Saturday, January 28, 2023

UWT Moshi vijijini yajitayarisha kujenga Chuo cha Ushonaji

Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Moshi Vijini imekusudia kujenga Chuo cha Ushonaji ili kuwawezesha wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu ili waweze kujiimarisha kiuchumi. 

Hayo yalisemwa Januari 27,2023 na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Rwaichi Kaale kwenye mkutano  mkuu wa kwanza wa Baraza la Jumuiya hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa chama hicho Wilayani humo. 

Akizungumzia mpango kazi wa miaka mia Tano 2022-2027 Kaale amesema Jumuiya hiyo inakusudia kuwa na miradi ya kitegauchumi ili kuiwezesha Jumuiya hiyo kujiendeleza pasipo kutegemea wafadhili. 

Kaale aliitàja miradi hiyo ni pamoja na Chuo  cha ushonaji, kuanzisha kikundi cha mapishi, kuwa na mgahawa wa chakula na vinywaji pamoja na vyombo vya usafri kama vile bajaji. 

Katika hatua nyingine  Mwenyekiti wa UWT  Moshi Vijijini aliwaomba Wajumbe wa Baraza hilo kuvunja makundi na kuwataka kufanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kuijenga Jumuiya hiyo na chama kwa ujumla. 

Kwa upande wake Katibu wa UWT Moshi Vijijini Shakila Singano, alisema katika kuadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM  Jumuiya hiyo imeshiriki upandaji wa miti pamoja na kuwasajili wanachama wapya 500 kwa mfumo wa Kieletroniki ambapo matarajio ni kusajili wanachama 3,000 kwa mwaka 2023. 

Akifungua kikao hicho Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Moshi Vijijini Ramadhan Mahanyu amesema Serikali ya awamu ya sita imeipatia Wilaya hiyo kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni mbili ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya chama. 

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la UWT  Moshi Vijijini Gladness Mbwambo na Arapita Lyimo, wamesema uanzishwaji wa miradi ya kiuchumi ndani ya Jumuiya hiyo itaiwezesha UWT kuondokana na utegemezi sambamba na kuwasaidia vijana wa kike kujiepusha na ndoa za utotoni.




 

 

0 Comments:

Post a Comment