Wednesday, January 11, 2023

UVCCM Moshi Mjini yamjia juu Juma Raibu

 

Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Moshi Mjini umemjia juu aliyetimuliwa Umeya wa Manispaa Juma Raibu kuacha kukikosoa chama chake hadharani hususani katika mitandao ya kijamii na badala yake kupeleka changamoto hizo kwa kufuata utaratibu wa chama.

Akizungumza  katika Kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya CCM wilaya ya Moshi Mjini, Mwenyekiti wa  Sadath Sudi Ndibalemwa, alisema wako baadhi ya watu wachache ambao ni wana chama, baada ya kushindwa kuchaguliwa kwenye nafasi walizokuwa wameziomba kwenye chaguzi zilizomalizika hivi karibuni ndani ya chama hicho, wameunda kikundi cha kuanza kukichafua chama na viongozi wake  kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Licha ya Ndibalemwa kutomtaja moja kwa moja Juma Raibu lakini mitandao ya kijamii ya aliyekuwa Meya wa Manispaa hiyo na Diwani wa kataya Bomambuzi  ameonyesha ukosoaji mkubwa wa chama hususani baada ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kutangaza kuanza kwa mikutano ya hadhara kwa vyama vyote vya siasa nchini baada ya kuzuiwa enzi za utawala wa Dkt.John Pombe Magufuli.

Sadath Sudi Ndibalemwa,Mwenyekiti wa UVCCM wilaya wa Moshi Mjini

Katika akaunti ya Juma Raibu katika Instagram mnamo Januari 9,2023 aliandika, “Nemesikitishwa sana na baadhi viongozi wa chama changu mkoa na wachache wilaya na baadhi ya wanachama, kulaumu kuhusu Mh Rais Samia Kuruhusu mikutano ya hadhara, hakika huu ni udhaifu mkubwa sana na nikukimbia majukumu walioomba kwa Kuzoea kulala usingizi hakuna ushindi bila jasho…”

Juma Raibu anayefahamika kama ‘Man of the People’ yaani mtu wa Watu aliongeza katika utoaji wake wa maoni katika Instagram kuwa, “Twendeni kwa wananchi kusema yanayofanywa na CCM yetu na sio kuogopa mikutano tujipime kwa nguvu zetu Na sio kubebwa " hongera Mama Samia…tukutane Kazini”

Katika kuunga mkono juhudi zake Juma Raibu, wafuasi wake nao wameendelea kutoa maoni yao huku wakimtaka kukaza kamba zaidi

“Hao viongozi wa CCM wanaolalamika kwa nini mama karuhusu mikutano ingekuwa bora wangejiondoa kwenye nafasi zao, wawapishe watu wanaoweza kukisemea Chama. Viongozi dizaini hiyo ni wale waliozoea : " MSEREREKO " !!!!., Wana haja gani ya kuwa kwenye nafasi zao? waache uvivu walishazoea kulala usingizi. waamke...”alisema mfuasi aliyejitambulisha kwa jinala Job Faustine.

Viongozi wengine wa CCM waliojibu hoja za Juma Raibu ni Mrindoko Mwidadi ambaye ni Mwenyekiti wa Juumuiya ya Wazazi Tanzania mkoa wa Kilimanjaro alisema, “Viongozi gani wa Mkoa na Wilaya kwani tupo Mkoani?? pima maneno ya kuandika na kusema kwani ukiambiwa uthibitishe hili usije sema unaonewa!”

Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM (W) Moshi Mjini, Issa Bulilo alisema, “Hii sio sawa mkuu Viongozi wa Chama ngazi ya Mkoa na Wilaya wamelalamika wapi kufuatia Mh Rais kuruhusu mikutano??

Mnamo Januari 3,2023 Rais Samia aliruhusu mikutano ya vyama vya siasa baada ya marufuku ya miaka zaidi ya 6 iliyowekwa na mtangulizi wake, hayati John Magufuli.



0 Comments:

Post a Comment