HAI, KILIMANJARO
Baada ya Kura za Maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Hai mkoani Kilimanjaro
kufanyika mengi yameibuka baada ya baadhi ta majina ya wagombea kushindwa
kupenya katika ngazi ya udiwani huku kidole cha lawamani kikielekezwa katika
ngazi ya chama kwa kile kinachodaiwa kuwabeba baadhi ya wagombea katika kura za
maoni.
Baadhi ya wanachama wa CCM wilayani humo (majina yao
yamehifadhiwa) wamekiri kuwa mchakato wa kura za maoni uliofanyika hivi
karibuni katika wilaya ya Hai haukwenda
kama ilivyotarajiwa kutokana na
dosari mbalimbali kujitokeza.
Wanachama hao wanadai kuwa wakurugenzi wa uchaguzi
walikuwa wakionyesha hisia zao kwa mgombea
badala ya kuwa wasimamizi wa zoezi zima la kura za maoni.
“Kwa mujibu wa muundo wa chama, makatibu wa kata ndio watendaji na kwa nyakati za uchaguzi hugeuka kuwa
wasimamizi wa haki na taratibu. Lakini katika uchaguzi huu makatibu wa kata
waliweka kando dhamana hiyo na kuwa wapambe wa mgombea ubunge Saashisha
Mafuwe,” alisema mwanachama wa CCM.
Aidha baadhi ya wanachama hao wa CCM walidai kuwa siku
ya kura za maoni wajumbe walihusika waziwazi
kupokea kiasi cha shilling 50,000; pia wengine walisafirishwa na magari
kuelekea katika mkutano wa kura za maoni na baadhi ya wagombea wa udiwani na
ubunge.
“Wajumbe wa kamati ya siasa na wasimamizi waliotumwa
katika kata ikiwamo kata ya Bondeni alionekana wazi kuendesha kampeni na kutoa
maelekezo kwa wajumbe kumpigia kura mgombea Saashisha Mafue,” alisema
mwanachama huyo wa CCM.
Wanachama hao wanadai kuwa kutokana na dosari hizo ni
wazi kwamba zimeshusha hadhi ya chama chao kwa watanzania hatua ambayo inaweza kuwa na athari katika
kupeleka maendeleo kwa jamii inayowazunguka.
“Hebu fikiria katika kazta zote wajumbe wasio
halali waliingizwa kwa maelekezo ya
makatibu kata. Baadhi ya nafasi za wajumbe
waliokufa zilijazwa bila kufuata
utaratibu na baadhi ya wajumbe walipiga kura mara mbili, inaleta picha gani kwa
jamii?” alisema mwanachama wa CCM.
Akizungumza kwa njia ya simu Katibu wa CCM wilaya ya
Hai Hamis Mkaruka Kura alikiri kumsimamisha
Katibu Kata wa Machame Kaskazini baada ya kukiuka utaratibu baada ya
kuandika barua makanisani na misikitini kuhimiza waumini wamchague Saashisha
Mafuwe.
“Uchaguzi ulienda vizuri tu; sasa wanapodai kuwa
makatibu kata waliharibu kura za maoni kwa kuwa wapiga kampeni sio kweli; wanatokana katika vyumba vya
kupigia kura wakati wao ni wasimamizi, mengine ni hearsay,” alisema Katibu
huyo.
Katibu huyo aliongeza kusema tuhuma za rushwa ni mambo
ya kusikia kwani hadi sasa hajaletewa ripoti yoyote ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu vitendo vya rushwa wakati wa kura za
maoni wilaya ya Hai zilipofanyika.
Mgombea ubunge wa Jimbo hilo Saashisha Mafuwe ambaye
yupo katika kinyang’anyiro ndani ya chama katika nafasi hiyo alipotafutwa
kuzungumzia sakata hilo alikata kuzungumza akisema mambo yote chama ndicho
kinasimamia.
“Kwa sasa siwezi kusema lolote; kama unataka kuhusu
hayo kawaone chama watakueleza mimi kwa
sasa hapana,” alisema Mafuwe.
Kwa upande wake Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro
Mussa Chaulo alisema hadi sasa hajapokea taarifa yoyote ya vitendo vya rushwa
kutoka wilaya ya Hai kwani yupo nje ya ofisi kwa majuma mawili.