Monday, November 11, 2024

KADCO, APM lawamani manunuzi ye jenereta mbili, Takukuru yaokoa Mil. 329

 



Sintofahamu ya ununuzi wa majenereta katika Kampuni ya Uendeshaji na Uendelezwaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), imetatuliwa baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro kusimamisha ulipaji wa malipo ya jenereta.

Kadco iliagiza majenereta mawili yenye thamani ya milioni mia tatu ishirini na tisa, laki nne, sabini na tisa elfu mia sita (Tshs. 329, 479,600/=) kutoka Kampuni ya African Power Machinery (APM) iliyopo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro Mkuu wa Takukuru mkoani humo Mussa Chaulo alisema uchunguzi umebaini kuwa kampuni ya APM iliwauzia majenereta feki na kwamba zilipakwa rangi tu.

“Jenereta zilizowasilishwa  zilikuwa na mapungufu kadhaa, ikiwa ni pamoja na cable zilizotakiwa kuwa tofauti  na zilizowasilishwa na injini zake zilikuwa za zamani,” alisema Mussa Chaulo.

Chaulo aliongeza kuwa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro ilibaini kuwa maeneo mengi ya jenereta hizo yalikuwa na kutu  na maeneo mengine yalikuwa yamepakwa rangi.

“Takukuru tumefanya udhibiti juu ya manunuzi ya jenereta hizo  mbili na kuzuia malipo kufanyika kwa kampuni iliyosambaza jenerator hizo na hivyo tumeokoa shilingi 329,479,600/= ambazo zingetumika kulipa jenereta zisizo na ubora kulingana na mahitaji yaliyoanishwa,” aliongeza Chaulo.

Kadco imekuwa ikiendesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa takribani miaka 26 sasa tangu iliposajiliwa mnamo mwaka 1998 licha ya vuta nikuvute na hapa na pale.

Novemba 10, 2023 shughuli za uendeshaji wa KIA zilikabidhiwa kwa TAA ambapo ilidumu hadi Aprili 2024 ilitangazwa tena kuwa KADCO itarudi kuendelea na shughuli zake katika uwanja wa KIA.

Miezi 3 tu baada ya KADCO kusajiliwa mnamo tarehe 17 Julai 1998), iliingia mkataba mpya wa umiliki wa hisa, ambapo serikali ya Tanzania ilipata 24% ya hisa za kampuni, Mott MacDonald International Ltd (41.4%), South Africa Infrastructure Fund (30). %) na Inter Consult (T) Ltd (4.6%).

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema Kadco imekuwa kivuli cha wapigaji hivyo kununuliwa kwa majenereta feki ni kielelezo kwamba ubadhirifu bado unaendelea katika Uwanja wa Ndege wa KIA.

0 Comments:

Post a Comment