Sunday, November 3, 2024

Shujaaz yatinga vijijini kuwahamasisha vijana wa kike kujihusisha kwenye Kilimo na Ufugaji

Kuna sababu kadhaa ambazo zinaweza kuchangia vijana wa kike wasijihusishe sana na kilimo na ufugaji; Miongoni mwa hizo mitazamo kwa baadhi ya jamii kwamba kazi za kilimo na ufugaji ni za kiume, Ukosefu wa upatikanaji wa Rasilimali; Elimu ya kutosha kuhusu faida za kilimo na ufugaji au jinsi ya kuendesha shughuli hizo kwa ufanisi pia mabadiliko ya muktadha wa kiuchumi

Hivyo basi ni kwa namna gani vijana hususani wa kike katika wilaya za Hai na Siha wataweza kujikita katika tasnia ya kilimo na ufugaji, Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) na Taasisi ya Vijana ‘Shujaaz’ kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimekuja na suluhisho la pamoja kwa ajili ya vijana hao.

Akizungumza na vyombo vya habari, Ngarenairobi, West Kilimanjaro hivi karibuni Meneja wa Shujaaz Alan Lucky Komba alisema malengo ya mradi huo ni kufanya semina mbalimbali kwa vijana wakishirikiana na viongozi wa serikali katika maeneo husika ili kuongeza uelewa wao kuhusu kilimo na ufugaji na kubaini changamoto zinazowakabili vijana hao kwenye tasnia hiyo.

“Kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana wa kike hususani changamoto za kijamii na kijinsia hivyo tumefika katika jamii husika na  ushirikishwaji wa viongozi wa serikali, viongozi wa dini na viongozi wa kimila utachangia kwa kiasi kikubwa utatua,” alisema Lucky.

Mnufaika wa semina hizo Reina Mrema, mkazi wa Ngarenairobi, alisema kinachowatatiza vijana ni elimu na ufahamu kwa upana wake kuhusu masuala ya Kilimo na Ufugaji wa kisasa ambao ukifanyika vizuri unawainua kiuchumi.

 "Kila kijana mwenye umri wa miaka kuanzia 18 Hadi 35 asikimbilie kwenye bodaboda na badala yake anatakiwa kuona ufugaji Wa kuku Kama fursa,Kama kazi ya ofisini   kwa kuamua na kuwekeza  nguvu kazi katika ufugaji na niwahakikishie hakuna atakaejuta kwani ufugaji Wa kuku unalipa"alisema Reina.

Awali katika semina iliyofanyika mtaa wa amani wilayani Hai, Afisa mifugo wilayani humo Fraten Mtika alisema uongozi wa wilaya hiyo umejipanga kuhamasisha na kutoa elimu ya ujasiriamali, kuwawezesha kwa kuwapa vijana mikopo ya kwenye halmashauri na kuwatafutia masoko rasmi ili kurahisisha ukuaji wa uchumi kwa kijana Wa kike watakaokuwa na nia ya kufanya biashara na ufugaji wa kuku.

Mradi huo hadi sasa umefanya semina katika maeneo 8 tofauti katika wilaya za Hai na Siha ambazo ni  Mtaa wa Amani, Mtaa wa Nyerere, Mtaa wa Uzunguni, Mtaa wa kibaoni, kijiji cha Kyeri, na kijiji cha Foo katika wilaya ya Hai, kijiji cha Lawate na kijiji cha Ngarenairobi katika wilayani Siha.

Kwa mawasiliano zaidi: 
+255 693 710 200; 
Kitengo cha Habari, JAIZMELA
Reina Mrema, mkazi wa Ngarenairobi, Siha

Alan Lucky, Meneja wa Shujaaz









0 Comments:

Post a Comment