Hiki ni kisa cha kweli kilichomkuta kijana James mkazi wa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro…Nani alimsaliti kijana huyu mwenye umri wa miaka 37 afike hapo alipofikia? ANKO TUNUNU anaanza katika sehemu ya kwanza ya makala haya…
Tulipokuwa shuleni tulikuwa tukifundishwa
methali, vitendawili, misemo na mambo kadha wa kadha. Katika kipengele cha
methali miongoni mwao ilikuwa ni “Hujafa, Hujaumbika”.
Maana yake halishi ni kwamba mwili wa binadamu
unaweza kubadilika kimaumbile wakati wowote angali akiwa hai.
Hivyo basi haifai kwa sababu yoyote ile
kumcheka, kumdhihaki au kumkejeli mtu ambaye ana ulemavu wa kiungo mwilini
mwake.
Aliyekufa ndio amekamilika, safari yake
imefika mwisho. Mfuatiliji wa makala haya utakubaliana name na methali hii kwa
asilimia mia moja, utapofuatilia kisa hiki cha kweli kilichompata kijana
anayefahamika kwa jina la James Severin Mushi (37) mkazi wa Moshi katika mkoa
wa Kilimanjaro.
Watu wengi hupewa sifa na heshima
wanazostahili wakishakufa.
Wakati wa uhai wao watu huwachukulia
"poa", hawautambui au kuuthamini mchango wao mpaka wakishakufa na
pengo lao kuonekana.
Watu wachache sana katika historia
walifanikiwa "kuumbika" angali wakiwa hai.
Kwa haraka watu wanaokuja kichwani ni kama
Nelson Mandela, Michael Jackson, Steven Hawkings, Muhammad Ali na wengineo.
Wapo pia wenye bahati zaidi ambao wanapewa
tuzo za heshima sana au kupendwa na mamilioni ya watu angali wakiwa hai kama
Barak Obama, Pele, Beyonce na kadhalika.
Kisa hiki cha kweli cha kijana James kinaanzia
katika kivuko cha waenda kwa miguu cha Karanga-Magereza mjini Moshi mnamo
Aprili 2003 majira ya saa 11 jioni wakati akitoka shule.
Wakati huo alikuwa akisomea katika shule ya
Ufundi ya Moshi masuala ya ufundi bomba (Plumbing).
James anasema, “Nakumbuka ilikuwa siku ya
Ijumaa mida ya saa 11 jioni katika kivuko cha waenda kwa miguu eneo la Karanga
nikiwa na baiskeli basi lilinigonga.”
Muathirika huyo ambaye kwa sasa hana miguu
yake ya asili, alijikuta akiwa katika Hospitali ya KCMC iliyopo mjini Moshi
akiwa kwenye vitanda vya hospitali hiyo huku maumivu makali yakiendelea katika
mwili wake.
James anasema machozi yalizidi kutoka baada ya
kugundua kuwa maumivu makali sio pekee yamesababishwa na ajali kama ajali bali
ni baada ya taa ya mwili (macho) kuangaza katika mwili wake na kujikuta hana
miguu yote miwili.
“Baada ya kupelekwa hospitalini na kufika huko
miguu ilikuwa haina uwezo tena wa kutibika isipokuwa kukatwa…machozi yalinitoka
sikujua la kufanya,” anasimulia James.
ITAENDELEA…