Makala yaliyopita tuliangazia namna kocha Ron Davis
alivyoamka asubuhi mjini Edmonton na ndoto ya maisha yake kubadilika pale
alipokutana na mwanariadha wa kwanza aliyeipa medali ya kwanza Tanzania Filbert
Bayi na baadaye kocha Sulus.
Tukio hilo lilitokea mwaka 1978 kwenye michuano ya Jumuiya ya
Madola ilifanyika mjini Edmonton, Alberta nchini Canada ambako Tanzania
ilishiriki. Ron Davis alikuwapo Edmonton kama kocha wa Nigeria ambayo ilikacha
kushiriki baada ya kutoka All Africa Games jijini Algiers. Katika makala haya
tutaendelea na safari ya Ron Davis kilichofuata baada ya kupokea miadi kutoka
kwa Kocha Sulus.
Ron Davis anasema, “ Sulus alinipigia simu siku chache
baadaye na kuniambia kuwa Waziri wa Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Chadiel
Mgonja anapenda kukutana na mimi.”
Wakati huo Ron Davis alikuwa bado kocha wa timu ya taifa ya
Nigeria, na tukio hilo lilimfanya sasa aanze kuwa karibu kwani hakutegemea kuwa
ingeweza kuwa muujiza mkubwa wa yeye ambao ulikuwa akiusubiri kwa miaka mingi.
Ron Davis alijiuliza maswali mengi kwamba je asubuhi ile
katika viunga vya Edmonton nchini Canada akimsemesha Bayi wakati akifanya
mazoezi yake kama utani tu ndio imekuwa kitu kamili.
Ilimstaajabisha sana raia huyo wa Marekani. Aidha tukio hilo
la kupigiwa simu liliweza kudakwa na magazeti ya Canada wakati ule kwani
walikuwa wakimfahamu vizuri Ron Davis kwani aliwahi miaka ya nyuma kuwapo huko
Alberta kwa kama mkurugenzi wa michezo.
MAZUNGUMZO
NA GAZETI LA CANADA
Kukutana na Waziri Mgonja ilikuwa habari kubwa sana kwa
wanahabari nchini Canada na waliomba kukutana naye kwa ajili ya mahojiano.
Lakini Ron Davis anakiri kwamba mahojiano yale yalitaka kumtokea puani kutokana
na kwamba alikuwa bado na kibarua na taifa la Nigeria.
Wanahabari walitaka kujua kutoka kwake sababu za Nigeria
hatohudhuria michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola mjini Edmonton. Ron Davis
anasema, “Mojawapo ya vitu nilivyosema ilikuwa ni kwamba maofisa wa Nigeria
ndio walioamua kutoshiriki michuano hiyo.”
Kwa taarifa yako jibu hilo lilitosha kujaa kwenye kurasa za
magazeti ya Canada siku iliyofuata na kusomwa na watu wengi nchini humo. Ron
Davis anasema alishindwa kumjibu mwandishi wa habari katika muktadha wa
kisiasa.
Kwa muktadha wa kisiasa jibu lingekuwa siku zote Nigeria iko
mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya vitendo vya ubaguzi wa rangi na
kukosekana kwao ni sehemu ya msimamo wa viongozi kuhusu vitendo hivyo.
Baada ya tukio hilo alikutana na Abraham Ordia ambaye alikuwa
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Nigeria na Rais wa Baraza Kuu la Michezo
barani Afrika. Ordia alimwambia kuwa hajapendezwa na baadhi ya kauli alizozitoa
kwenye vyombo vya habari na kumtaka asizungumze tena na vyombo vya habari akiwa
nchini Canada labda kwa makubaliano maalum.
Ron Davis anasema aliomba radhi kutokana na makosa hayo
ambayo yalimfanya hata yeye mwenyewe ajisikie vibaya.
AKUTANA NA
CHADIEL MGONJA
Hatimaye siku iliwadia pale alipokutana na Waziri Mgonja. Ron
Davis anasema, “Nilifurahi sana kukutana na Mgonja na ilipendeza sana.”
Katika mahojiano yao Ron Davis alijisemea moyoni endapo
atafanikiwa kuajiriwa na serikali ya Tanzania utakuwa uhusiano ambao
hautavunjika kamwe. Mafanikio aliyoyapata akiwa na Nigeria ilikuwa pointi
muhimu ambayo ilimpa nafasi ya kuwa kocha wa Tanzania.
Mgonja alionyesha wazi kuwa alikuwa na mipango mikubwa kwa
ajili ya Tanzania pale alipomwambia kuwa anamtaka Ron Davis kwa ajili ya kuwa
kocha wa timu ambayo itashiriki michuano ya Olimpiki mwaka 1980.
Katika mkutano wake na Mgonja kulikuwapo na mjumbe wa ubalozi
wa Tanzania. Kila kitu kilifikiwa kuhusu uhamisho wake na namna ya kufanya kazi
Tanzania. Ron Davis alitoa taarifa zake hali hiyo ilimfanya ajione kuwa
anatembea angani kutokana na furaha isiyo kifani na tabasamu lililojaa
matumaini makubwa ya kufanya kazi Tanzania.
Akiwa Edmonton alimshuhudia na alijua kuwa Bayi angekimbia
fainali za mita 1500. John Carlos na rafiki zake waliungana naye kuona namna
Bayi atakapofika kwenye kinyang’anyiro.
Ron Davis alimuona Bayi akianza kwa nguvu lakini katika mita
100 za mwisho Mwingereza Dave Morcroft alimburuza na kutwaa medali ya dhahabu
na kusalia kuwa na medali ya fedha. Kitendo hicho kilimuuma sana Ron Davis,
Carlos na wenzake kwani hawakutarajia kama angepitwa.
Wakiwa katika hali uchungu wa uwanjani zilikuja taarifa
nyingine kuwa mke wa John Carlos alikuwa amefariki dunia, sasa hapo ikawa
habari nyingine chungu zaidi na suala la Bayi likafutika kwenye vichwa vyao.
Ron alirudi Nigeria na kuaga vizuri kisha safari ya Tanzania
ikaanza baada ya kupewa taarifa kwamba amechaguliwa kuwa kocha mkuu wa Timu ya
Taifa katika mbio za uwanja.
Alipotua Tanzania alishangazwa na umati wa wanahabari katika
Uwanja wa Ndege wakimsubiri kwa shauku. Kilichomstaajabisha alikuwa hajawahi
kuona hapo kabla. Ilikuwa ngumu kuamini kwani watu hawakuficha shauku na
matarajio yao kwake katika medani ya riadha.
Makala haya
yametayarishwa na Jabir Johnson ambaye alipata fursa ya kuzungumza na Ron
Davis katika masuala mbalimbali ya
maisha yake na medani ya riadha alipotua nchini Tanzania. Kwa maoni ushauri
barua pepe: jaizmela2010@gmail.com
0 Comments:
Post a Comment