NA JEMAH MAKAMBA
|
Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya ya Chalinze Anthony Nyange (aliyesimama) akizungumza katika semina hiyo |
JAMII imetakiwa kuungana na
taasisi zisizo za kiserikali katika vita dhidi ya rushwa ya ngono katika maeneo
ya kazi ili kuiweka nchi katika nafasi nzuri kimaendeleo.
Akizungumza katika semina ya
uwezeshaji iliyofanyika Miono wilayani Chalinze, Pwani hivi karibuni Afisa
Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo Anthony Nyange alisema rushwa ya ngono
imesababisha madhara makubwa katika jamii.
“Rushwa ya Ngono imekuwa sugu
nchini kutokana ugumu uliopo katika kumgundua mhusika, bila nguvu ya jamii
pamoja na NGO’s hizi vita hii itakuwa ngumu kuikabili na itawatafuna watoto
wetu hususani wa kike,” alisema Nyange.
Katika semina hiyo iliyoandaliwa
na na Shirika la Maendeleo ya Wajasiriamali Miono (SHIMAWAMI) kwa msaada wa
Women Fund Tanzania (WFT), Nyange aliweka bayana kuwa taasisi zinazoendesha
harakati mbalimbali za kimaendeleo ni muhimu kwani zinaikumbusha serikali
ulazima wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Nyange alisisitiza kuwa
umaridadi umekuwa ukitumiwa na wengi kutenda maovu kutokana na uvivu miongoni
mwa wanawake, tamaa, ukosefu wa sifa kwenye ajira na uwezo wa kifedha.
Hata hivyo Nyange
aliwakumbusha washiriki akali wa 65 wa SHIMAWAMI kuwa utafiti umeonyesha wanawake na wasichana wengi
wamekuwa wakikosa sifa katika maeneo ya kazi lakini wameendelea na kazi
kutokana na mahusiano ya kimapenzi na mabosi wao.