Sunday, January 5, 2025

China Communication Construction Company kuanza ujenzi barabara ya Ndungu-Mkomazi

 

Wakala wa barabara Nchini (TANROADS) wametakiwa kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa wazawa kwenye miradi ya ujenzi barabara na kuwawezesha vijana kupata ajira kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi .

Waziri wa ujenzi Abdalla Ulega ametoa agizo hilo alipokuwa Wilayani Same mkoani Kilimanjaro katika hafla ya kumkabidhi mkandarasi CHINA COMMUNICATION CONSTRUCTION COMPANY (CCCC) mradi wa ujenzi wa barabara ya Ndungu -Mkomazi yenye urefu wa kilomita 36 itakayo tengenezwa kwa kiwango Cha lami ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa serikali kuhakikisha Uwepo wa Maendeleo na ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

Ulega amesema ujenzi wa barabara hiyo utaondoa kero ya usafiri pia kuimarisha na kuchochea Kasi ya uchumi ,kilimo, biashara na utalii hususani kwa wananchi wote wa wilaya ya Same, Kanda ya kaskazini na Pwani.

"Serikali imetoa fedha zaidi ya bilioni 59 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ya Ndungu -Mkomazi itakayowakomboa wananchi kiuchumi hivyo vijana changamkieni fursa za ajira zitakazotokana na ujenzi wa barabara hii,zalisheni kwa wingi Mpunga,Tanga wizi na ndizi ili kukuza mtandao wa biashara Kati ya Same ,Mikoa ya Tanga na Pwani" amesema Waziri Ulega.

Kutokana na umuhimu mkubwa wa ujenzi wa barabara hiyo utakao rahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji amesisitiza vijana wa maeneo yanayopitiwa na mradi wa ujenzi kuchangamkia fursa za ajira zitokanazo na mradi huo.

Awali Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro amesema ujenzi wa barabara hiyo inayopita kwenye idadi kubwa ya wananchi Wilayani humo utarahisisha Maisha na kuibua fursa nyingi za kiuchumi .

Barabara ya Ndungu- Mkomazi ni Moja ya barabara muhimu hapa nchini hususani katika shughuli za Maendeleo zinazochochea uchumi wa nchi kupitia kilimo,utalii na biashara na kwa kuliona hilo serikali imeshakamilisha malipo ya awali takribani bilioni 5.8 kwa mkandarasi ili kuanza kazi rasmi ya ujenzi wa kilomita 36 kwa kiwango Cha lami.

Credit to: Elizabeth Mkumbo; Freelancer/JAIZMELA




0 Comments:

Post a Comment