✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨✨
Viongozi wa kimila mkoani Kilimanjaro wameanza mchakato wa
kumpa tuzo maalum ya heshima Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kazi alizozifanya katika
kipindi cha miaka mitano ndani ya uongozi wake.
Akizungumza hivi karibuni na Waandishi wa habari Mwenyekiti
wa Machifu Tanzania Frank Marealle, alisema katika kipindi cha miaka mitano ya
kwanza ndani ya uongozi wake Rais Magufuli ameweza kuifikisha nchi katika
uchumi wa kati hivyo anastahili kupewa tuzo ya heshima.
“Jambo ambalo tumeona kumuandalia ni tuzo ya heshima Rais
wetu, kwanza jambo la kwanza hakuweza kuwafungia wananchi wake majumbani
(lockdown) kutokana na virusi vya ugonjwa wa Covid-19 vilipotokea, endapo
angefanya hivyo tungekuwa na hali mbaya ya kiuchumi, ikiwemo wafanyakazi wa
Umma na taasisi binafsi, athari yake ingekuwa kubwa kupita kiasi,”anasema Chifu
Marealle.
Marealle aliongeza kuwa anamshukuru Rais Magufuli kwa kutilia
mkazo kwa nguvu zote suala la kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19
huku wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji mali na ujenzi wa Taifa.
Chifu kutoka Wilaya ya Siha Godfrend Kileo, alimwelezea Rais
Dkt. Magufuli kuw ani mchapaka kazi asiyechoka hususani katika uchumi ikiwemo
ukusanyaji wa kodi, uboreshaji wa miundombinu, ujenzi wa viwanda,
urejeshwaji wa fedha zilizoibiwa kutoka vyama vya ushirika, urahisi wa
mikopo inayotolewa na serikali kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Kwa upande wake Katibu anayeshughulikia maandalizi ya Tuzo ya
Rais Joseph Msele, alisema hadi sasa
maandalizi hayo yamefikia asilimia 90 hivyo anamuomba Rais Dkt. Magufuli
akubali kuja kuipokea tuzo hiyo ya heshima iliyoandaliwa na wazee hao.
Alisema msukumo na dhamira ya uandaaji wa tuzo hiyo ni
kutokana na utendaji kazi wake kwa
kuweza kuifikisha nchi katika Uchumi wa kati mwaka 2020.
Msele alisema katika Mkoa wa Kilimanjaro yapo mambo mengi
ambayo ameyatekeleza ndani ya miaka mitano ikiwemo ufufuaji wa Reli, ujenzi wa viwanda vipya, barabara pamoja
na ujenzi wa vituo vya afya.
Aidha Msele alisema sherehe hizo zitafanyika katika uwanja wa
Chuo Kikuu cha Ushirika (MoCU) ambapo mbali na wazee hao kumpatia tuzo ya
heshima Rais Dkt. Magufuli pia Mama Janeth Magufuli naye atakabidhiwa tuzo huku
akitoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi kuja
kushuhudia tukio hilo la kihistoria pale tarehe rasmi itakapotangazwa.