MBUNGE wa Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi, Januari 7, 2021 alikabidhi mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya kuharakisha ukamilishaji wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Mpirani na Mabogini zilizopo katika Kata ya Mabogini wilayani humo, zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa.
Aidha Mbunge huyo pia alikabidhi kiasi cha Sh. milioni moja katika shule ya Sekondari Cyril Chami iliyopo Kata ya Kibosho Mashariki kwa ajili ya kununu bati za kuezekea madarasa, hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika mbele ya Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Moshi Juma Tukosa, kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Kastori Msigala.
“Mimi kama mdau wa maendeleo nimeguswa na changamoto hii nikaona ni vema nikachangia kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa saba ambayo yanapungua katika shule ya sekondari Mpirani na Mabogini, ili hawa watoto wetu waende shule ili waeze kufanikisha azma yao ya elimu ambayo serikali inapambana ili kila mtoto anayestahili aweze kwenda sekondari,”alisema Mbunge Ndakidemi.
Aliongeza “Kata ya Mabogini ndiyo Kata pekee yenye changamoto ya upunguzu wa vyumba vya madarasa, baada ya kuliona hili nimeguswa kuchangia mifuko ya saruji 100 ambapo shule ya sekondari Mabogini nimewapatia mifuko 40 na shule ya Mpirani mifuko 60 ya saruji,”alisema.
Ndakidemi alisema shule ya sekondari Mabogini inakabiliwa na upungufu wa vymba vya madarasa matatu, huku shule ya Mpirani ikikabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa manne.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Moshi Juma Tukosa, alisema halmashauri hiyo inazo jumla ya shule za sekondari 98, kati ya hizo shule 59 ni shule za serikali na kwamba shule tatu kati ya hizo 59 ni kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
“Halmashauri ya Moshi inajumla ya shule za sekondari 98, kati ya hizo shule za sekondari za serikali ziko 59, zinazoendeshwa na na taasisi za binafsi na madhehebu ya kidini ziko 39, shule 59 za serikali tulizonazo shule tatu ni kwa ajili ya kidato cha tano na sita,”alisema Mwl Tukosa.
Alisema idadi ya wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha kwanza 2021 ni wanafunzi 7,923 kati ya hao wanafunzi 350, walikuwa hawajachaguliwa kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa, ambapo upungufu huo wa vyumba vya madarasa upo katika Kata ya Mabogini yenye shule mbili za sekondari.
Akizungumzia msaasa huo wa saruji ulitolewa na Mbunge, ambao unakwenda kuchagiza ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya kupokea wanafunzi kwa muhura wa masomo 2021 Makamu mkuu wa shule ya Sekondari Mpirani Mwl Remmy Kaganga, alisema “Mifuko 60 ya saruji iliyotolewa itatusaidia sana kwa ujenzi wa madarasa manane ambayo tunayajenga kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza,”alisema Kaganga.
Alisema “Tunahitaji madarasa manane ili tutosheleza wanafunzi 596, waliopangwa katika shule yetu, pia tunaishukuru serikali ambayo imetusaidia Sh. milioni 47 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba mawili vya madarasa kwa Sh. milioni 40 na choo kitakachogharimu kiasi cha Sh. milioni 7, ”alisema.
Hata hivyo Makamu huyo wa shule aliishukuru Halmashauri ya Moshi kwa kuwapati Sh Ml. 15 kwa ajili ya kutengeneza madawati ya kidato cha kwanza kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuwapokea.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Chekereni Kamili Kishingo, alisema shule ya sekondari Mabogini inauhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa zaidi ya saba kulingana na uhitaji ikiwemo hostel, pamoja na maabara.