“Hayo ni Maisha Yangu”; alisikika Mjapan mmoja akitamka mnamo Januari 26, 2025 katika viunga vya jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini baada ya kuwasili akitokea Nairobi, Kenya kwa mguu.
Cha kustaajabisha ni kwamba Mjapan huyo aliyefahamika
kwa jina la Yuji ‘Gump’ Suzuki aliwasili katika jiji hilo lililo umbali wa
kilometa 6,400 kutoka Nairobi, Kenya akiwa na mkokoteni wa matairi mawili
akiongozana na vijana wengine wawili wa Kijapan.
Mjapan Yuji mwenye umri wa miaka 34 aliwasili jijini Cape Town humo akitumia siku 210 sawa na takribani miezi saba tangu alipoianza safari yake mnamo Julai 2024, alipita nchini Tanzania, Zambia, Zimbabwe na Namibia kabla ya kuingia Afrika Kusini.
Mapema asubuhi ya Januari 26, 2025 akiwa na mkokoteni wake uliojizolea
umaarufu mkubwa wa ‘Rickshaw’ wenye uzito wa kilogramu 100; Yuji aliukokota kwa
furaha na kuwapongeza vijana wenzake kwa kumuunga mkono katika safari hizo za kitalii
“Nisingeweza kufanya bila ninyi ndugu zangu, ninatembea kwa
furaha, nimekuwa nikisafiri kwa miaka tisa sasa na nimekuwa nikiungwa mkono
nanyi hivyo narudisha kwenu. Hayo ni maisha yangu,” alisema Suzuki.
Yuji aliongeza kuwa changamoto za barabarani kubwa lakini iliyokuwa ngumu zaidi ni ya kupenya Jangwa la Namibia.
Kwa mujibu wa tovuti yake; mnamo mwaka 2016-2017 Yuji Suzuki; alitembea kutoka China hadi India pia kilometa 2,500 alizunguka barani Ulaya mnamo mwaka 2017; pia kilometa 5,100 nchini Marekani kati yam waka 2022-2023.
Mkokoteni wa magurudumu
mawili (Rickshaw) ulianza kutumika lini?
Rickshaw ya kwanza ilivumbuliwa nchini Ufaransa mwishoni mwa
karne ya 17; kwa ajili ya mahitaji ya usafiri licha ya uwepo wa aina nyingine
za vyombo vya usafiri. Miaka hiyo ya 1679 Ufaransa ilikuwa imeendelea sana
katika masuala ya usafiri aina ya “Omnibus”
ambazo zilikuwa zinafanana na waendeshaji wa mikokoteni ya kuuza mvinyo katika
mitaa ya jiji la Paris. Wakati huo mikokoteni hiyo ilikuwa ikisukumwa na watu
wawili mmoja anakuwa mbele akivuta na mwingine nyuma akisukuma. Huyu wa mbele
alikuwa akishikilia mbao fulani ikiwa ni sehemu ya kutafuta mizania na kuongoza
uelekeo anaoutaka.
Wasanii wa uchoraji hawakuwa nyuma Msanii Claude
Gillot alichora picha yake aliyoipa jina la “Les deux carosses” ambao ulionyesha
mikokoteni hiyo miwili; mchoro huo aliuchora mnamo mwaka 1707.
Katika ardhi ya Japan, wao walivumbua kivyao mnamo mwaka 1869
ambapo kipindi cha utawala wa Tokugawa (1603-1868) kulipigwa marufuku ya
matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia matairi ikiwamo mikokoteni. Wakati mikokoteni
ya Rickshaw ikianza ndio kipindi ambacho Japan ilikuwa imeanza kukua katika
masuala ya ufundi.
Izumi Yosuke anasalia kuwa mvumbuzi wa kwanza wa Rickshaw
nchini Japan akishirikiana na Suzuki Tokujiro na Takayama Kosuke ambao wote kwa
pamoja walipata wazo kutokana na namna magari ya Farasi yanavyofanya kazi,
miaka michache baadaye waliyaingiza mitaani na kuwa sehemu ya maisha kisha
kusambaa hadi China na kwingineko.
Credit to: Jabir Johnson/ JAIZMELA/Mashirika ya Habari/Wikipedia
+255 693 710 200
0 Comments:
Post a Comment