Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Sunday, November 24, 2024

Wananchi watakiwa kutunza mazao ya chakula kukabiliana na mabadi

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro Dankan Urasa.


Wananchi wametakiwa kutunza mazao ya chakula waliozalisha na  kuweka akiba ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa chakula inayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza katika  kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 cha baraza la madiwani, mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro Dankan Urasa katika  humo alisema;

"Msimu uliopita hali ya mavuno ya chakula haikuwa ya kuridhisha na kusababisha upungufu wa chakula hivyo nawaomba madiwani kutilia mkazo kwa  kusisitiza  wananchi kutunza chakula pia kuendelea kulima  na kupanda mazao yanayostahimili ukame "amesema Urassa.

Aidha Urasa alitoa rai kwa  wataalamu na viongozi  katika Ofisi ya Mkurugenzi wa wilaya hiyo kusimamia  utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ambayo inaendelea Wilayani humo ili ikamilike kwa wakati ikiwemo mradi wa ujenzi wa kituo Cha afya Lawate,shule ya wasichana Kilimanjaro girls na shule ya Amani kata ya Ndumet.

Urassa aliwasisitiza wananchi kutunza miundombinu ya barabara kwa kuacha kupitisha mifugo kwenye barabara pia kuwaomba wakala wa maji Safi na mazingira vijijini ( RUWASA) na wakala wa barabara za Mijini na vijijini (TARURA) kushirikiana kwa pamoja ili kutatua Changamoto ya uharibifu wa miundombinu ya Maji inayotokea wakati wa matengenezo ya barabara.

Kikao hicho cha robo ya Kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 kilifanyika katika  ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya halmashauri hiyo.

USULI KUHUSU MABADILIKO TABIANCHI

Mabadiliko ya tabia nchi (pia huitwa "mabadiliko ya hali ya hewa") yanarejelea mabadiliko katika mifumo ya hali ya hewa duniani, ambayo hutokea kwa kipindi cha muda mrefu. Mabadiliko haya yanaweza kuwa ya asili, lakini kwa sasa, mabadiliko makubwa yanayoshuhudiwa yanahusiana na shughuli za binadamu, hasa utoaji wa gesi chafuzi kama vile kaboni dioksidi (CO2), metani (CH4), na oksidi za nitrojeni (NOx).

Hii ni mifano ya athari za mabadiliko ya tabia nchi:

  1. Kuongezeka kwa joto duniani: Hii ni matokeo ya kupanda kwa kiwango cha gesi chafuzi angani, ambayo hufanya joto la dunia kuongezeka, na kusababisha ongezeko la joto kwenye sayari yetu.

  2. Mabadiliko katika mvua na ukame: Mabadiliko ya tabia nchi yanaweza kusababisha maeneo fulani kupokea mvua nyingi zaidi wakati mwingine kuathiriwa na ukame wa muda mrefu. Hii inaathiri kilimo, upatikanaji wa maji, na bioanuwai.

  3. Kupanda kwa kiwango cha bahari: Kwa sababu ya joto kuongezeka, barafu za polar na theluji kwenye milima zinayeyuka, na kuongeza kiasi cha maji baharini. Hii inaweza kusababisha maeneo ya pwani kuwa hatarini kwa mafuriko.

  4. Mabadiliko katika mifumo ya maisha ya wanyama na mimea: Wanyama na mimea wanahitaji mazingira maalum ili kuishi. Mabadiliko ya tabia nchi yanayohusisha joto, mvua, na makazi yanaweza kuathiri bioanuwai, na kusababisha aina fulani kuhamia sehemu nyingine au kutoweka kabisa.

Mabadiliko haya ni tishio kubwa kwa ustawi wa binadamu, jamii, na mazingira. Kwa hiyo, kuna juhudi nyingi duniani kote kutafuta suluhisho la kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha mifumo ya nishati, usafiri, na kilimo ili kudhibiti ongezeko la joto na kuzuia madhara zaidi.

Mabadiliko ya tabia nchi yanaweza kusababisha maeneo fulani kupokea mvua nyingi zaidi wakati mwingine kuathiriwa na ukame wa muda mrefu. Hii inaathiri kilimo, upatikanaji wa maji, na bioanuwai.


Thursday, November 14, 2024

Mwanaume ajinyonga Pasua, Moshi; Uchunguzi unaendelea

Mwili wa Marehemu Hassan Ali ukiwa chini kabla ya kuondolewa na Jeshi la Polisi Tanzania mnamo Novemba 14, 2024 katika eneo la Nelson Mandela, Pasua mjini Moshi. 

Mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 amefariki dunia kwa kujinyonga katika mti eneo la Nelson Mandela mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, kwa kile kinachosadikika kuwa ni kujinyonga kwa kamba za katani pembezoni mwa uwanja wa Nelson Mandela; Pasua mjini Moshi.

Tukio hilo ni la tatu katika eneo hilo la Pasua kwa mwaka huu la watu kuchukua uamuzi mbaya wa kujinyonga kutokana na sababu mbalimbali.

Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia EATV kuwa marehemu alikutwa asubuhi ya Novemba 14, 2024 akiwa amelala chini baada ya tawi la mti kukatika na kumbwaga chini huku wengine wakidai chanzo cha umauti ni kukata tamaa ya maisha na mahusiano ya kimapenzi.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro lilifika eneo la tukio baada ya wananchi kutoa taarifa kuhusu kukutwa kwa mwili huo katika eneo la Nelson Mandela ambapo mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika Hospitali ya KCMC

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro SACP Simon Maigwa alitoa wito kwa wananchi.

"Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa mapema kwenye taasisi zenye mamlaka ya kushughulikia migogoro ya ndoa ili kuepeusha misongo ya mawazo inayopelekea kutoa maamuzi magumu ikiwa ni pamoja na kusababisha mauaji na kujitoa uhai," alisema SACP Maigwa. 

Hata hivyo baadhi ya wakazi mjini Moshi wametoa maoni ili kupata mwarobaini wa changamoto ya kuchukua maamuzi magumu kutokana na kuhisi kuwa maisha yao hayana maana yoyote au hawaoni sababu ya kuendelea kuishi.

Suala la kujinyonga linaendelea kuwa changamoto kubwa katika jamii nyingi, likihusisha masuala ya kiuchumi, kijamii, na kisaikolojia.

Credit to: Yesse Tunuka, Ombeni Mjema, Johnson Jabir; JAIZMELA



Monday, November 11, 2024

KADCO, APM lawamani manunuzi ye jenereta mbili, Takukuru yaokoa Mil. 329

 



Sintofahamu ya ununuzi wa majenereta katika Kampuni ya Uendeshaji na Uendelezwaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), imetatuliwa baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro kusimamisha ulipaji wa malipo ya jenereta.

Kadco iliagiza majenereta mawili yenye thamani ya milioni mia tatu ishirini na tisa, laki nne, sabini na tisa elfu mia sita (Tshs. 329, 479,600/=) kutoka Kampuni ya African Power Machinery (APM) iliyopo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro Mkuu wa Takukuru mkoani humo Mussa Chaulo alisema uchunguzi umebaini kuwa kampuni ya APM iliwauzia majenereta feki na kwamba zilipakwa rangi tu.

“Jenereta zilizowasilishwa  zilikuwa na mapungufu kadhaa, ikiwa ni pamoja na cable zilizotakiwa kuwa tofauti  na zilizowasilishwa na injini zake zilikuwa za zamani,” alisema Mussa Chaulo.

Chaulo aliongeza kuwa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro ilibaini kuwa maeneo mengi ya jenereta hizo yalikuwa na kutu  na maeneo mengine yalikuwa yamepakwa rangi.

“Takukuru tumefanya udhibiti juu ya manunuzi ya jenereta hizo  mbili na kuzuia malipo kufanyika kwa kampuni iliyosambaza jenerator hizo na hivyo tumeokoa shilingi 329,479,600/= ambazo zingetumika kulipa jenereta zisizo na ubora kulingana na mahitaji yaliyoanishwa,” aliongeza Chaulo.

Kadco imekuwa ikiendesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa takribani miaka 26 sasa tangu iliposajiliwa mnamo mwaka 1998 licha ya vuta nikuvute na hapa na pale.

Novemba 10, 2023 shughuli za uendeshaji wa KIA zilikabidhiwa kwa TAA ambapo ilidumu hadi Aprili 2024 ilitangazwa tena kuwa KADCO itarudi kuendelea na shughuli zake katika uwanja wa KIA.

Miezi 3 tu baada ya KADCO kusajiliwa mnamo tarehe 17 Julai 1998), iliingia mkataba mpya wa umiliki wa hisa, ambapo serikali ya Tanzania ilipata 24% ya hisa za kampuni, Mott MacDonald International Ltd (41.4%), South Africa Infrastructure Fund (30). %) na Inter Consult (T) Ltd (4.6%).

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema Kadco imekuwa kivuli cha wapigaji hivyo kununuliwa kwa majenereta feki ni kielelezo kwamba ubadhirifu bado unaendelea katika Uwanja wa Ndege wa KIA.

Monday, November 4, 2024

Al Mahboob a.k.a ya Dkt. Hassan Abbas

 


Dkt. Hassan Abbas au Dkt. Hassan Abbas Mahboob?

A.K.A, au "Also Known As," ni jina linalotumika mara nyingi kuelezea majina au mitindo mingine ambayo mtu anaweza kuwa nayo. Katika muktadha wa historia ya falsafa, "A.K.A" inaweza kutumika kuashiria mtu au wazo lililo na majina tofauti.

Katika historia, watu maarufu au wasanii mara nyingi hutumia "A.K.A" kutoa majina yao mengine au majina ya jukwaani.

Kwa mfano, msanii wa hip-hop anaweza kuwa na jina la kuzaliwa lakini akatumia jina tofauti katika tasnia ya muziki. Katika muktadha wa sheria au wanasiasa, "A.K.A" inaweza kutumika kutambulisha majina ambayo yanaweza kuwa maarufu zaidi kwa umma.

Katika muktadha wa historia, watu wengi maarufu wamekuwa wakitumia "A.K.A" ili kutambulisha majina yao mengine au majina ya utani. Hapa kuna baadhi ya mifano:

Malcolm X: Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Malcolm Little, lakini alijulikana kama Malcolm X, ambapo "X" lilimwakilisha kutokujulikana kwa asili yake.

Marilyn Monroe: Alizaliwa kama Norma Jeane Mortenson, lakini akapata umaarufu mkubwa kwa jina lake la jukwaa, Marilyn Monroe.

Notorious B.I.G.: Jina lake halisi lilikuwa Christopher Wallace, lakini alikuwa maarufu kwa jina lake la jukwaa, Notorious B.I.G., na pia alijulikana kama Biggie Smalls.

Freddie Mercury: Alizaliwa kama Farrokh Bulsara, lakini alipata umaarufu mkubwa kama mwanamuziki wa rock chini ya jina la Freddie Mercury.

Elvis Presley: Ingawa jina lake lilikuwa Elvis Aaron Presley, alijulikana pia kwa majina kama "The King of Rock and Roll" au "The King."

Mifano hii inaonyesha jinsi "A.K.A" inavyotumiwa kuonyesha majina yanayojulikana zaidi au majina ya utani ambayo yanabeba maana maalum katika muktadha wa maisha na kazi za watu hawa.

Inaweza kukustaajabisha kwa kiongozi wa serikali nchini Tanzania Dkt. Hassan Abbas ambaye katika serikali ya awamu ya sita ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kujipachika A.K.A…..

Dkt. Hassan Abbas amejipachika A.K.A ya Al Mahboob…hapo sasa; Ilikuwa Novemba Mosi, 2024 katika Mahafali ya 27 ya wanafunzi wa Chuo cha Viwanda vya Misitu  (FITI) mjini Moshi ambako alivutiwa na utenzi wa wanachuo. 

Dkt. Hassan Abbas akawajibu na kujiita Dkt. Hassan Abbas Al Mahboob… Imekaaje hiyo?

Neno "Al Mahboob" linatokana na lugha ya Kiarabu na lina maana ya "mpendwa" au "wapendwa." Katika muktadha wa Kiarabu, neno hili linaweza kutumika kuelezea mtu anayepewa upendo mkubwa au heshima, kama vile mpendwa wa moyo au rafiki wa karibu.

Mara nyingi  "Al Mahboob" hutumika kama jina la mtu, hasa katika tamaduni za Kiarabu; pia Neno hili linaweza kutumika katika mashairi au hadithi kuelezea hisia za upendo au kiini cha uhusiano wa karibu.

Al Mahboob; Wengi wa wasanii wa Kiarabu wanaweza kutumia neno hili katika nyimbo zao kama sehemu ya kuelezea hisia za upendo.

Kwa hivyo, "Al Mahboob" ni neno lenye uzito wa kihisia na linatumika katika muktadha tofauti ili kuonyesha upendo na heshima.

Hongera Dkt. Hassan Abbas Al Mahboob……Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Sunday, November 3, 2024

Shujaaz yatinga vijijini kuwahamasisha vijana wa kike kujihusisha kwenye Kilimo na Ufugaji

Kuna sababu kadhaa ambazo zinaweza kuchangia vijana wa kike wasijihusishe sana na kilimo na ufugaji; Miongoni mwa hizo mitazamo kwa baadhi ya jamii kwamba kazi za kilimo na ufugaji ni za kiume, Ukosefu wa upatikanaji wa Rasilimali; Elimu ya kutosha kuhusu faida za kilimo na ufugaji au jinsi ya kuendesha shughuli hizo kwa ufanisi pia mabadiliko ya muktadha wa kiuchumi

Hivyo basi ni kwa namna gani vijana hususani wa kike katika wilaya za Hai na Siha wataweza kujikita katika tasnia ya kilimo na ufugaji, Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) na Taasisi ya Vijana ‘Shujaaz’ kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimekuja na suluhisho la pamoja kwa ajili ya vijana hao.

Akizungumza na vyombo vya habari, Ngarenairobi, West Kilimanjaro hivi karibuni Meneja wa Shujaaz Alan Lucky Komba alisema malengo ya mradi huo ni kufanya semina mbalimbali kwa vijana wakishirikiana na viongozi wa serikali katika maeneo husika ili kuongeza uelewa wao kuhusu kilimo na ufugaji na kubaini changamoto zinazowakabili vijana hao kwenye tasnia hiyo.

“Kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana wa kike hususani changamoto za kijamii na kijinsia hivyo tumefika katika jamii husika na  ushirikishwaji wa viongozi wa serikali, viongozi wa dini na viongozi wa kimila utachangia kwa kiasi kikubwa utatua,” alisema Lucky.

Mnufaika wa semina hizo Reina Mrema, mkazi wa Ngarenairobi, alisema kinachowatatiza vijana ni elimu na ufahamu kwa upana wake kuhusu masuala ya Kilimo na Ufugaji wa kisasa ambao ukifanyika vizuri unawainua kiuchumi.

 "Kila kijana mwenye umri wa miaka kuanzia 18 Hadi 35 asikimbilie kwenye bodaboda na badala yake anatakiwa kuona ufugaji Wa kuku Kama fursa,Kama kazi ya ofisini   kwa kuamua na kuwekeza  nguvu kazi katika ufugaji na niwahakikishie hakuna atakaejuta kwani ufugaji Wa kuku unalipa"alisema Reina.

Awali katika semina iliyofanyika mtaa wa amani wilayani Hai, Afisa mifugo wilayani humo Fraten Mtika alisema uongozi wa wilaya hiyo umejipanga kuhamasisha na kutoa elimu ya ujasiriamali, kuwawezesha kwa kuwapa vijana mikopo ya kwenye halmashauri na kuwatafutia masoko rasmi ili kurahisisha ukuaji wa uchumi kwa kijana Wa kike watakaokuwa na nia ya kufanya biashara na ufugaji wa kuku.

Mradi huo hadi sasa umefanya semina katika maeneo 8 tofauti katika wilaya za Hai na Siha ambazo ni  Mtaa wa Amani, Mtaa wa Nyerere, Mtaa wa Uzunguni, Mtaa wa kibaoni, kijiji cha Kyeri, na kijiji cha Foo katika wilaya ya Hai, kijiji cha Lawate na kijiji cha Ngarenairobi katika wilayani Siha.

Kwa mawasiliano zaidi: 
+255 693 710 200; 
Kitengo cha Habari, JAIZMELA
Reina Mrema, mkazi wa Ngarenairobi, Siha

Alan Lucky, Meneja wa Shujaaz