Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Monday, May 31, 2021

Mamadou Sakho azuru Zanzibar

Mamadou Sakho katika viunga vya Zanzibar, Tanzania.
Mchezaji wa timu ya Crystal Palace ya Uingereza na inayoshiriki ligi kuu ya EPL Mamadou Sakho kwasasa yupo Zanzibar kwa ajili ya ziara ya kitalii.

Sakho raia wa Ufaransa ameamua kuja zake Zanzibar kwa ajili ya kula bata katika likizo hii ya msimu wa ligi ya Uingreza kuisha wiki iliopita. na anatarajia kutembelea sehemu mbalimbali nchini.

Nyota huyo aliyewahi kuhudumu na Liverpool kabla ya kutua Kusini mwa London mnamo mwaka 2017, mpaka sasa amecheza mechi 64 na kufunga bao moja tu.

Nyota huyo mrefu hucheza kwa nguvu katika nafasi ya ulinzi na mwandishi Richard Innes wa gazeti la Daily Mirror mnamo Aprili 2016 alimtaja Sakho kama, “A defensive maverick” akiwa na maana kuwa anapocheza dimbani hucheza kwa sheria zake.

Msimu wa 2020/21 Palace wamemaliza nafasi ya 14 wakiwa na alama 44 na kuwa miongoni mwa timu tano za jiji la London kuendelea kusalia katika Ligi Kuu ya England. Jiji la London ndilo linaloongoza kwa kuwa na timu nyingi za ligi kuu kuliko miji mingine ya Uingereza.  Chelsea, Arsenal, Tottenham, West Ham na Crystal Palace.

Kwa maoni ya mwandishi wa habari nchini Tanzania Jabir Johnson anasema, “Sasa yupo nchini Tanzania akipata mapumziko mafupi. Sakho ni mwislamu nafikiri amependelea zaidi Zanzibar kutokana na historia ndefu ya kisiwa hicho ambayo jamii mbalimbali zinafahamu na wengi wamekuwa na ndoto ya kukitembelea kisiwa hicho kujionea. Pia kazi ya serikali kutangaza utalii wake ni jambo linalovutia, wageni wengi kutoka kila pembe ya dunia.” 

Mamadou Sakho katika mojawapo ya mechi akiwa na Crystal Palace muda mchache kabla ya kuanza mechi akipiga goti na kuunga mkono Black Lives Matter #BLM.

 

Mkonapa FC, Mabingwa wa Soka Wilaya ya Same

Mkonapa FC vs Green Forest muda mchache kabla ya mchezo wa fainali ya Ligi daraja la nne Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Mei 30, 2021 ambapo Mkonapa FC iliibuka bingwa wa michuano hiyo. (Picha na Kilimanjaro Soccer/Harold Kifunda)

Timu ya MKONAPA FC ya Gonja Maole jana Jumapili (Mei 30, 2021) imetwaa taji la ligi daraja la nne baada ya kuizabua Green Forest ya Same Mjini kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa katika uga wa Kwasakwasa.

Katika mchezo huo uliochezwa Same Mjini, wenyeji walishindwa kutumia nafasi walizopata walau kulibakisha taji hilo na kujikuta wakipoteza.

Mshindi wa kwanza hadi watatu walipata zawadi.

ZAWADI ZA WASHINDI.

(1). Kikombe, Jezi na Mpira.

(2). Kikombe kidogo na jezi

(3). Mpira.

MAKTABA YA JAIZMELA: Mohammed ‘Adolph’ Rishard ni nani?

Mohammed 'Adolph' Rishard baada ya kustaafu soka na kuwa kocha wa mchezo huo nchini Tanzania.

Young Africans SC  (Yanga) ni klabu ya soka nchini Tanzania ambayo iliasisiwa rasmi kwa jina la New Youngs mnamo Februari 12, 1935.

Mnamo mwaka 1938 lilibadilishwa na kuwa Young Africans yaani Vijana wa Afrika. Wakati Yanga inaasisiwa pia kulikuwa na vilabu vingine vya michezo vya Wazungu na WaAsia kama Goans, European Club, Yatch na Aga Khan na baadaye Sunderland ambayo kwa sasa ni Simba SC iliyoasisiwa mnamo mwaka 1936.

Wengi wa wanachama wa Yanga walikuwa ni wazalendo na wenyeji wa Dar es Salaam na vitongoji vyake. Wakti huo vilikuwa vikikaliwa kwa wingi na watu wenye asili ya Uzaramo, Undegereko, Wakwere, Warufiji na Wamakonde wachache.

Wenyeji hawa katika kuishi kwao walitegemea zaidi uvuvi, biashara, kilimo na shughuli za bandarini. Miaka ilizidi kusonga ambapo Yanga ilifanikiwa kuwa klabu yenye kujitegemea na mfumo mpya wa soka ulipoanzishwa nchini mnamo mwaka 1965, Yanga ilikuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki licha ya kombe hilo kunyakuliwa na Simba.

Katika makala haya yatamwangazia miongoni mwa wachezaji wa Yanga; Mohammed ‘Adolph’ Rishard.

Rishard  alicheza soka na klabu ya Yanga miaka ile ya 1970; klabu alizochezea ni West German, Hale (1968), Scotland SC (1969-1970), Young Kids (1971-1973),  Yanga (1974-1976) hadi iliposambaratika. Baada ya mgogoro alijiunga na klabu ya Pilsner  iliyokuwa ikimilikiwa na kiwanda cha bia  kisha akajiunga na Pan African. Mafanikio mengine ya soka ni kuchaguliwa timu ya taifa.

Mnamo mwaka 1977-78 alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka, kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa  nchini Austria mnamo mwaka 1984-85 katika klabu ya SK Austria Klagenfurt, kisha mwaka 1986 alirejea nchini na kujiunga na Pamba ya Mwanza kabla ya ya kutimka tena kwenda nchini Oman katika timu ya Oman SC, mnamo mwaka 1988 alihudumu na Al Nasr, Sohar SC (1993-94) kisha Pan African kwa mara ya pili mnamo mwaka 1995. Pia Rishard alishawahi kuitumikia timu ya taifa, kisha kusomea masuala ya ukocha ambapo amewahi kuwafundisha klabu mbalimbali za soka nchini ikiwamo Tanzania Prisons.

Makocha wa timu ya taifa, Joel Bendera na Ray Gama wakimkabidhi Kombe la CCM Nahodha wa Pan Africans, Mohammed ‘Adolph’ Rishard Februari 5, mwaka 1977 baada ya kuwafunga Coastal Union ya Tanga 3-0 kwenye fainali Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Katikati anayetazama kamera ni mshambuliaji Kassim Manara ambaye siku hiyo alifunga mabao mawili.

KWANINI ALIKUWA MAARUFU KWA JINA LA ADOLPH?

Wakati akiwa shuleni miaka ile ya 1960 wanafunzi wenzake walimwita Adolph ambapo wakati huo alikuwapo mchezaji mahiri nchini Ureno aliyefahamika kwa jina la Adolfo Antonio da Luz Calisto.

Adolfo Calisto alikuwa nani katika soka nchini Ureno? Nyota huyo alizaliwa Januari 4, 1944 katika Manispaa ya Barreiro huko nchini Ureno. Katika maisha yake ya soka alipewa jina la ‘Barreiro Lokomotiv’ kutokana na uwezo wake wa kukimbia na kukaba katika nafasi ya ulinzi. Adolfo alikuwa akicheza kama beki wa kushoto.

Alijichotea umaarufu mkubwa na kuwa miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kutokea nchini Ureno. Aliwika katika soka miaka ile ya 1960 hadi 1970. Akiwa na Benfica alikocheza mechi 300 na kufumania nyavu mara tano alikuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi.

Alihudumu na Benfica kutoka msimu wa 1965/66 hadi 1974/75. Alikuwa miongoni mwa wachezaji walioifikisha Benfica kwenye Fainali ya Kombe la Ulaya (kwa sasa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya) mnamo mwaka 1968 ambapo walitandikwa kwa mabao 4-1 na Manchester United katika mchezo uliochezwa katika dimba la Wembley.

Adolfo alistaafu soka akiwa na umri wa miaka 33. Hadi mwaka 2021 Adolfo ni miongoni mwa wachezaji walio hai waliowahi kuhudumu na timu ya taifa ya Ureno akiwa na umri wa miaka 77.

Adolfo Antonio da Luz Calisto, enzi zake akiwa na Benfica ya Ureno. Alifahamika nchini humo kama 'Barreiro Lokomotiv'.

 

 

 


Sunday, May 30, 2021

Chelsea yatwaa taji Ligi ya Mabingwa Ulaya 2020/21

 

Bao pekee la Karl Havertz katika dakika ya 42 lilitosha kuipa ubingwa wa Ulaya Chelsea dhidi ya Manchester City. Chelsea ikiwa chini ya kocha Thomas Tuchel na Man City mikononi mwa Pep Guardiola.



 

Monday, May 24, 2021

Mapato na matumizi yamkimbiza M/Kijiji Yamu Makaa

 

Wanakijiji wa Yamu Makaa wakifunga barabara kuzuia malori ya mchang kuingia kijiji kwao, mpaka taarifa ya Mapato na Matumizi ya Kijiji itakaposomwa.

Wanakijiji wa Yamu Makaa wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wamefanya maandamano makubwa kijijini hapo yaliyosababisha mwenyekiti wa kijiji hicho kukimbia kwa kile kinachodaiwa ufujaji wa rasilimali za kijiji yakiwamo machimbo ya moramu.

Maandamano hayo yasiyo rasmi yalipelekea Jeshi la Polisi kufika kijijini hapo, baada ya wanakijiji hao kuzuia malori ya mchanga yaliyokuwa yakipita kwenda kuchukua moramu  katika kitongoji cha Kiuo ‘A’ yalipo machimbo hayo.

Aidha wanakijiji hao walisema kumekuwa na ubadhirifu wa fedha kutokana machimbo hayo, utoaji wa risiti za kieletroniki haufanyi huku risiti zinazotolewa kwa karatasi ukipewa msisitizo jambo ambalo linaongeza mianya ya rushwa.

“Ofisi ya Kijiji tumekuwa tukiisisitiza kutusomea mapato na matumizi, hususani kwenye haya machimbo kwani wanaochimba hatuoni risiti wakipewa na tunahisi kuna upigaji mkubwa wa fedha ambayo mwenyekiti na ofisi yake wanahusika,” alisema mwanakijiji (jina tunalihifadhi).

“Kuna siku tumeshuhudia hapa ndani ya siku mbili tripu 80 za mchanga zimesombwa hapa, lakini tulipomuuliza mwenyekiti akatuambia ni tripu 10 tu, jambo ambalo si kweli, tumechoka na ndio tukaona bila kutumia nguvu tutaibiwa kila siku,” alisema Joachim Kessy.

Sakata la Mwenyekiti wa Kijiji hicho Omary Mdee kukimbia lilianza baada ya kutakiwa na Jeshi la Polisi lililofika mahali hapo kutuliza ghasia hizo kuitisha mkutano wa kijiji na kuwasomea mapato na matumizi wanakijiji hao.

Siku ya pili Mdee alikiri kuwa angeitisha mkutano huo majira ya saa tatu asubuhi lakini cha kustaajabisha ni pale alipotoa taarifa kuwa mkutano hautaweza kufanyika kutokana na msiba uliotokea kijijini hapo.

Ndipo wanakijiji walipoamsha hasira zao na kufunga safari kwenda kwa Mwenyekiti huyo ambapo walimtaka aitishe mkutano huo na baada ya kumaliza watakwenda wote kwenye huo msiba ambao maziko yalitarajiwa kufanyika saa nane za mchana.

Kwa kuona hivyo mwenyekiti hakuonekana mbele yao kwa kuwataka wasubiri kidogo kisha atatoa jibu rasmi ambapo taarifa zilizotufikia baadaye zikabainisha kuwa mwenyekiti huyo amesafiri kwenda Tanga kwa sababu ambazo hazikuwekwa bayana na alipotafutwa kwa simu hakupatikana.  

Awali kabla ya maandamano hayo kufanyika, wananchi hao walilazimika kuyazuia malori hayo  kwa saa mbili, baada ya kuchoshwa na uongozi wa serikali ya kijiji hicho baada ya kushindwa kuwapa taarifa za makubaliano ya mikataba walioingia na mkandarasi wa Kampuni ya Kyara Construction Co.Ltd, ya kuchimba madini hayo na ubovu wa barabara yenye urefu wa kilometa moja na nusu.

Mkazi wa Kijiji hicho Veronica Mvungi, alikaririwa akisema kina mama wajawazito na wagonjwa, wamekuwa wakiteseka kutokana na ubovu wa barabara hiyo hususan katika kipindi cha mvua, licha ya kwamba madini hayo yamekuwa yakichimbwa katika eneo lao huku magari yenye uzito mkubwa yakipita na kuchukua moramu hiyo bila kuwatengenezea barabara.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kiuo 'A' Ramadhan Mgonja, alisemachangarawe hiyo inachimbwa amesema walikubaliana na mkandarasi huyo kuweka moramu roli sita kwenye barabara hiyo jambo ambalo amelitekeleza lakini anashangazwa kuona na wananchi hao kuyazuia magari yake.

Kwa upande wake mkandarasi huyo Prosper Kyara, alisema ameshangazwa na wananchi kuzuia magari yake kwani taratibu zote alipewa na ofisi ya Kijiji na kwamba makubaliano yalikuwa kila tripu moja ya Lori alikuwa akiwalipa serikali ya Kijiji Tsh 25,000 hadi sasa ameshachukua tripu 25 na pesa hizo amekwishailipa serikali ya Kijiji.

Mwenyekiti wa kijiji cha Yamu Makaa Omary Mdee (katikati)

Mojawapo ya mkazi wa kijiji ch Yamu Makaa akihoji kuhusu mapato na matumizi ya kijiji.

Baadhi ya wanakijiji wa Yamu Makaa walizuia uchimbaji wa moramu usiendelee mpaka pale Mwenyekiti wa Kijiji atakapoweka bayana mapato na matumizi.

 

Thursday, May 20, 2021

Kozi ya waamuzi kufanyika Julai wilayani Mwanga

 

Unaposema waamuzi katika soka, kwa mpenda michezo yeyote kichwa lazima kitauma tu; hii inatokana na waamuzi hao kuwa wachache na hao wachache wenyewe hawatumiki ipasavyo kutokana na changamoto mbalimbali.

Kwa kulitambua hilo wilaya ya Mwanga inatarajia kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kuendesha kozi ya waamuzi wa soka wilaya humo mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Afisa Michezo wa wilaya hiyo Denis Msemo alisema, “Tumebaini changamoto ya waamuzi wa soka katika wilaya yetu, na changamoto hii ipo pia kwenye wilaya za jirani sisi tumeona tukae na wadau tuendeshe kozi hii kwa manufaa yetu na taifa kwa ujumla.”

Msemo aliongeza kuwa wamechagua Julai mwaka huu kutokana na kwamba michezo ya Umitashumita na Umiseta itakuwa imefikia kilele hivyo wadau wengi wa kutaka kozi hiyo watakuja kwa wingi.

“Tunatamani kuwa na waamuzi wengi wenye viwango bora, lakini hawawezi kupatikana kama tusipoendesha kozi zinazowafaa, Mwanga inatakiwa kuwa chimbuko la waamuzi bora kwa mkoa mzima wa Kilimanjaro,” alisisita.

Aidha Msemo alisema uwepo wa waamuzi bora utasaidia kuondoa malalamiko na pia ubora wao utaboresha maslahi yao wanapokuwa kazini.

Monday, May 3, 2021

Ifahamu Hifadhi ya Msitu Asilia ya Rau

Mhifadhi Mkuu wa Msitu Asilia wa Rau, Godson Ollomi

Hifadhi ya Msitu wa Rau (RCFR) iliyopo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro ilianzishwa kutokana na tangazo la serikali Na. 127 0F 25/5/1951. Msitu huu asilia unapatikana kilometa tatu Kusini Mashariki mwa mji wa Moshi. Msitu asilia wa Rau umechukua eneo la hekta zipatazo 584 ambao ndani yake una mime na wanyama ambao wanatakiwa kutunzwa ipasavyo.

Pia una vyanzo  vya maji na hifadhi ya udongo wambao ni muhimu kwa ukuaji wa viumbe hao. Msitu huu asilia wa Rau una chemichemi sita za maji safi zinazotoka chini ya ardhi ambazo asili yake ni Mlima Kilimanjaro. Maji huifikia ikolojia ya msitu huo kupitia mito  iliyopo chini ya ardhi  ambayo ilijitokeza kutokana na mlipuko wa volkano iliyotengeneza mlima huo mrefu barani Afrika.

Msitu asilia wa Rau una aina mbalimbali za mimea ikiwamo Msoo (Oxystigma msoo- caelsalpinioideae ambao kwa ukanda wa Afrika Mashariki haupatikani popote isipokuwa Rau. Katika Afrika unaweza kuuona kwa wingi katika misitu ya Guinea-Kongo.)

Kulingana na Polhill mnamo mwaka 1968 alisema uwepo wa msoo umesababisha aina nyingine za miti kuendelea kujitokeza akiwa na maana kuwa unapoouona  msoo basi miti kama mivule (Milicia excelsa) na migunga (Acacia usambarensis) haikosekani eneo hilo. Aina nyingine inayopatikana hapo Rau ni Diospyros, Ficus Lecaniodiscus na Tapura fischer.

Rivina humilis

 Utafiti uliofanywa na Wakala wa Misitu  Tanzania (TFS) unaonyesha msitu asilia wa Rau una aina 37 za miti huku mivule ikishika eneo hilo kwa wingi.

Kwa upande wa aina za wanyama katika RCFR  una wanyama kama

1.     Mbega (wapo wa aina mbili wa bluu-Cercopithecus mitis, weupe-weusi-Simian polycomos)

2.     Swala

3.     Digidigi (Madoqua quentheri)

4.     Sungura

5.     Ngiri (Phacochoerus africanus)

6.     Panya wenye masikio makubwa kama ya Tembo

7.     Pongo (Madoqua kirkii na Madoqua piacentinii

8.     Popo

Chemichemi ya Maziwa ya Rau

Msitu Asilia wa Rau una insekta wa aina mbalimbali mbu weusi wa msituni, nyuki (Apis mellifera adansonii na Stingless bees-Mellipolina), buibui, bundi, panzi, siafu weusi, mchwa wa kwenye mapango, tandu, jongoo, beetles, vipepeo na Natriciteres sylvatia.

Aidha kuna ndege wanaopatikana katika mstu asilia wa Rau wanakadiriwa kuwa zaidi ya aina 50  wakiwamo African spoonbill, Suni birds, African paradise, Flycatcher,

King fisher's, African doves, Speckled, Mouse birds, African Jacana, Black-winged stilt, Black Smith lapwing, Heron, Hamerkop storks, Marabou storks, Ibises, Egrets na Grossy Ibis.

RCFR ina aina kuu tatu za nyoka ambao ni Chatu, Nyoka wa Kijani na Kifutu.

Mti aina ya Mvule

 Imetayarishwa na; Jaizmela kwa msaada wa TFS