Jeshi la Polisi limezua gumzo usiku wa kuamkia leo baada ya kulizingira Kanisa la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, wakati wa ibada ya maombi ya usiku maarufu kama mkesha.
Tukio hilo lililotokea majira ya saa nne za usiku, wa tarehe 2 Juni 2025 katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam lilipo kanisa hilo ambapo hatua hiyo imeibua maswali mengi miongoni mwa waumini na watanzania kwa ujumla kuhusu dhamira na ujumbe ulioambatana na hatua hiyo ya vyombo vya dola.
Kulishuhudiwa polisi wakiwasili kwa magari kadhaa na kuimarisha ulinzi nje ya majengo ya kanisa hilo, hatua ambayo iliwafanya waumini wengine kusalia ndani na wengine nje ya kanisa hilo.
Hayo yanajiri kukiwa na taarifa za kanisa lake kufungiwa kuendesha ibada zake na mamlaka za serikali jambo ambalo amelikanusa mapema leo tarehe 3 Juni 2025.
Kwa upande wa waumini na wanaharakati wa haki za binadamu, hatua hiyo inaweza kutafsiriwa kama kuingilia uhuru wa kuabudu, jambo ambalo linaweza kuleta taswira hasi kwa serikali katika macho ya umma na kimataifa. Katika tukio hilo kuamkia la usiku kulisikika waumini wakisema uhuru wao wa kuabudu unazuiwa huku wakirusha mawe kuwaondoa askari hao.
Kwa kuwa Askofu Gwajima ni kiongozi wa dini na pia mbunge wa Kawe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ambaye kwa sasa ameshikilia msimamo wa kusema ukweli kuhusu vikundi vya watekaji, tukio hilo linaingiza mchanganyiko wa dini, siasa, na usalama.
Hii inatoa taswira ya hali tete ambapo mipaka kati ya mihimili hiyo mitatu inaanza kuchanganyika. Mchungaji Dickson Kabugumila amekaririwa akisisitiiza hali ambayo itatokea ndani ya Chama cha Mapinduzi mwaka huu.
Kufuatia tukio la Polisi kuzingira Kanisa la Ufufuo na Uzima; Rais wa Chama cha Wanasheria nchini Tanganyika Law Society Boniface Anyisile Mwabukusi ameweka bayana kuwa kwa sasa hawatakiwi tena kujifanya hawamjui anayewateka watu hapa nchini.
Wakili Mwabukusi ameandika katika ukurasa wa Facebook, maneno haya “Mtekaji amepata ujasiri yuko tayari kufanya chochote hadharani kuzuia tusipige kelele za Utekaji. Sisi tunaotekwa na kupotelewa na ndugu tuendelee kumuonea Aibu na upuuzi wake huu? La hasha ......Kanisa Linashambuliwa, kwa Kusimama katika Kweli. Tukatae dhuluma hii.Tuna haki ya kujilinda...tuna haki ya kulinda ndugu zetu na rafiki zetu....Usikae kimya tena"
Awali Askofu Gwajima alithibitisha kuhusu Askari wa Jeshi la Polisi kuzingira kanisa lake wakati wa usiku wakiendelea na huduma Kanisa hapo.
Baadhi wa wafuatiliaji wa masuala ya siasa za ndani na nje ya Tanzania wanasema Katika mazingira ya sasa, sauti za viongozi wa CCM kuhusu masuala nyeti zimesikika kwa nadra sana au hazipo kabisa. Badala yake, sauti za kejeli, vitisho, au ukosoaji wa upinzani ndizo zinazopewa kipaumbele ikiwa ni ishara ya chama kilichojikita zaidi katika kujilinda kuliko kuwatumikia wananchi.
Hata hivyo Katibu wa zamani wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliwahi kutoa tahadhari kuhusu uwepo wa serikali za kihuni ndani ya mamlaka kamili katika chama au serikali iliyopo madarakani.
Kwa upande wake mwanaharakati na mwandishi wa habari mwandamizi Cyprian Musiba aliwahi kukaririwa akikitahadharisha Chama cha Mapinduzi kuhusu mabadiliko ya dunia ambayo kwa sasa kuna serikali za kihuni dunia ambazo zinataka vyama vyote vilivyokaa madarakani kwa muda mrefu kuondolewa.
Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa bado kina mtandao mpana wa kisiasa na miundombinu ya uongozi nchini, ukimya wake katika masuala nyeti unatoa ishara hatari: kwamba chama hicho huenda hakina tena msukumo wa kisiasa wa awali wa kutetea wanyonge, bali kimegeuka kuwa sehemu ya mfumo unaotajwa kuwa wa kukandamiza sauti mbadala. Wananchi wanaanza kuhoji — si tu kwa kelele mitandaoni, bali kwa ukimya wa kutojihusisha, kuonyesha kukata tamaa, au kutafuta mabadiliko nje ya mfumo rasmi wa kisiasa.