Wakili Boniface Mwabukusi Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) |
Kushindwa kuandika wosia kumetajwa kama chanzo cha migogoro ya ardhi na mirathi
Akizungumza katika uzinduzi wa wiki ya sheria mnamo Januari 29, 2025 mkoani Kilimanjaro Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Wakili Boniface Mwabukusi alisema Migogoro ya ardhi na mirathi ni matatizo yanayoweza kutokea kutokana na sababu mbalimbali, na mara nyingi husababishwa na mifumo ya kijamii, kiuchumi, na kisheria.
“Huduma ya Msaada wa kisheria ni ibada, ni ibada kwasababu tunashughulika na maisha ya watu ya kila siku; ni wakati wa kuifanya kwa unyenyekevu na ukamilifu wake na kuelewa kwamba hata mitume wangekuwepo leo au Yesu angekuwa Kilimanjaro sehemu ya kwanza kufika ingekuwa hapa kwenye Legal Aid,” alianza Mwabukusi
Aidha Mwabukusi alisema kuwa kutokuwa na utaratibu mzuri katika kugawa mali za marehemu, kunakosababishwa na maelezo hafifu ya wosia, au kutokuwepo kwa wosia kabisa.
“Matatizo mwakubwa na changamoto ya legal yanayogusa wananchi yapo kwenye ardhi na mirathi, na yanachangiwa na utafsiri mbaya wa sheria au watu wakorofi tu na kwenye mirathi ni kwasababu hatupendi kuandika wosia,” alisisitiza Mwabukusi.
Mwabukusi aliongeza kuwa wakati mwingine, wanajamii wanachukulia kwamba wao wanastahili sehemu fulani ya ardhi au mali ya familia, na hivyo kuleta migogoro kuhusu nani anapaswa kumiliki nini.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu alithibitisha kuwepo kwa changamoto ya ardhi katika mkoa wake huku akitaja sababu ya ongezeko la watu na ardhi kuwa finyu.
“ Tuseme ukweli waliotanguliwa wanasema mkoa wa Kilimanjaro liko tatizo kubwa la ardhi....ni kweli....kwasababu ardhi yetu ni finyu; na ardhi hiyo ilishagawanywa kwa muda mrefu na waliokuwa nayo; na watu wanaongezeka na wazazi wanaendelea kuzaa, ili wagawane vihamba ndipo tatizo linapoanzia; ” alisema Babu.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema wananchi wanapoitafuta haki wanaonyesha ustaarabu na ndio sababu ya kufanyika kwa kampeni ya utoaji wa msaada wa kisheria nchini iliyoratibiwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Watu hawa wanajitokeza kwa wingi katika kampeni hii ya Mama Samia Legal Aid kwasababu wanaitafuta haki ili wakidhi kiu yao; ya kupata haki, Ukiona wananchi wanaitafuta haki kwanza ni kuwapongeza sana kwasababu wananchi hao wamestaarabika; tunakwenda kuhakikisha Mama Samia Legal Aid inaleta Haki ambayo italiinua taifa,” alisema Dkt. Ndumbaro.
Kauli mbiu mwaka huu katika wiki na siku ya Sheria, “ Tanzania ya 2050; Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”