February 20, 2024

Uko tayariiiiiiii! Same Utalii Festival 2024

 

Kamishna Emmanuel Mwerane wa Hifadhi ya Mkomazi akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Same Bi. Kaslida Mgeni katika geti kuu la kuingilia hifadhi hiyo kuashiria ukaribisho wa watalii katika hifadhi  hiyo kuelekea Same Utalii Festival 2024 ambalo litafanyika wilayani humo kuanzia Februari 22-24. (Picha na JAIZMELA)

Uko tayariiiiii? Ndio neno pekee ninaloweza kukuambia kwamba mambo yameiva katika wilaya ya Same na vivutio vyake mwaka huu ambapo hadi sasa maandalizi ya Same Utalii Festival yamefanyika kwa kiasi kikubwa.

 

Huyu hapa mkuu wa wilaya ya Same Bi. Kaslida Mgeni Amethibitisha uwepo wa mgeni rasmi wa tamasha hilo Waziri wa Maliasili na Utalii Bi. Angela Kairuki.

 

Bi. Kaslida Mgeni anaongeza kuhusu Kivutio cha Mlima Shengena akisisitiza uwepo wa Bata wawili na maji ya rangi nyekundu na unapoyachota huwa na mwonekano wa rangi ya njano.

 

Kwa upande wake Kamishna Emmanuel Mwerane Mhifadhi wa Hifadhi ya Wanyama ya Mkomazi amesema ni jambo la kujivunia kwa wakazi wote wa Same ambapo kuelekea Tamasha hilo wamepeleka vikundi mbalimbali kwenye maeneo ya wilaya hiyo kuhamasisha kuhusu Same Utalii Festival 2024.

 

Same UtaliI Festival itafanyika kwa siku tatu mfululizo kutoka Februari 22 hadi 24 mwaka huu katika viunga vya Same huku burudani kutoka kwa wasanii wakubwa nchini Sholo Mwamba, Nandy na Misomisondo itapamba tamasha hilo.



 








Thursday, February 8, 2024

Kuteketea Soko la Mbuyuni kutoa fursa taasisi binafsi kudhibiti majanga ya moto?

 


MOSHI, KILIMANJARO


SOKO la Mbuyuni lililopo Manispaa ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa masoko maarufu makubwa nchini ambayo yameingia katika orodha ya kuteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa kwa Wafanyabiashara, ndugu jamaa na marafiki kuathirika kisaikolojia na wengine kupoteza maisha kutokana na mshtuko

 

Masoko mengine ni kama vile Soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya, Soko la Mandela lililopo Sumbawanga mkoani Rukwa, Soko Kuu la Mpanda mkoani Katavi na Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam yamewahi kukutana na changamoto ya majanga ya moto

 

Usiku wa Februari 5 mwaka huu, moto uliteketeza Soko Kuu la Mbuyuni, lililokuwa na vibanda vya Wafanyabiashara 2,500 janga ambalo linadaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme

 

Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba hakuna madhara kwa watu yaliyotokana na maafa hayo, japokuwa mali na pengine fedha, vitu vilivyotafutwa kwa jasho jingi na muda mrefu vilitokea dakika chache

 

Pamoja na msemo wa waswahili unaosema kwamba ajali haina kinga, tunaamini kwamba majanga ya aina hii ambayo aghalabu husababisha uharibifu mkubwa wa mali au hata kugharimu maisha ya watu yanaweza kuzuilika kwa kiwango kikubwa ikiwa tu hatua za tahadhari zitachukuliwa

 

Wakizungumza na Tanzania Leo kwa nyakati tofauti wakazi wa Manispaa ya Moshi wamesema kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu imewafungua na kuitaka serikali kuruhusu taasisi nyingine kudhibiti majanga ya moto.

 

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Injinia Zuberi Kidumo akiwa na Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini katika eneo la Soko la Mbuyuni lililoteketea kwa moto mnamo usiku wa manane wa Februari 6, 2024.

Mkazi wa Kata ya Miembeni Manispaa ya Moshi Isack Kireti, ameishauri serikali kuzipa fursa taasisi nyingine imara zinazoweza kupambana na majanga ya moto yanapotokea nchini  badala ya kutegemea Jeshi la Zimamoto pekee kufanya shughuli hiyo kutokana na idadi ya watu kuongezeka kila mwaka huku vifaa vya Jeshi hilo vikishindwa kwenda na kasi ya mabadiliko

 

“Baada ya zimamoto kurudishwa Wizara ya Mambo ya Ndani ndio mambo yalipoharibika, ni vema ikarudishwa iweze kujitegemea kabisa au kuleta washindani nje ya mfumo ikiwamo kuziruhusu taasisi nyingine kusaidia kudhibiti majanga ya moto,” alisema Kireti.

 

Mkazi wa Kata ya Majengo Gadson Mdee, alisema elimu duni, uelewa ndogo juu ya namna ya kujikinga na majanga ya moto ambayo anaamini kwaba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likijipanga na kuweka mkakati balaa hilo linaweza kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

 

“Wananchi wanahitaji kuelimishwa kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya umeme kwenye nyumba na maeneo ya biashara majanga mengine yamekuwa yakisababishwa na ujivu wa masuala ya umeme na kufikia hata kuhamisha nyaya  bila ya kuzingatia wachache na vifaa stahiki.”alisema Mdee.

 

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO NURDIN BABU ANENA;

 

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu akizungumza jambo kuhusu kuteketea kwa Soko la Mbuyuni ofisi kwake.

Serikali mkoani Kilimanjaro inafanya tathmini ya kujua chanzo cha moto ulioteketeza Soko Kuu la Mbuyuni usiku wa Februari 5 mwaka huu.

 

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, aliyabainisha hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuati tukio la hilo, lililoteketeza bidhaa za Wafanyabiashara zaidi ya 2,000.

 

Babu alisema jambo lolote linapotokea halipangwi na kwamba gari la zima moto kutokufika kwa wakati katika eneo la tukio ni kutokana na hitilafu kwa takribani mwezi mmoja sasa.

 

“Kwanza nichukue fursa hii kuwapa pole sana wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo, moto huu ulianza kuwaka muda wa saa sita na nusu usiku wa Februari 5, 2024, mimi na Kamati yangu ya ulinzi na usalama ya mkoa;

 

Tulifika eneo la tukio muda wa saa saba usiku tulishirikiana na viongozi wengine waliokuwepo akiwemo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwajuma Nasombe na Mkuu wa Wilaya Kisare Makori, tulikuwa tuna hakikisha moto ule hauvuki kwenda kwenye makazi ya watu, jambo ambalo tulifanikiwa hadi ile asubuhi moto ukawa umezimika.”alisema RC Babu.

 

Awali mwenyekiti wa soko hilo Lameck Mziray, alisema soko hilo lina wafanyabiashara wasiopungua 2,500 na kwamba soko hilo limeungua lote na kuteketeza mali zote zilizokuwepo.

 

“Soko linawafanyabiashara wasiopungua 2500, mpaka sasa hivi, soko hili limeunmgua lote hakuna palilpo salia,” alisema.

 

MANISPAA KUANZA KULIJENGA UPYA SOKO LA MBUYUNI;

 

Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini Faraji Swai akizungumza na waathirika wa Janga la Moto soko la Mbuyuni mnamo Februari 7, 2024.

Ujenzi wa Soko Kuu la Mbuyuni mjini Moshi unatarajiwa kuanza Februari 9,2024 baada ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kuruhusu miradi ya Kata nyingine isiendelee kwa ajili ya dharura.

 

Akizungumza katika mkutano wake na Wafanyabiashara wa soko la Mbuyuni kuwaeleza waliyoafikiana na Baraza la Madiwani kuhusu mustakabali wao baada ya soko kuteketea Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Injinia Zuberi Kidumo, alisema Madiwani kwa pamoja wamekubali kuzuia fedha za miradi ambayo ilikuwa inakwenda kutekelezwa kwenye kata zao na fedha hizo ziweze kutumika kujenga soko hilo.

 

Alisema soko la Mbuyuni litarejea kama ambavyo lilikuwa awali, kwa sasa tuko katika hatua za kumtafuta mkandarasi ili aweze kuanza haraka ujenzi wa soko hili.

 

Mstahiki Meya Kidumo, alisema wako Wafanyabiashara  wengi katika soko hilo walikuwa  wamekopa fedha kwenye taasisi  za kifedha, aliwaomba wenye mabenki kutowasumbua kuhusu marejesho ya fedha hadi hapo soko hilo litakapokamilika, ndipo waendelee na urejeshaji wa mikopo hiyo.

 

“Ndugu zangu wafanyabiashara nafahamu wengi wenu mnamikopo kwenye mabenki, nataka niwahakikishie su=ala hili mkuu wetu wa Mkoa wa Kilimanjaro analifahamu, anafanya utaratibu wa kuongea na viongozi wa benki mlizokopo fedha ili waweze kuwa na subra kidogo kuhusu urejeshaji wa fedha hizo, pindi soko hili litakapokamilika na nyie mkaanza kufanya biashara hata mtaanza kuzirejesha fedha hizo lakini kwa sasa tumewaomba wawe na uvumilivu kidogo.”alisema Mhandisi Kidumo.

 

Katika hatua nyingine Mstahiki Meya Kidumo, alimtaka Meneja wa soko hilo, mfanyabiashara aliyekuwa anafanyabiashara eneo hilo, pindi soko hilo litakapokamilika aweze kupata sehemu yake ya kufanyia biashara na asiwepo mtu wa kuachwa.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Mwajuma Nasombe alisema mkandarasi ataanza kazi hiyo Februari 9, 2024 na ili kuepuka usumbufu, eneo lote la soko litazungushiwa uzio wa mabati.

 

“Wakati ujenzi huu ukiendelea hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kufanya biashara  yake kwenye uzio wa eneo hilo, nawaomba sana wafanyabiashara mtu ushirikiano na tunataka zoezi hili liende mapama zaidi ili muweze kuendelea na biashara zenu,”alisema Nasombe.

 

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Moshi Mjini Faraji Swai, aliwapa pole wafanyabishara hao, ambao wamefikwa  na janga hilo la kuunguliwa na mali zao.


Aidha aliwaondoa wasiwasi  Wafanyabiashara hao kuwa hakuna mtu yeyote atakayeondolewa ambae alikuwa akifanya biashara yake katika eneo hilo.

#KijaElias_Moshi